Amosi 6

Amosi 6

Adhabu kwa sababu ya kujiamini

1Ole wenu nyinyi mnaostarehe huko Siyoni,

nanyi mnaojiona salama mlimani Samaria!

Nyinyi mwaonekana kuwa viongozi wa taifa maarufu

ambao Waisraeli wote huwategemea.

2Haya! Nendeni Kalne mkaangalie kila mahali,[#6:2 Aya hii inaweza kueleweka kama onyo la Amosi kwa viongozi wa Israeli, au kama maneno ya kujivuna ambayo Amosi anawawekea mdomoni mwao. “Kalne” na “Hamathi” ilikuwa miji maarufu ya Siria (Isa 10:9).]

tokeni huko mwende hadi mji ule mkubwa wa Hamathi,

kisha teremkeni hadi Gathi kwa Wafilisti.

Je, falme zao si bora kuliko zenu

na eneo lao si bora kuliko lenu?”

3Nyinyi mnajaribu kuifukuza siku mbaya.

Lakini mnauleta karibu utawala dhalimu.

4Ole wenu mnaolala juu ya vitanda vya pembe za ndovu

na kujinyosha juu ya masofa,

mkila nyama za wanakondoo na ndama!

5Nyinyi mnapenda kuimba ovyo na sauti ya vinubi

na kubuni ala mpya za muziki mkimwiga mfalme Daudi.

6Mnakunywa divai kwa mabakuli,

na kujipaka marashi mazuri mno.

Lakini hamhuzuniki hata kidogo

juu ya kuangamia kwa wazawa wa Yosefu.

7Kwa hiyo mtakuwa wa kwanza kwenda uhamishoni,[#6:7 Taz Amo 5:27.]

na karamu za wenye kustarehe zitatoweka.

8Bwana Mwenyezi-Mungu ameapa kwa nafsi yake;

Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi asema:

“Nachukizwa mno na kiburi cha wazawa wa Yakobo;

tena nayachukia majumba yao ya fahari.

Mji wao na vyote vilivyomo nitawapa adui zao.”

9Kama wakibaki watu kumi katika nyumba moja, wote watakufa.

10Na atakapokuja mjomba wa aliyekufa kuitoa maiti nje aichome, akamwuliza yeyote atakayekuwako ndani pembeni mwa nyumba, “Je kuna mtu mwingine pamoja nawe?” Naye atamjibu, “La! Hamna!” Naye atamwambia, “Nyamaza kimya! Tusilitaje hata jina la Mwenyezi-Mungu.”[#6:10 Maana ya aya hii katika Kiebrania si dhahiri. Lakini inaonekana kwamba wazo la kutokumtaja Mwenyezi-Mungu katika mazingira hayo ni kutaka kuepa madhara zaidi.]

11Tazama! Mwenyezi-Mungu anatoa amri,

nalo jumba kubwa labomoka vipandevipande,

na nyumba ndogo kusagikasagika.

12Je, farasi waweza kupiga mbio miambani?

Je, watu huilima bahari kwa ng'ombe?

Lakini nyinyi mmeigeuza haki kuwa sumu,

na tunda la uadilifu kuwa uchungu.

13Nyinyi mnashangilia juu ya Lodebari,[#6:13 Matumizi ya jina hili katika Kiebrania ni kama neno lenye maana “kitu batili” au “upuuzi.”]

na kusema mmeuteka Karnaimu kwa nguvu zenu wenyewe.

14Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:

“Enyi Waisraeli,

kweli nitaleta taifa moja lije kuwashambulia,

nalo litawatesa nyinyi kuanzia Lebo-hamathi kaskazini,

hadi kijito cha Araba, upande wa kusini.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania