1 Wamakabayo 1

1 Wamakabayo 1

Aleksanda Mkuu

1Aleksanda wa Makedonia, mwana wa Filipo, aliyetoka nchini Kitimu, alimshambulia na kumshinda Dario, mfalme wa Persia na Media, akawa mfalme badala yake. Wakati huo Aleksanda alikwisha kuwa mfalme wa Ugiriki.[#1:1 Jina ambalo awali lilitaja kisiwa cha Kupro ambacho kiko katika Bahari ya Mediteranea, lakini wataalamu wa Biblia wanaona kwamba hapa yahusu nchi ya Makedonia.]

2Alipigana vita vingi, akateka miji yenye ngome na kuwaua wafalme wa nchi hizo.

3Akasonga mbele hadi miisho ya dunia, akayateka mataifa yasiyohesabika. Hatimaye, ulimwengu wote ulipotulia chini ya utawala wake, aliona fahari kupita kiasi, akajisikia mkuu.[#1:3 Maneno yanayoashiria kwamba vita vilienea kila mahali.]

4Aliunda jeshi lenye nguvu kupindukia, akatawala nchi, mataifa, na wakuu wao; akawalazimisha kulipa kodi kwake.

5Kisha, mfalme Aleksanda akawa mgonjwa, akahisi kwamba kifo kimekaribia.

6Basi, akawaita maofisa wake maarufu ambao walikuwa wamelelewa pamoja naye tangu utoto wake, akawagawia milki yake wakati angali hai.

7Aleksanda alipofariki dunia alikuwa ametawala kwa miaka kumi na miwili.[#1:7 Aleksanda Mkubwa alikufa mwaka 323 K.K.]

8Maofisa wake wakaanza kutawala, kila mmoja katika eneo lake.

9Wote hao walitawazwa wafalme, Aleksanda alipokufa, na wazawa wao wakawa wafalme baada yao kwa miaka mingi; wakasababisha maovu chungu nzima duniani.

Antioko Epifane na Wayahudi wasiojali sheria

(2 Mak 4:7-17)

10Mmoja wa wazawa hao ni yule mwovu, Antioko Epifane, mwana wa mfalme Antioko. Kabla ya kutawazwa kuwa mfalme mwaka 137 wa enzi ya Wagiriki, Antioko Epifane alikuwa mateka huko Roma.[#1:10 Huyo alikuwa miongoni mwa mateka waliokabidhiwa kwa Waroma na baba yake mnamo mwaka 189 K.K.; #1:10 Ni sawa na 175 K.K.]

11Wakati huo kikazuka kikundi cha Wayahudi wasiojali sheria huko Israeli, ambacho kiliwapotosha watu wengi, kikisema: “Twende kufanya mkataba na jirani zetu wa mataifa mengine, maana tangu tulipojitenga nao tumepata misiba mingi.”[#1:11 Sheria ilikataza kufanya mikataba ya kimataifa kwa kuhofia kutiwa unajisi kidini. Rejea Kut 23:32-33; 34:12-16; Ezra 9:1-2.]

12Pendekezo hilo likawapendeza watu,

13na baadhi yao wakamwendea mfalme kwa hamaki. Mfalme akawaruhusu kuzifuata mila na desturi za watu hao wa mataifa mengine.

14Basi, wakajenga uwanja wa michezo mjini Yerusalemu kwa mtindo wa mataifa mengine.[#1:14 Huo ulikuwa mahali kiini pa utamaduni na michezo ambapo vijana walifunzwa utamaduni wa Kigiriki.]

15Wakaondoa miilini mwao alama za kutahiriwa, na kuliacha agano takatifu. Walijiunga na watu hao wa mataifa mengine, wakajizamisha katika kutenda maovu.[#1:15 Kujisingizia kwamba hawakutahiriwa ilikuwa sawa na kuvunja lile agano. Rejea Mwa 17:9-14; 1Kor 7:18.; #1:15 Yaani walikubali pia desturi za kidini za hayo mataifa.]

Antioko aishambulia Misri

16Alipoona utawala wake umeimarika, Antioko aliazimu kuiteka Misri na kuwa mfalme wa nchi hiyo pia, licha ya Siria.

17Kwa hiyo akaivamia Misri kwa jeshi lake kali lenye magari ya kukokotwa, tembo, askari wapandafarasi, na msururu wa vyombo vya baharini.[#1:17 Hao walitumiwa vitani. Rejea 1Mak 6:30,34-37.]

18Vita vilipopamba moto, Tolemai, mfalme wa Misri, akarudi nyuma na kukimbilia mbali. Wengi wa askari wake walijeruhiwa na kuuawa.

19Miji yenye maboma ilikamatwa, na nchi ya Misri ikatekwa.

Antioko awadhulumu Wayahudi

20Baada ya kuiteka Misri, Antioko, pamoja na jeshi lake lenye nguvu, aliikabili nchi ya Israeli, 143, akawasili mjini Yerusalemu.[#1:20 Ni sawa na 169 K.K.]

21Kwa majivuno aliingia hekaluni na kujichukulia madhabahu ya tambiko, kinara cha taa na vifaa vyake vyote.

22Pia alitwaa meza ya mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, vikombe vitakatifu, mabakuli, vyetezo vya dhahabu, pazia, na mataji. Akayabandulia mbali mapambo ya dhahabu katika ukuta wa mbele wa hekalu.

23Akavichukua vyombo vya fedha na vya dhahabu na vya thamani. Hali kadhalika, akatwaa na vitu vyote vya tunu alivyovikuta vimefichwa.[#1:23 Mahekalu ya hapo kale yalitumiwa pia kuweka na kuhifadhi kiasi kikubwa cha fedha, hata za watu wa kawaida (2Mak 3:4-13; 5:16).]

24Akabeba hivyo vyote na kwenda navyo nchini kwake. Alikuwa amemwaga damu nyingi sana, na akawa anajigamba sana juu yake.

25Kilio kilikuwa kikubwa katika Israeli yote;

26watawala na wazee walilia kwa huzuni

wasichana na wavulana wakanyong'onyea;

uzuri wa wanawake ukatoweka.

27Kila bwanaharusi aliomboleza;

kila bibiarusi chumbani mwake alilia.

28Nchi ilitetemeka kwa ajili ya wakazi wake,

na jamii yote ya Yakobo ilivikwa fedheha.

29Miaka miwili baadaye, mfalme Antioko alimtuma mtozaushuru mkuu kwa miji ya Yudea. Huyo aliwasili Yerusalemu, akisindikizwa na jeshi kubwa la askari.[#1:29 Yapata mwanzo wa kiangazi cha mwaka 167 K.K.; #1:29 Hapa yahusu Apolonio. Taz 2Mak 5:24.]

30Lugha yake ilikuwa tamu, lakini yenye hila. Kwani, mji wote ulipomwamini, ghafla akauvamia na kuupiga vibaya sana. Aliwaua watu wengi wa Israeli,

31akauteka na kuuchoma moto mji wa Yerusalemu, akazibomoa nyumba na kuta za kila upande,

32akawachukua mateka wanawake, watoto, na mifugo.

33Halafu Antioko na majeshi yake wakajenga kuta ndefu na minara imara kuuzunguka mji wa Daudi; ikawa ngome yao.[#1:33 Wakati ule waliuita Mji wa Daudi eneo la juu la magharibi ya hekalu.]

34Kisha akaweka hapo watu ovyo, wasiojali sheria, walinde. Hao waliimarisha ulinzi wao;

35walikusanya na kuhifadhi silaha na chakula, wakaokota nyara zote walizoteka Yerusalemu, wakaziweka ngomeni. Ngome hiyo ilikuwa tishio kubwa kwa mji wa Yerusalemu.

36Ilikuwa tishio kubwa kwa hekalu,

hatari mbaya ya kudumu kwa Israeli.

37Watu wasio na hatia waliuawa kandokando ya madhabahu;

mahali patakatifu pakatiwa unajisi hivyo.

38Wakazi wa Yerusalemu wakakimbia kwa sababu yao,

mji ukawa makao ya wageni,

ukawa wa kigeni kwa watu wake,

na watoto wake wakauacha.

39Hekalu lake likawa tupu kama jangwa;

sikukuu zake zikageuka kuwa maombolezo,

furaha ya Sabato zake ikageuka kuwa lawama,

na heshima yake ikawa fedheha.

40Aibu ya kuanguka kwake ililingana na utukufu wake wa awali;

na fahari yake ikageuka kuwa maombolezo.

41Kisha, mfalme Antioko akaandika agizo kwa watu wote katika milki yake wawe taifa moja,

42na kwamba kila mtu aachilie mbali mila na desturi zake.[#1:42 Kwa agizo au ilani hiyo, hali ya kidini na kitamaduni ya Wayahudi ilitiwa katika hatari ya kuangamizwa. Taz 1Mak 1:13.]

43Watu wote wa mataifa mengine waliipokea amri hiyo ya mfalme. Watu wengi hata Waisraeli wakaifuata dini yake kwa furaha; wakatambika kwa vinyago vya miungu na kuitia unajisi siku ya Sabato.[#1:43 Ilihusu ibada kwa mungu Zeu Olimpia. Taz 2Mak 6:2 maelezo.]

44Naye mfalme akawatuma watu kupeleka barua Yerusalemu na kwenye miji ya Yudea, akiamuru kwamba watu wafuate mila na desturi hizo za kigeni.

45Aliwakataza wasitoe tambiko za kuteketezwa, tambiko za nafaka wala sadaka za vinywaji hekaluni. Aliamuru Sabato na sikukuu ziwe siku za kawaida.

46Watu waliamriwa kulitia najisi hekalu na wahudumu wake,

47kujenga madhabahu, mahekalu na mahali patakatifu kwa ajili ya vinyago vya miungu, kutoa sadaka ya nguruwe na wanyama najisi,

48na kuwaacha wana wao bila kutahiriwa. Walitakiwa kujitia unajisi kwa kila namna waliyoweza,

49ili waisahau sheria na kubadili mila na desturi zao zote.

50Yeyote aliyekaidi amri ya mfalme alihukumiwa kifo.

51Licha ya kuieneza amri hiyo katika milki yake yote, mfalme Antioko aliwateua wakaguzi wa kusimamia utekelezaji wake, akaamuru watu wa miji yote ya Yudea watoe tambiko kwa miungu.

52Wengi wa Wayahudi, yaani wale walioiasi sheria, waliwatii wasimamizi hao. Hivi wakaitia unajisi nchi kwa uovu wao,

53na kuwafanya watu waaminifu wa Israeli watoroke na kujificha popote walipoweza.

54Siku ya kumi na tano ya mwezi wa Kislevu, mwaka 145, mfalme Antioko aliisimamisha lile Chukizo Haribifu juu ya madhabahu kuu ya sadaka za kuteketezwa hekaluni, na vimadhabahu vya miungu vikajengwa katika miji yote ya Yudea,[#1:54 Ni sawa na 167 K.K. (tarehe 8 Desemba).]

55wakawa wanafukiza ubani milangoni mwa kila nyumba na mitaani.

56Vitabu vyovyote vya sheria walivyoviona walivichanachana na kuvichoma moto.

57Yeyote aliyeshikwa ana kitabu cha agano au anaifuata sheria, aliuawa kwa amri ya mfalme.[#1:57 Hapa yahusu vitabu vya Pentateuko, yaani vitabu vitano vya kwanza vya Biblia.]

58Mwezi hata mwezi, watu hao waovu walitumia mabavu dhidi ya Waisraeli waliokamatwa katika miji mbalimbali.

59Siku ya ishirini na tano ya mwezi huo huo, watu hao walitoa tambiko katika kimadhabahu kilichosimamishwa juu ya madhabahu kuu ya sadaka za kuteketezwa hekaluni.[#1:59 Siku hiyo ilikuwa siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa mfalme.]

60Kwa mujibu wa amri iliyotolewa, waliwaua wanawake wote waliowaruhusu watoto wao kutahiriwa,

61na jamaa zao na wale waliowatahiri watoto hao; na watoto wenyewe wakawanyonga kwa kuwaning'iniza shingoni mwa mama zao.

62Hata hivyo, wengi katika Israeli walisimama imara, wakaamua kwa dhati kutokula chakula najisi.

63Walikuwa tayari kufa kuliko kuvunja agano takatifu na kula chakula najisi - na kwa kweli, wengi waliuawa.

64Ghadhabu kubwa iliwapata Waisraeli.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania