Zaburi 141

Zaburi 141

Hatari za tamaa mbaya

1Nakuita, ee Mwenyezi-Mungu,

uje haraka kunisaidia!

Uisikilize sauti yangu wakati ninapokuita!

2Sala yangu uipokee kama ubani;[#Taz Ufu 5:8]

niinuapo mikono yangu kwako unikubali kama tambiko ya jioni.

3Ee Mwenyezi-Mungu ukilinde kinywa changu,

uweke ulinzi mlangoni mwa mdomo wangu.

4Unikinge nisielekee kufanya mabaya,

nisijishughulishe na matendo maovu;

nisijiunge na watu watendao mabaya,

wala nisishiriki kamwe karamu zao.

5Afadhali mtu mwema anipige kunionya;

lakini sikubali kamwe kusifiwa na wabaya,

maana nasali daima dhidi ya maovu yao.

6Wakuu wao watakapopondwa miambani,

ndipo watatambua maneno yangu yalikuwa sawa.

7Mifupa yao itatawanywa mdomoni pa Kuzimu

kama kuni zilizopasuliwa vipandevipande!

8Bali mimi nakutegemea, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu;

ninakimbilia usalama kwako, usiniache hatarini.

9Unikinge na mitego waliyonitegea,

uniepushe na matanzi ya hao watu waovu.

10Waovu wanaswe katika mitego yao wenyewe,

wakati mimi najiendea zangu salama.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania