2 Wakorintho 1

2 Wakorintho 1

1Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia nyinyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho, na watu wote wa Mungu kila mahali katika Akaya.[#1:1 Tazama 1Kor 1:1; Gal 1:1.; #1:1 Tazama maelezo katika Mate 16:1. Wakati Paulo alipoanzisha Kanisa la Korintho, Timotheo alikuwapo pamoja naye (Tazama aya 19 na pia Mate 18:5).; #1:1 Neno kwa neno: Watakatifu. Tazama Rom 1:7 maelezo.; #1:1-2 Paulo anaandika barua hii kwa Kanisa la Korintho kutoka huko Makedonia (2Kor 7:5; 9:2-4).]

2Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

Shukrani kwa Mungu

3Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote.[#1:3 Neno “faraja” latafsiri neno la Kigiriki ambalo lina maana pia ya kutia moyo na kusaidia; ni neno lile lile linalotumiwa kumtaja Roho Mtakatifu “parakletos”, yaani Mfariji (Taz Yoh 14:16-17).]

4Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.[#1:4 Paulo anatumia wingi: “Hutufariji katika taabu zetu”, “tupate”, yaani nafsi ya kwanza wingi hata mahali ambapo anahusika yeye peke yake. Mahala pengine ni wazi wanaohusika ni yeye na mwingine, k.m. Timotheo.]

5Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi kufarijiwa naye.

6Ikiwa tunapata taabu, basi ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu. Tukifarijika, ni kwa ajili ya kuwafariji nyinyi na kuwaunga mkono mpate nguvu ya kustahimili mateso yaleyale tunayoteseka sisi.

7Tena, matumaini tuliyo nayo kwa ajili yenu ni imara; tunajua kwamba mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu.

8Ndugu, tunataka kuwajulisheni taabu zilizotupata kule Asia; taabu hizo zilitulemea kupita kiasi, hata tukakata matumaini yote ya kuendelea kuishi.[#1:8-9 Mkoa wa utawala wa Waroma, ambao sasa ni Uturuki. Si dhahiri ni taabu gani hasa ambazo zilimpata Paulo, lakini tazama pia Mate 1Kor 15:32; 16:9.]

9Naam, tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu zetu sisi wenyewe.

10Yeye alituokoa katika hatari kubwa ya kifo, na anaendelea kutuokoa; sisi tumemwekea tumaini letu kwamba atatuokoa tena,[#1:10 Hati nyingine: “Kifo cha kutisha sana”.]

11nyinyi mkiwa mnatuunga mkono kwa kutuombea. Hivyo neema tutakazokuwa tumepata kutokana na maombi ya watu wengi hivyo, ziwe sababu ya watu wengi zaidi kumshukuru Mungu kwa ajili yetu.

Badiliko katika safari ya Paulo

12Sisi tunajivunia kitu kimoja: dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali na neema ya Mungu.

13Tunawaandikia nyinyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba mtaelewa vizuri kabisa,[#1:13 Kwa kusema hivyo yaonekana kulikuwa na watu waliofikiri au kusema kwamba Paulo alikuwa mgumu kueleweka anapoandika au kusema (ling na 2Kor 2:17; 4:2).]

14maana mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile siku ya Bwana Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea nyinyi fahari.

15Nikiwa na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu.[#1:15-17 Paulo alikuwa ameshambuliwa kwamba hakuwa na msimamo katika maamuzi ya ziara na safari zake au alikuwa dhaifu (taz pia Mate 19:21; 1Kor 16:5-7); ukweli ni kwamba, kama asemavyo katika 2Kor 1:23—2:3, mabadiliko aliyokuwa anayafanya yalikuwa kwa faida yao. Paulo anajitetea dhidi ya lawama walizotoa watu.]

16Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia na wakati wa kurudi pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea.

17Je, mnadhani nilipopanga hivyo nimekuwa kama mtu asiye na msimamo? Je, mnadhani kwamba ninafanya uamuzi wangu kwa fikira za kibinadamu na kwamba nasema “Ndiyo” na “Siyo” papo hapo?

18Mungu ni ukweli tupu; basi, kile tulichowaambia nyinyi si jambo la “Ndiyo” na “Siyo”.

19Maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silwano na Timotheo, tulimhubiri kwenu, hakuwa mtu wa “Ndiyo” na “Siyo;” bali yeye daima ni “Ndiyo” ya Mungu.[#1:19 Namna ya kuandika kwa Kilatini jina lile lile la “Sila” (Mate 15:22).]

20Maana ndani yake ahadi zote za Mungu zimekuwa “Ndiyo”. Kwa sababu hiyo, “Amina” yetu husemwa kwa njia ya Kristo kwa ajili ya kumtukuza Mungu.[#1:20 Neno la Kiebrania ambalo latumiwa hapa kwa maana ya “Ndiyo”. Katika Rom 1:25 “Amina” linatumika karibu kama litumikavyo katika kumalizia sala na kukazia maombi (ling Zab 41:13). Laweza pia kutafsiriwa: “Ndivyo”, “Iwe hivyo”, “Iwe imara”, n.k. Tazama pia 1Kor 14:16.]

21Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na nyinyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu;[#1:21 Neno kwa neno “anayetupaka mafuta”. Huu ni msemo unaotokana na desturi ya kuwapaka mafuta ya zeituni wale walioteuliwa kwa wadhifa fulani kama vile makuhani na wafalme (Kut 28:41; 1Sam 16:13; Isa 61:1). Tazama pia Luka 4:18.]

22ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.[#1:22 Aghalabu dhamana ni malipo fulani yatolewayo kama ahadi au uthibitisho kwamba malipo yaliyobaki au jambo lililoahidiwa litafanyika kwa hakika kabisa (taz 2Kor 5:5; Efe 1:14). Hivyo kadiri ya Paulo zawadi ya Roho Mtakatifu ni zawadi ya kwanza.]

23Mungu ndiye shahidi wangu; yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho kwa sababu tu ya kuwahurumieni.

24Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; nyinyi mko imara katika imani yenu. Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania