The chat will start when you send the first message.
1Hata ikawa katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati ambapo wafalme huenda vitani, Daudi alimtuma Yoabu na maofisa wake pamoja na Waisraeli wote kupigana; nao waliteka nyara Waamoni na kuuzingira mji wa Raba. Lakini Daudi alibaki Yerusalemu.[#11:1 Huo ulikuwa wakati baada ya mavuno na hivyo nafaka ilikuwako ya kutosha kuchukua vitani na watu wengi zaidi wangeweza kwenda vitani. Taz pia 1Fal 20:22,26; 1 Nya 20:1.]
2Siku moja, wakati wa jioni, Daudi aliamka kitandani akaenda kwenye paa ya ikulu. Alipokuwa anatembea huko juu, alimwona mwanamke mmoja akioga na mwanamke huyo alikuwa mzuri sana.[#11:2 Kwa kawaida nyumba zilikuwa na mapaa yaliyokuwa sawasawa au bapa hivyo kwamba watu waliweza kutembea huko hasa wakati wa kiangazi kwa kuwa huko kulikuwa baridi kuliko ndani ya nyumba na kulifaa kwa kupunga upepo.]
3Daudi akatuma mtu kuuliza mwanamke huyo ni nani. Mtu huyo akamwambia Daudi “Mwanamke huyo ni Bathsheba binti wa Eliabu, na ni mke wa Uria Mhiti.”[#11:2-4 Wahiti walitoka katika eneo ambalo sasa ni nchi ya Uturuki na wakati mmoja, hapo kale, walimiliki karibu eneo lote la Mashariki ya Kati ya Kale (taz Yos 1:4). Baadhi yao, wakati wa Daudi, walihamia katika maeneo ya Waisraeli (Mwa 23:3; Hes 13:29; Yos 1:4) na hata kuchukua majina ya Kiebrania yakiwa yameambatishwa na majina ya Kihiti. Hapa jina “Uria” Kiebrania lina maana ya “Mwenyezi-Mungu ni mwanga”.]
4Basi, Daudi alituma wajumbe wamlete. Basi Bathsheba akaja kwa Daudi, naye Daudi akalala naye; (mwanamke huyo alikuwa ndio tu amejitakasa baada ya hedhi yake); kisha akarudi nyumbani kwake.
5Mwanamke huyo akapata mimba, naye akatuma habari kwa Daudi kuwa ana mimba yake.
6Basi, Daudi akamtumia Yoabu ujumbe, “Mtume Uria, Mhiti kwangu.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi.
7Uria alipofika kwake, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, watu wote, na hali ya vita.
8Halafu Daudi alimwambia Uria, “Rudi nyumbani kwako ukanawe miguu yako.” Uria alitoka nyumbani kwa mfalme, na mara mfalme akampelekea zawadi.[#11:8 Msemo huu waweza kuwa na maana ya kupumzika (taz Mwa 18:4; 43:24) au unaweza kuwa na maana ya kupumzika na kustarehe na mke wake.]
9Lakini Uria hakurudi nyumbani kwake, bali alilala pamoja na watumishi wote wa bwana wake kwenye lango la ikulu.
10Daudi alipoambiwa kwamba Uria hakwenda nyumbani kwake, Daudi alimwuliza Uria, “Wewe umetoka safari, kwa nini hukuenda nyumbani kwako?”
11Uria alimjibu Daudi “Sanduku la agano, pamoja na majeshi yote ya Israeli na Yuda yanakaa kwenye vibanda vitani. Bwana wangu Yoabu na watumishi wake wote wamepiga kambi mbugani; je ni sawa mimi niende nyumbani nikale na kunywa na kulala na mke wangu? Kama uishivyo na roho yako inavyoishi, sitafanya kitu cha namna hiyo.”[#11:11 Ingawa Daudi alikuwa amelileta sanduku la agano na kuliweka kule Yerusalemu, inaonekana kwamba bado lilichukuliwa kuandamana na majeshi vitani ili Mwenyezi-Mungu awe pamoja na majeshi hayo na kuyapatia ushindi.; #11:11 Kwa desturi za nyakati hizo askari hawakuruhusiwa kujamiiana na wake zao kwani hiyo ingewafanya kuwa najisi wasifae kupigana vita vya Mwenyezi-Mungu (taz 1Sam 21:4 maelezo).]
