Matendo 18

Matendo 18

Paulo kule Korintho

1Baada ya hayo, Paulo aliondoka Athene, akaenda Korintho.[#18:1 Mji mkuu wa serikali ya mkoa wa Akaya na mji maarufu kabisa wa biashara. Mji wenyewe ulikuwa umejengwa katika sehemu ya nchi iliyotenganisha bahari ya Aegea na ile ya Adria. Wakati wa Paulo Korintho ulikuwa mji ambao tamaduni nyingi zilifana. Huko kulikuwa na mahekalu, masoko na majumba ya maonesho na usanii.]

2Huko Korintho, alimkuta Myahudi mmoja aitwaye Akula, mzaliwa wa Ponto. Akula pamoja na mkewe aitwaye Priskila, walikuwa wamerudi kutoka Italia siku hizohizo kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Roma. Paulo alikwenda kuwaona,[#18:2 Eneo kaskazini mwa Asia Ndogo.; #18:2 Jina lioneshalo udogo nalo latokana na jina (Rom 16:3; 1Kor 16:19; 2Tim 4:19).; #18:2 Amri ya Kaisari Klaudio ya kuwafukuza Wayahudi kutoka Roma ilitolewa yapata mwaka 49 B.K. (taz Mate 11:28).]

3na kwa vile wao walikuwa mafundi wa kushona mahema kama yeye, Paulo alikaa nao akafanya kazi.

4Kila Sabato alifanya majadiliano katika sunagogi akijaribu kuwavuta Wayahudi na Wagiriki.

5Baada ya Sila na Timotheo kuwasili kutoka Makedonia, Paulo alianza kutumia wakati wake wote kwa ajili ya kuhubiri, akawathibitishia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo.[#18:5 Au: “Yesu ndiye Masiha”. Taz Mate 3:18 maelezo.]

6Walipompinga na kuanza kumtukana, aliyakung'uta mavazi yake mbele yao akisema, “Mkipotea ni shauri lenu wenyewe; mimi sina lawama yoyote juu ya jambo hilo. Na tangu sasa nitawaendea watu na mataifa mengine.”[#18:6 Kama ishara ya kukata uhusiano nao; yaani hata mavumbi ya mahali hapo anawaachia.]

7Basi, akatoka hapo akaenda kukaa nyumbani kwa mtu mmoja mcha Mungu aitwaye Tito Yusto, ambaye nyumba yake ilikuwa karibu na lile sunagogi.[#18:7 Huyu yamkini alikuwa Mroma, au walau alikuwa si Myahudi. Kwamba Paulo alikwenda kukaa nyumbani kwake kwadhihirisha kwamba wakati huo alikuwa amekata uhusiano na sunagogi la Wayahudi (taz 10:28).]

8Krispo, mkuu wa hilo sunagogi, alimwamini Bwana yeye pamoja na jamaa yake yote. Wakorintho wengi waliusikiliza ujumbe huo, wakaamini na kubatizwa.

9Siku moja usiku, Bwana alimwambia Paulo katika maono: “Usiogope, endelea kuhubiri tu bila kufa moyo,

10maana mimi niko pamoja nawe. Hakuna mtu atakayejaribu kukudhuru maana hapa mjini pana watu wengi walio upande wangu.”

11Basi, Paulo alikaa huko akifundisha neno la Mungu kati yao kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.

12Lakini wakati Galio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Akaya, Wayahudi walimvamia Paulo kwa pamoja na kumpeleka mahakamani.[#18:12 Galio alikuwa gavana au mtawala wa mkoa wa Kiroma wa Akaya yapata mwaka 51 mpaka 52 B.K.]

13Wakasema, “Tunamshtaki mtu huyu kwa sababu ya kuwashawishi watu wamwabudu Mungu kwa namna inayopingana na sheria.”

14Kabla tu Paulo hajaanza kusema, Galio aliwaambia Wayahudi, “Sikilizeni enyi Wayahudi! Kama kweli jambo hili lingekuwa juu ya uhalifu au uovu ningekuwa tayari kuwasikilizeni.

15Lakini kama ni shauri la ubishi kuhusu maneno na majina na sheria yenu, amueni nyinyi wenyewe. Mimi sitaki kuwa hakimu wa mambo hayo!”

16Basi, akawafukuza kutoka mahakamani.

17Nao wote wakamkamata Sosthene ambaye alikuwa kiongozi wa sunagogi, wakampiga palepale mbele ya mahakama. Lakini Galio hakujali kitendo hicho hata kidogo.[#18:17 Yamkini alikuwa mwenzi wa kazi wa Krispo (aya 8) naye huenda ni mtu yuleyule anayetajwa katika 1Kor 1:1.; #18:17 Gavana wa Kiroma alifikiri dini ya Kikristo ni maendelezo tu ya dini ya Kiyahudi, kwa hiyo alimruhusu Paulo kuhubiri bila pingamizi.]

Paulo anarudi tena Antiokia

18Paulo alikaa bado na wale ndugu huko Korintho kwa siku nyingi. Kisha aliwaaga, akapanda meli kwenda Siria pamoja na Priskila na Akula. Huko Kenkrea, alinyoa nywele zake kwa sababu ya nadhiri aliyokuwa ameweka.[#18:18 Ilikuwa bandari ya Korintho kwa upande wa bahari ya Aegea.; #18:18 (Hes 6:2-18). Ilikuwa nadhiri ambayo, baadhi ya mengine, mhusika alitakiwa kuacha kunyoa kwa muda fulani.]

19Walifika Efeso na hapo Paulo aliwaacha Priskila na Akula, akaenda katika sunagogi, akajadiliana na Wayahudi.[#18:19 Bandari maarufu na mji mkuu wa mkoa wa Kiroma wa Asia (sasa ni sehemu ya Uturuki).]

20Walimwomba akae nao muda mrefu zaidi, lakini hakupenda.

21Bali alipokuwa anaondoka, alisema, “Mungu akipenda nitakuja kwenu tena.” Akaondoka Efeso kwa meli.

22Meli ilitia nanga Kaisarea, naye Paulo akaenda Yerusalemu kulisalimia lile kanisa, kisha akaenda Antiokia.

23Alikaa huko muda mfupi, halafu akaendelea na safari kwa kupitia sehemu za Galatia na Frugia akiwatia moyo wafuasi wote.[#18:23—20:18 Hapa inaanza habari juu ya ziara ya tatu ya kitume ya Paulo, ambayo labda ilianza mwaka 52 au 53 B.K. Katika ziara hii Paulo anaendelea na shughuli zake alizoanza huko Efeso (sura 19). Ziara hiyo inamalizika kwa safari ya kurudi Yerusalemu (Mate 21:15-17).]

Apolo anahubiri Efeso na Korintho

24Myahudi mmoja aitwaye Apolo, mzaliwa wa Aleksandria, alifika Efeso. Alikuwa mtu mwenye ufasaha wa kuongea na mwenye ujuzi mkubwa wa Maandiko Matakatifu.[#18:24 Ling na 1Kor 1:12; 3:3-10; 16:12.; #18:24 Mji wa Misri mahali ambapo mto Nili unaingia baharini; mji huo ulikuwa kitovu cha mafunzo na makazi ya Wayahudi wengi walioongea Kigiriki.]

25Alikuwa amefundishwa juu ya hiyo njia ya Bwana, na akiwa motomoto, aliongea juu ya habari za Yesu akafundisha kwa usahihi ingawa alikuwa amepata ubatizo wa Yohane tu.[#18:25 Yaani Mbatizaji; Ling na 19:3-5.]

26Priskila na Akula walipomsikia akiongea kwa uhodari ndani ya sunagogi, walimchukua kwao wakamfundisha hiyo njia ya Mungu kwa usahihi zaidi.

27Apolo alipoamua kwenda Akaya, wale ndugu walimtia moyo kwa kuwaandikia wafuasi kule Akaya wampokee. Alipofika huko, aliweza kwa msaada wa neema ya Mungu, kuwasaidia sana wale ndugu waliopata kuwa waumini;[#18:27 Athene na Korintho ilikuwa miji maarufu ya mkoa wa Akaya (Mate 19:1).]

28kwa maana aliendelea kwa uhodari kuwashinda Wayahudi hadharani akithibitisha kwa Maandiko Matakatifu kuwa Yesu ni Kristo.[#18:28 Mate 9:22; 18:5.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania