Ezekieli 28

Ezekieli 28

Unabii juu ya mfalme wa Tiro

1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

2“Wewe mtu! Mwambie mfalme wa Tiro kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:

Wewe una kiburi cha moyo,

na umesema kwamba wewe ni mungu,

kwamba umekalia kiti cha enzi cha miungu,

umekaa mbali huko baharini.

Lakini, wewe ni binadamu tu wala si Mungu,

ingawa wajiona kuwa una hekima kama Mungu.

3Haya! Wewe wajiona mwenye hekima kuliko Danieli,

wadhani hakuna siri yoyote usiyoijua.

4Kwa hekima na akili yako

umejipatia utajiri,

umejikusanyia dhahabu na fedha

ukaziweka katika hazina zako.

5Kwa busara yako kubwa katika biashara

umejiongezea utajiri wako,

ukawa na kiburi kwa mali zako!

6Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:

Kwa vile unajiona mwenye hekima kama Mungu,

7basi nitakuletea watu wageni,

mataifa katili kuliko yote.

Wataharibu fahari ya hekima yako

na kuchafua uzuri wako.

8Watakutumbukiza chini shimoni,

nawe utakufa kifo cha kikatili kilindini mwa bahari.

9Je, utajiona bado kuwa mungu

mbele ya hao watakaokuua?

Mikononi mwa hao watakaokuangamiza,

utatambua kuwa wewe ni mtu tu, wala si Mungu!

10Utakufa kifo cha aibu kubwa

mikononi mwa watu wa mataifa.

Ni mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Kuanguka kwa mfalme wa Tiro:

11Tena neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

12“Wewe mtu! Imba wimbo wa maombolezo juu ya mfalme wa Tiro. Mwambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:

Wewe mfalme wa Tiro ulikuwa upeo wa ukamilifu;

ulijaa hekima na uzuri kamili.

13Ulikaa Edeni, bustani ya Mungu.

Ulipambwa kwa kila namna ya johari,

akiki, topazi, yaspi, zabarajadi, berili,

sardoniki, johari ya rangi ya samawati, almasi na zumaridi.

Ulikuwa na mapambo ya dhahabu.

Yote uliwekewa tayari siku ulipoumbwa.

14Nilimteua malaika kukulinda,[#28:14 Makala ya Kiebrania si dhahiri.]

uliishi katika mlima wangu mtakatifu

na kutembea juu ya vito vinavyometameta.

15Uliishi maisha yasiyo na lawama,

tangu siku ile ulipoumbwa,

hadi ulipoanza kufanya uovu.

16Ufanisi wa biashara yako

ulikujaza dhuluma, ukatenda dhambi.

Kwa hiyo nilikufukuza kama kinyaa,

mbali na mlima wangu mtakatifu.

Na yule malaika aliyekulinda

akakufukuzia mbali na vito vinavyometameta.

17Ulikuwa na kiburi

kwa sababu ya uzuri wako.

Uliharibu hekima yako kwa sababu ya fahari yako.

Nilikubwaga chini udongoni,

nikakufanya kuwa kioja kwa wafalme.

18Kwa wingi wa uhalifu wako

na udanganyifu katika biashara yako

ulipachafua mahali pako pa ibada;

kwa hiyo nilizusha moto kwako, nao ukakuteketeza,

nami nikakufanya majivu juu ya nchi,

mbele ya wote waliokutazama.

19Wote wanaokufahamu kati ya mataifa

wameshikwa na mshangao juu yako.

Umeufikia mwisho wa kutisha,

na hutakuwapo tena milele.”

Unabii juu ya Sidoni

20Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:[#28:20-26 Taz Yoe 3:4-8; Zek 9:1-2; Mat 11:21-22; Luka 10:13-14]

21“Wewe mtu! Ugeukie mji wa Sidoni,

22utoe unabii juu yake kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:

Mimi nitapambana nawe Sidoni,

na kuudhihirisha utukufu wangu kati yako.

Nitakapotekeleza hukumu zangu juu yako

na kukudhihirishia utakatifu wangu,

ndipo utakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.

23Nitakupelekea maradhi mabaya

na umwagaji damu utafanyika katika barabara zako.

Utashambuliwa kwa upanga toka pande zote

na watu wako watakaouawa, watakuwa wengi.

Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

Waisraeli watapata baraka

24Mungu asema, “Mataifa jirani na Waisraeli ambayo yalikuwa yanawaudhi hayataweza tena kuwaumiza Waisraeli kama vile kwa miiba na michongoma. Ndipo watakapojua ya kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu.

25“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawakusanya na kuwaleta Waisraeli kutoka katika mataifa yote ambamo walitawanywa. Hivyo nitawafanya watu wa mataifa waone kuwa mimi ni mtakatifu. Watu wa Israeli wataishi katika nchi yao ambayo mimi nilimpa mtumishi wangu Yakobo.

26Watakaa humo salama salimini; watajenga nyumba na kupanda mizabibu. Wataishi bila hofu maana mataifa jirani zao ambayo yaliwaudhi, mimi nitayaadhibu. Hapo watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania