The chat will start when you send the first message.
1Gorgia akawachukua askari wa miguu 5,000 na wapandafarasi wenye uzoefu 1,000, akatoka nao usiku
2kwenda kulishambulia ghafla jeshi la Wayahudi; walioongoza njia walikuwa walinzi wa ngome ya Yerusalemu.
3Lakini Yuda aliugundua mpango huo, akaondoka na watu wake ili kulishambulia jeshi la mfalme kule Emau
4wakati Gorgia na vikosi vyake bado hawajarejea kambini.
5Basi, Gorgia na jeshi lake wakafika kwenye kambi la Yuda usiku huo. Hawakumkuta yeyote yule huko. Wakaanza kuwatafuta milimani, wakidhani kwamba walikuwa wametoroka.
6Kulipopambazuka, Yuda alitokea kwenye tambarare akiwa na watu 3,000, lakini hawakuwa na silaha za kuwaridhisha.
7Wakaliona jeshi kubwa la watu wa mataifa mengine, wenye uzoefu wa vita, wamejisheheneza silaha, na ngome yao imezungukwa na askari wapandafarasi.
8Lakini Yuda akawaambia watu wake, “Msihangaike juu ya ukubwa wa jeshi lao, wala msiogope watakaposhambulia.
9Kumbukeni jinsi wazee wetu walivyookolewa katika Bahari ya Shamu mfalme wa Misri alipokuwa anawafuatia na jeshi lake!
10Sasa na tumwombe Mungu atuonee huruma. Tusali ili alishike agano lake na wazee wetu, na hivi aliponde jeshi mbele yetu leo.
11Ndipo watu wote wa mataifa mengine watatambua kwamba kunaye mwenye kuwakomboa na kuwaokoa watu wa Israeli.”
12Hao watu wa mataifa mengine walipochungulia na kuona Yuda na watu wake wanawajia,
13wakatoka kambini mwao ili kupiga vita. Yuda na watu wake wakapiga tarumbeta
14na kuanza kushambulia. Maadui wakatawanyika na kukimbilia kwenye tambarare,
15na askari wao wote waliokuwa mstari wa nyuma wameuawa kwa upanga. Waisraeli wakawafukuza maadui hadi Gazara na tambarare za Idumea, mpaka Ashdodi na Yamnia. Adui 3,000 wakaangamia.[#4:15 Namna ya Kigiriki ya kuandika “Edomu”.]
16Halafu Yuda na kikosi chake wakaacha kuwafukuza maadui, wakarudi nyuma.
17Yuda akawaambia watu wake, “Msiwe na pupa ya mateka. Tunakabiliwa bado na mapambano.
18Gorgia na jeshi lake wapo hapo milimani, karibu nasi. Lazima tusimame imara na kumpiga adui. Baada ya ushindi, kila mmoja ataweza kuchukua mateka anayotaka.”
19Kabla Yuda hajamaliza kusema hayo, kikosi cha adui kikatokeza, kikivizia kutoka milimani.
20Mara kiligundua kwamba jeshi lake lilikuwa limefukuziwa mbali, na kwamba, kutokana na moshi waliouona, Wayahudi walikuwa wanalichoma moto kambi lake.
21Ndipo wakashikwa na hofu kubwa. Na walipoliona jeshi la Yuda limejipanga kwenye tambarare, tayari kwa vita,
22wote wakakimbilia nchi ya Wafilisti.
23Basi, Yuda akarudi na kuliteka kambi la adui; wakapata dhahabu na fedha nyingi, nguo za buluu na urujuani, na mali nyingi.
24Walipokuwa wanarudi kambini kwao, Wayahudi wakaimba utenzi wa sifa kwa Mungu:
“Kwa kuwa yeye ni mwema,
na huruma yake yadumu milele.”
25Hivi, Israeli ilifaidi wokovu mkubwa siku hiyo.
26Wale wanajeshi wa mataifa mengine walionusurika walimwendea Lisia na kumwarifu yote yaliyokuwa yametukia.
27Aliposikia hayo, Lisia alifadhaika na kuvunjika moyo, kwa vile Waisraeli hawakuwa wamepigwa kama alivyokuwa amekusudia wala hawakupatwa na yale aliyoamuru.
28Mwaka uliofuata, Lisia akakusanya jeshi la askari wa miguu 60,000 na wapandafarasi 5,000 ili kuwashinda Wayahudi.
29Wakaingia Idumea na kupiga kambi Beth-zuri. Yuda, pamoja na askari 10,000, akaja hapo kupambana nao.[#4:29 Mahali mwafaka kabisa kwa pambano, yapata kilomita 28 kusini mwa Yerusalemu, kuelekea Hebroni.]
30Yuda alipoona kuwa jeshi la adui lilikuwa lenye nguvu, akasali, akisema: “Usifiwe wewe, Mwokozi wa Israeli, uliyekomesha mashambulio ya lile jitu kwa mkono wa mtumishi wako Daudi, ukalitia jeshi la Wafilisti mikononi mwa Yonathani mwana wa Shauli na yule kijana mchukuasilaha zake.
31Sasa uyadhoofishe pia majeshi haya kwa mkono wa watu wako Israeli, uwafanye watu wake waone aibu juu ya askari wao wa miguu na wapandafarasi wao.
32Uwajaze woga, uyeyushe uhodari wa nguvu yao, watetemeke katika maangamizi.
33Uwaangushe chini kwa upanga wa wale wakupendao, na kuwawezesha wote walijualo jina lako wakusifu kwa nyimbo.”
34Ndipo vita vikaanza; katika mapambano, waliuawa watu 5,000 wa Lisia.
35Lisia alipoona jeshi lake linalemewa, na alipoona ujasiri na ushupavu wa Yuda na watu wake - ambao walionesha kwamba walikuwa tayari kuishi au kufa kuilinda hadhi yao - akarudi Antiokia. Huko akaandikisha askari wa kukodi, ili aende tena Yudea siku za mbele na jeshi kubwa zaidi.[#4:35 Kadiri ya 2Mak 11:13-14 pambano hili lilifuatiwa na mazungumzo kati ya wenye ugomvi.]
36Yuda na ndugu zake wakasema: “Sasa maadui zetu wameshindwa. Twende zetu Yerusalemu tukalitakase hekalu na kulitabaruku upya.”
37Basi, jeshi lote likakusanyika, likaenda kwenye mlima Siyoni.
38Huko watu wakakuta hekalu limeachwa ukiwa, madhabahu yake imetiwa unajisi, milango yake imechomwa moto, nyasi na vichaka vimeota katika nyua zake kama porini au milimani, na vyumba vya makuhani vimebomolewa.
39Hapo wakararua mavazi yao, wakalia na kuomboleza kwa huzuni kubwa, wakijitia majivu kichwani
40na kuanguka kifudifudi. Tarumbeta ilipopigwa kutoa alama, kila mmoja alimlilia Bwana.
41Halafu Yuda, akawaamuru baadhi ya askari wake wawashambulie watu waliokuwa ngomeni, wakati yeye analitakasa hekalu.
42Aliwachagua makuhani kadha waliostahili na walioshika sheria kiaminifu.
43Hao wakalitakasa hekalu, wakayachukua mawe yaliyokuwa yametiwa unajisi na kuyapeleka nje mahali pachafu.
44Wakajadiliana wafanye nini na madhabahu ya sadaka za kuteketezwa, ambayo ilikuwa imetiwa unajisi.
45Wakaamua afadhali kuibomoa, ili isibaki imesimama hekaluni na kuwaletea lawama kwa vile watu wa mataifa walikuwa wameitia unajisi. Basi, wakaibomoa madhabahu
46na kuyahifadhi mawe yake mahali pazuri juu ya mlima wa hekalu, mpaka nabii atokee wa kuamua nini cha kuyafanyia mawe hayo.
47Halafu wakachukua mawe yasiyochongwa, kwa mujibu wa sheria, wakajenga madhabahu mpya, sawa na madhabahu ya zamani.
48Hali kadhalika walilifanyia matengenezo hekalu, ndani na nje, wakazitakasa na nyua zake.
49Walitengeneza vyombo vipya kwa ajili ya ibada, na wakaingiza hekaluni kinara, madhabahu ya ubani, na meza ya mikate.
50Wakafukiza ubani juu ya madhabahu, na kuwasha taa za kinarani zipate kuangaza hekaluni.
51Wakaweka mikate mezani, wakatundika mapazia, na kumaliza kazi yote waliyokuwa wamenuia kufanya.
52Mapema asubuhi, siku ya ishirini na tano ya mwezi wa tisa, yaani, mwezi wa Kislevu, mwaka 148,[#4:52 Huo ni sawa na 164 K.K.]
53wakaamka na kutambika, kadiri ya sheria, juu ya madhabahu mpya waliyokuwa wamejenga.
54Hivi, waliiweka wakfu madhabahu mpya kwa nyimbo na muziki wa vinubi na vinanda na matari, wakati ule ule na siku ileile ilipotiwa unajisi na watu wa mataifa mengine, mwaka mmoja kabla yake.
55Watu wote wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu na kumsifu Bwana aliyewafanikisha.
56Kwa siku nane waliadhimisha sikukuu ya kuitabaruku madhabahu, wakatolea kwa furaha sadaka za kuteketezwa, na kutoa tambiko ya wokovu na shukrani.
57Waliupamba ukuta wa mbele wa hekalu kwa taji za dhahabu na ngao ndogondogo; wakatengeneza milango ya hekalu; wakajenga upya vyumba vya makuhani na kuweka milango.
58Watu walikuwa na furaha kubwa sana, nayo aibu iliyoletwa na watu wa mataifa mengine ikawa imeondolewa.
59Kisha, Yuda na nduguze na jumuiya yote ya Israeli wakaamua kwamba kila mwaka wakati kama ule ifanyike, kwa furaha na shangwe, kumbukumbu ya kutabaruku madhabahu kwa muda wa siku nane, kuanzia siku ya ishirini na tano ya mwezi Kislevu.[#4:52-59 Hiyo ilikuwa sikukuu ya kuweka wakfu iitwayo “hanuka” na ambayo iliadhimishwa na Wayahudi kwa siku nane mnamo mwezi wa Desemba. Rejea 2Mak 10:1-8; taz Yoh 10:22.]
60Halafu wakajenga kuta ndefu na minara imara kuuzunguka mlima Siyoni, kuwazuia watu wa mataifa mengine wasiingie tena na kuikanyaga kama walivyofanya.
61Yuda akaweka kikosi cha askari hapo ili kulinda hekalu. Pia aliuimarisha mji wa Beth-zuri, ili watu wa Israeli wawe na ngome moja inayokabiliana na Idumea.