12Kisha, Daudi akamwambia Uria, “Basi, kaa hapa leo pia, na kesho nitakuacha urudi.” Hivyo Uria akabaki mjini Yerusalemu siku hiyo. Siku iliyofuata,
13Daudi alimwalika Uria kula na kunywa huko kwake, akamfanya Uria alewe. Hata hivyo, usiku ule Uria hakwenda nyumbani kwake, ila alilala kwenye kochi lake pamoja na watumishi wa bwana wake.
14Asubuhi yake, Daudi alimwandikia Yoabu barua akampa Uria aipeleke kwa Yoabu.
15Katika barua hiyo Daudi aliandika hivi: “Mweke Uria kwenye mstari wa mbele, mahali ambako mapigano ni makali kabisa, kisha umwache huko na kurudi nyuma ili apigwe, afe.”[#11:14-15 Kwamba Daudi anaandika barua yenye mpango wa kumwua Uria na kumpatia barua hiyohiyo ampelekee Yoabu ni kitu kisichoeleweka; wengine wanafikiri Uria hakujua kusoma au alikuwa mtu mwaminifu kiasi kwamba hangeweza kufungua barua ya mtu mwingine.]
16Basi, Yoabu alipokuwa anauzingira mji alimweka Uria mahali ambapo alijua wazi wanajeshi wa adui walikuwa hodari sana.
17Wakazi wa mji huo walitoka katika mji wao na kupigana na Yoabu. Baadhi ya watumishi wa Daudi, waliuawa. Uria Mhiti naye aliuawa pia.
18Kisha, Yoabu alipeleka habari zote kwa Daudi akimweleza juu ya vita.
19Yoabu akamwamuru huyo mtumishi aliyemtuma hivi, “Baada ya kumweleza mfalme mambo yote kuhusu vita,
20akikasirika na kukuuliza, ‘Kwa nini mlikwenda karibu na mji mlipokuwa mnapigana? Hamkujua kwamba wangewapiga mishale kutoka kwenye kuta za mji wao?[#11:20 Miji mingi ya wakati huo ilikuwa imezungushiwa kuta ndefu na pana kiasi cha askari kutembea juu yake na wakati wa vita kuwapiga mishale maadui wao.]
21Nani alimuua Abimeleki mwana wa Yerubeshethi? Si alikuwa mwanamke mmoja mjini Thebesi ambaye alitupa jiwe la kusagia kutoka kwenye ukuta nalo likamuua Abimeleki? Kwa nini basi, mlikwenda karibu na ukuta?’ Basi, wewe utamwambia hivi, ‘Hata mtumishi wako Uria Mhiti, naye amekufa.’”[#11:21 Amu 9:53]
22Yule mjumbe alikwenda kwa Daudi na kumwambia yote aliyotumwa na Yoabu ayaseme.
23Yule mjumbe akamwambia Daudi, “Adui zetu walituzidi nguvu, wakatoka nje ya miji na kutushambulia nyikani. Hata hivyo sisi tuliwarudisha mpaka kwenye lango la mji.
24Halafu wakatupiga mishale sisi watumishi wako kutoka ukutani. Baadhi ya watumishi wako waliuawa. Hata mtumishi wako Uria, Mhiti, naye amekufa.”
25Daudi akamwambia yule mjumbe, “Utamwambia hivi Yoabu, ‘Jambo hili lisikusumbue kwani upanga hauna macho, vita huua yeyote yule. Bali, imarisha mashambulizi dhidi ya mji, hadi umeuangamiza mji huo’. Ndivyo utakavyomtia moyo Yoabu.”
26Bathsheba mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe Uria amekufa, alimwombolezea mumewe.
27Muda wa matanga ulipokwisha, Daudi aliagiza Bathsheba achukuliwe na kupelekwa nyumbani kwake. Bathsheba akawa mke wa Daudi, naye akamzalia Daudi mtoto wa kiume. Lakini jambo hilo alilofanya Daudi lilimchukiza Mwenyezi-Mungu.[#11:27 Kwa kawaida muda huo ulikuwa wa siku saba.]