1 Samueli 16

1 Samueli 16

Daudi anapakwa mafuta kuwa mfalme

1Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Utamlilia Shauli mpaka lini? Wewe unajua kuwa mimi nimemkataa kuwa mfalme juu ya Israeli. Sasa, jaza upembe wako mafuta, uondoke. Nitakutuma kwa Yese wa mji wa Bethlehemu. Maana nimejipatia mfalme miongoni mwa wanawe.”[#16:1—31:13 Sehemu hii inayofuata inaanzia na kuingia kwa Daudi katika historia ya Waisraeli na kumalizia na simulizi la kusisimua kuhusu kifo cha Shauli (sura 31). Katika sehemu hii kuna visa viwili vinavyoelekeana na kupingana: kwanza kuingia kwa Daudi katika historia ya Waisraeli na kuendelea kufanikiwa kwake, na kwa upande mwingine Shauli na mambo yake yakiendelea kuwa mabaya siku kwa siku hata kuelekea mwisho wake wa kusikitisha. Licha ya hao wawili anatokea pia mtu mwingine ambaye ni Yonathani, rafiki na msiri mwaminifu wa Daudi.; #16:1 Alikuwa wa kabila la Yuda na mjukuu wa Ruthu na Boazi (taz Rut 4:12,17-22; 1 Nya 2:3-12).; #16:1 Mji yapata kilomita nane Kusini mwa Yerusalemu. Unatajwa mara ya kwanza katika Mwa 35:19, na ni mji alikozaliwa Daudi (1Sam 17:12,15). Juu ya umaarufu wa mji huu kuhusu “Masiha” taz Mika 5:1-2; Mat 2:5-6 na Yoh 7:42.]

2Samueli akasema, “Nitawezaje kwenda? Kama Shauli akisikia habari hizo, ataniua!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Chukua ndama pamoja nawe, na ukifika huko useme, ‘Nimekuja kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko’.

3Mwalike Yese kwenye tambiko hiyo nami nitakuonesha la kufanya. Utampaka mafuta kwa ajili yangu mtu yule nitakayekutajia.”

4Samueli akafanya kama alivyoambiwa na Mwenyezi-Mungu, akaenda Bethlehemu. Wazee wa mji wakatoka kumlaki wakiwa wanatetemeka, wakamwuliza, “Je, umekuja kwa amani?”

5Samueli akawaambia, “Nimekuja kwa amani. Nimekuja kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Jitakaseni wenyewe halafu twendeni kutoa tambiko.” Samueli akamtakasa Yese pamoja na wanawe, akawakaribisha kwenye tambiko.[#16:5 Katika matambiko ya namna hiyo ni wale tu waliokuwa safi kidini (yaani si najisi) ndio walioruhusiwa kushiriki (taz Lawi 7:20-21; 15:2,31; Kumb 23:10-11).]

6Walipofika, na Samueli alipomwona Eliabu, alijisemea moyoni mwake, “Hakika, mpakwa mafuta wa Mwenyezi-Mungu ndiye huyu aliye mbele ya Mwenyezi-Mungu!”[#16:6 Samueli alifikiri anajua Mungu alimtaka nani, lakini hata yeye ilibidi aoneshwe na Mungu mwenyewe.]

7Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Usiangalie sura yake na urefu wa kimo chake. Mimi nimemkataa kwani siangalii mambo kama wanavyoyaangalia binadamu wenye kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje, lakini mimi naangalia moyoni.”

8Kisha, Yese akamwita Abinadabu na kumleta mbele ya Samueli. Lakini Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.”

9Yese akamleta Shama. Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.”

10Yese aliwapitisha wanawe wote saba mbele ya Samueli lakini Samueli akamwambia, “Mwenyezi-Mungu hajamchagua yeyote kati ya hawa.”

11Halafu akamwambia, “Je, wanao wote wako hapa?”

Yese akajibu, “Bado yuko mdogo, lakini amekwenda kuchunga kondoo.” Samueli akamwambia, “Mtume mtu amlete; sisi hatutaketi chini, mpaka atakapokuja hapa.”

12Hivyo, Yese alituma mtu, naye akaletwa. Yule kijana alikuwa mwenye afya, mwenye macho maangavu na wa kupendeza. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Sasa, huyu ndiye; inuka umpake mafuta.”[#16:12 Yamkini ndugu zake Daudi ambao walishuhudia Samueli akimpaka mafuta hawakujua maana yake (taz 17:28 ambapo Eliabu, kaka yake mkubwa, anamgombeza).]

13Samueli akachukua upembe wake wenye mafuta akammiminia Daudi mafuta mbele ya kaka zake. Mara roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Daudi kwa nguvu, ikakaa tangu siku hiyo na kuendelea. Kisha Samueli akarudi mjini Rama.[#16:13 Katika 1Sam 10:6 na 10 maneno hayo hayo yalisemwa kuhusu Shauli; lakini mwandishi anasema zaidi: “ikakaa tangu siku hiyo na kuendelea” kwa maana kwamba nguvu hiyo ya Mwenyezi-Mungu ilikaa kwake na kudumu, tofauti sana na Shauli au Samsoni.]

Daudi kwenye ukumbi wa Shauli

14Baadaye roho ya Mwenyezi-Mungu ilimwacha Shauli, na roho mwovu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ikamsumbua.[#16:14 Taz 18:10-12; 19:9-10; 1Fal 22:19-23; Luka 11:24-26. Hali ya Shauli inazidi kuwa mbaya tangu roho ya Mungu ilipomwacha (16:14).]

15Ndipo watumishi wake Shauli wakamwambia, “Tunajua kwamba roho mwovu kutoka kwa Mungu anakusumbua.

16Sasa, ee bwana wetu, amuru watumishi wako wanaokutumikia wamtafute mtu mwenye ufundi wa kupiga kinubi, na huyo roho mwovu kutoka kwa Mungu atakapokujia, mtu huyo atapiga kinubi, nawe utapata nafuu.”[#16:16 Ala ya muziki.]

17Shauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mtu huyo anayeweza kupiga kinubi vizuri, mniletee.”

18Kijana mmoja miongoni mwa watumishi akasema, “Nimemwona kijana mmoja wa Yese, wa mji wa Bethlehemu. Kijana huyo ana ujuzi wa kupiga kinubi. Huyo kijana ni shujaa, hodari wa kupigana vitani, ana busara katika kusema na mwenye umbo zuri; Mwenyezi-Mungu yuko pamoja naye.”

19Hivyo, Shauli alituma ujumbe kwa Yese, na kusema, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.”[#16:19 Shauli bila kufahamu anamwalika katika mahakama mtu ambaye Mungu amemchagua kushika nafasi yake na kutambulishwa kwake kwa Waisraeli kunaanza.]

20Yese alimtuma Daudi kwa Shauli pamoja na punda aliyebeba mikate, kiriba cha divai na mwanambuzi.[#16:20 Mara nyingi divai ilihifadhiwa katika mfuko (kiriba) ambao ulitengenezwa kwa ngozi ya mbuzi.]

21Daudi alipofika akaingia kumtumikia Shauli. Shauli alimpenda sana, hata akamfanya awe mwenye kumbebea silaha zake.

22Halafu Shauli alituma ujumbe kwa Yese na kusema, “Nampenda Daudi; mwache akae hapa anitumikie.”

23Kila mara, yule roho mwovu kutoka kwa Mungu alipomjia Shauli, Daudi alichukua kinubi chake na kuanza kukipiga, na roho huyo alimwacha Shauli, naye akaburudika na kupata nafuu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania