Zaburi 40

Zaburi 40

Utenzi wa sifa

1Nilimngojea Mwenyezi-Mungu kwa uvumilivu,

akanielekea na kukisikia kilio changu.

2Aliniondoa katika shimo la hatari,

alinitoa katika matope ya dimbwi,

akanisimamisha salama juu ya mwamba,

na kuziimarisha hatua zangu.

3Alinifundisha wimbo mpya,

wimbo wa sifa kwa Mungu wetu.

Wengi wataona na kuogopa,

na kumtumainia Mwenyezi-Mungu.

4Heri mtu anayemtumainia Mwenyezi-Mungu;

mtu asiyejiunga na watu wenye majivuno,

watu waliopotoka kwa kuabudu miungu ya uongo.

5Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umetufanyia mengi ya ajabu,

na mipango yako juu yetu haihesabiki;

hakuna yeyote aliye kama wewe.

Kama ningeweza kusimulia hayo yote,

idadi yake ingenishinda.

6Wewe hutaki tambiko wala sadaka,[#Taz Ebr 10:5-7]

tambiko za kuteketeza wala za kuondoa dhambi;

lakini umenipa masikio nikusikie.

7Ndipo niliposema: “Niko tayari;

ninayotakiwa kufanya yameandikwa katika kitabu cha sheria;

8kutimiza matakwa yako, ee Mungu wangu ni furaha yangu,

sheria yako naishika kwa moyo wangu wote!”

9Nimesimulia habari njema za ukombozi,

mbele ya kusanyiko kubwa la watu.

Kama ujuavyo ee Mwenyezi-Mungu,

mimi sikujizuia kuitangaza.

10Sikuuficha moyoni mwangu ukombozi ulionijalia,

nimetangaza daima kuwa wewe ni mwokozi mwaminifu;

sikulificha kusanyiko kubwa la watu

fadhili zako na uaminifu wako.

11Ee Mwenyezi-Mungu, usininyime huruma yako!

Fadhili zako na uaminifu wako vinihifadhi daima.

Sala ya kuomba msaada

(Zaburi 70)

12Maafa yasiyohesabika yanizunguka,

maovu yangu yanikaba hata siwezi kuona;

ni mengi kuliko nywele kichwani mwangu,

nami nimevunjika moyo.

13Upende ee Mwenyezi-Mungu kuniokoa;

ee Mwenyezi-Mungu, uje haraka kunisaidia.

14Wanaonuia kuniangamiza,

na waaibike na kufedheheka!

Hao wanaotamani niumie,

na warudi nyuma na kuaibika!

15Hao wanaonisimanga,

na wapumbazike kwa kushindwa kwao!

16Lakini wote wale wanaokutafuta

wafurahi na kushangilia kwa sababu yako.

Wapendao wokovu wako,

waseme daima: “Mwenyezi-Mungu ni Mkuu!”

17Mimi ni maskini na fukara, ee Bwana;

lakini ee Bwana wewe wanikumbuka.

Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu;

uje, ee Mungu wangu, usikawie!

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania