1 Wamakabayo 12

1 Wamakabayo 12

Ushirika na Roma na Sparta

1Yonathani alipoona mambo yanamwendea vizuri, akachagua wajumbe na kuwatuma Roma kwenda kufufua na kuthibitisha urafiki na Waroma.

2Aidha alipeleka barua zenye ujumbe kama huo Sparta na mahali pengine.[#12:2 Mji wa Ugiriki ambao una historia ya kijeshi, ulikuwa maarufu katika nyakati zilizopita. Unaitwa pia Lakedemonia.]

3Hao wajumbe wakaenda Roma, ambako walikaribishwa katika Baraza Kuu la Wazee. Wakasema: “Yonathani, kuhani mkuu, na taifa la Wayahudi wametutuma kuja kufufua urafiki na ushirikiano ule wa awali na Roma.”[#12:3 Kule kumtaja kuhani mkuu mwanzoni kabisa mwa ujumbe huo kunadhihirisha kwamba kuhani mkuu alikuwa ndiye mwenye mamlaka makuu kwa Wayahudi wakati huo.]

4Waroma wakawapa barua za utambulisho kwa wakuu wa kila nchi ambayo wajumbe hao wangepita wakati wa kurudi Yudea, wakiomba wapatiwe usalama.

5Ifuatayo ni nakala ya barua ambayo Yonathani aliwaandikia Wasparta:

6“Kuhani Mkuu Yonathani, Baraza Kuu la Taifa, makuhani, na wananchi wote wa Yudea, kwa ndugu zetu wa Sparta: Salamu.

7Siku za nyuma, mfalme wenu Ario alimwandikia barua kuhani mkuu wetu, Onia, akieleza kwamba mataifa yetu haya mawili yana uhusiano, kama nakala iliyoambatishwa inavyoonesha.

8Onia alimpokea mjumbe wenu kwa heshima zote, na akajibu barua yenu hiyo iliyotangaza wazi urafiki na ushirika baina yetu.

9Na sasa, ingawa hatuna haja ya ushirika kama huo, kwa vile chimbuko la nguvu yetu ni vitabu vitakatifu tulivyo navyo,

10tumewaandikieni ili kufufua uhusiano wetu wa kindugu na kirafiki nanyi. Hatutaki kuvunja uhusiano; miaka mingi imepita sasa tangu mlipotupelekea barua yenu.[#12:10 Yahusu ile barua ya Ario I, ambayo inatajwa hapo juu (aya 20-23). Huyo alitawala tangu mwaka 309 mpaka 264 K.K.]

11Tunawakumbukeni daima kila upatikanapo wasaa: katika sikukuu zetu na siku nyingine za kufaa, katika sala na sadaka zetu, kama inavyotakiwa ndugu kukumbukana.

12Tena tunafurahi kwamba mmejipatia fahari.

13Lakini sisi tumekuwa tukikabiliwa na shida na matatizo na vita vya mara kwa mara, kwani mataifa jirani yamekuwa yakitushambulia.

14Wakati huo wa vita hatukutaka kuwasumbua nyinyi wala marafiki na washirika wetu wengine.

15Kwa vile msaada wetu watoka kwa Bwana, ambaye amewashinda adui zetu na kutuokoa na makucha yao.

16Hivi tumewachagua Numenio mwana wa Antioko na Antipateri mwana wa Yasoni, na kuwapeleka Roma kwenda kufufua urafiki na ushirika wetu na Waroma.

17Pia tumewaagiza wafike kwenu kuwasilisha salamu zetu na barua hii inayohusu ufufuaji wa uhusiano wetu wa kindugu.

18Tunatumaini kupata jibu kwa barua hii.”

19“Ifuatayo ni nakala ya barua yenu ya awali kwa Onia:

20“‘Mfalme Ario wa Sparta kwa kuhani mkuu Onia, salamu.[#12:20 Yahusu kuhani mkuu Onia I, ambaye alishika wadhifa wake kati ya mwaka 323 na 300 K.K.]

21Imeonekana katika maandishi fulani ya kuwa sisi Wasparta na nyinyi Wayahudi tunahusiana, na kwamba mataifa yetu yote mawili ni wazawa wa Abrahamu.

22Maadamu tumegundua hayo, tafadhali, tuleteeni taarifa juu ya hali yenu.

23Nasi tutawaandikieni kuwajulisha kwamba tupo tayari kuwashirikisheni mali yetu, pamoja na mifugo yetu, kama nanyi mtafanya hivyo. Tumewaagiza wajumbe wetu kuwaelezeni kinaganaga juu ya mambo hayo.’”

Kampeni za Yonathani na Simoni

24Ndipo Yonathani akapata habari kwamba maofisa wa Demetrio walikuwa wamekuja tena, na jeshi kubwa zaidi, kumshambulia yeye.

25Yonathani hakutaka kuwapa fursa ya kuivamia nchi yake. Kwa hiyo akaondoka Yerusalemu, akaenda kupambana nao katika eneo la Hamathi.[#12:25 Huu ulikuwa mji wa Siria upande wa kaskazini na hivyo nje ya eneo la Wayahudi.]

26Akapeleka wapelelezi kambini kwa maadui, wakarudi na kumwarifu ya kwamba maadui walikuwa wanafanya mipango kuwashambulia Wayahudi usiku.

27Hivi, jua lilipotua, Yonathani akawaamuru askari wake wote kukaa chonjo, silaha mkononi, tayari kwa shambulio lolote la ghafla saa za usiku. Pia aliwaweka askari walinzi kuzunguka kambi yote.

28Maadui waliposikia kwamba Yonathani na watu wake walikuwa wamejitayarisha kwa mapambano, wakaingiwa na hofu kubwa, wakakimbia na kuacha mioto inawaka kambini.

29Yonathani na watu wake waliona hiyo mioto ya kambini, lakini hawakutambua yaliyokuwa yametukia mpaka kesho yake asubuhi.

30Ndipo Yonathani akaondoka kuwafuata maadui. Lakini hakuweza kuwakuta kwa sababu walikuwa wamekwisha vuka mto Eleuthero.

31Basi, Yonathani akageuka, akashika njia ya pembeni na kuwashambulia Wazabadea, kabila moja la Waarabu. Aliwashinda, akateka mali yao.

32Halafu akaondoka hapo na kwenda Damasko, akipita kulikagua eneo lote la huko.

33Simoni naye aliondoka akapitia katika nchi ile akafika mbele hadi Askaloni na ngome za jirani. Halafu akageuka na kwenda Yopa, akautwaa mji huo kwa ghafla,

34maana alikuwa amesikia kwamba wenyeji wake walikuwa tayari kuwakabidhi ngome ya Yopa askari waliokuwa wametumwa na Demetrio. Simoni akaweka kikosi cha askari kuilinda ngome hiyo.

35Yonathani aliporejea, aliitisha mkutano wa wazee wa watu kufanya mipango ya kujenga maboma katika Yudea,

36kuongeza urefu wa kuta za Yerusalemu, na kujenga ukuta mrefu kati ya ngome na mji, ili kuitenga hiyo ngome, maadui washindwe kununua au kuuza chochote.

37Watu wakafanya kazi pamoja kuimarisha ukuta wa mji, kwa sababu sehemu ya ukuta wa upande wa mashariki ilikuwa imeanguka; aliitengeneza pia sehemu iliyoitwa Kafenatha.

38Simoni naye akaujenga upya mji wa Adida katika tambarare ya Shefela, akauimarisha na kuuwekea milango na mapingo.

Trifo amteka Yonathani

39Baada ya hayo, Trifo akafanya mbinu za kumpindua mfalme Antioko ili awe yeye mfalme wa Asia.

40Hata hivyo, aliogopa kwamba Yonathani asingekubaliana naye kuhusu mpango huo, na angeanzisha vita dhidi yake kuzuia jambo hilo. Hivi, Trifo akawa anatafuta kumkamata na kumuua; hivyo akaondoka, akaenda Beth-sheani.

41Lakini, Yonathani akaenda kumkabili huko Beth-sheani na askari waliochaguliwa 40,000.

42Trifo alipoona ukubwa wa jeshi la Yonathani, akaogopa kuanza uchokozi.

43Hivi, akampokea Yonathani kwa heshima zote, akamtambulisha kwa washauri wake wote, akampa zawadi, na kuwaagiza washauri wake na askari wake wamtii Yonathani kama walivyokuwa wanamtii yeye mwenyewe.

44Halafu akamwuliza Yonathani: “Kwa nini umewataabisha kiasi kikubwa hivyo hawa askari wako wakati ambapo hatupigani vita?

45Kwa nini usiwarudishe nyumbani? Chagua watu wachache wabaki nawe, na halafu unisindikize huko Tolemai. Nitakupatia mji huo wa Tolemai, pamoja na ngome nyinginezo, na askari, na maofisa wao wote. Halafu mimi nitakwenda zangu nyumbani. Hiyo ndiyo iliyonileta hapa.”

46Yonathani akaamini maneno hayo. Basi, kufuatana na hayo aliyosema Trifo, akawarudisha askari wake Yudea.

47Alijiwekea watu 3,000; 2,000 akawaacha Galilaya, na 1,000 tu wakafuatana naye.

48Lakini mara Yonathani alipoingia Tolemai, wakazi wake wakafunga milango ya mji, wakamkamata yeye na kuwaua wote aliokuwa amefuatana nao.

49Kisha Trifo akapeleka vikosi vya askari wa miguu na wapandafarasi Galilaya na kwenye Bonde la Yezreeli kwenda kuwaua askari wa Yonathani waliobaki.

50Hao askari Wayahudi wakahisi kwamba Yonathani alikuwa amekamatwa na kuuawa pamoja na wale waliokuwa wamefuatana naye. Hivi wakatiana moyo, wakajipanga kwa vita.

51Majeshi ya adui yaliposogea na kuona Wayahudi wamejipanga tayari kutetea maisha yao, wakarudi nyuma.

52Ndipo askari Wayahudi wakarejea Yudea salama, lakini wenye hofu. Taifa zima likaangua kilio kikubwa, kumlilia na kumwombolezea Yonathani na wenzake.

53Nayo mataifa yote ya jirani sasa yalijaribu kuwaangamiza Wayahudi. Walidhani kwamba Wayahudi hawakuwa na kiongozi tena wala msaidizi. Wakasema: “Ngoja tuwapige sasa na kufutilia mbali kumbukumbu yao duniani.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania