Kutoka 20

Kutoka 20

Amri kumi

(Kumb 5:1-21)

1Mwenyezi-Mungu alizungumza maneno haya yote, akasema,[#20:1-17 Amri kumi zinaitwa pia “Maneno kumi” kulingana na Kiebrania cha Kut 34:28; Kumb 4:13 na 10:4. Amri hizo kumi hupatikana pia katika Kumb 5:6-21 ambapo kuna machache yaliyo tofauti na orodha hii ya Kutoka. Kwa muhtasari orodha ya amri kumi huonesha wajibu wa binadamu kwa Mungu na kwa binadamu mwenzake. Mungu anachukua nafasi ya kwanza (aya 2-8) kisha kutoka uhusiano huo na Mungu, uhusiano na binadamu unatajwa (aya 12-17). Katika Kumbukumbu la Sheria amri kumi zinatajwa katika hotuba ya Mose kwa Waisraeli wakati walipokuwa wanajitayarisha kuingia nchini Kanaani (Kumb 1:5).]

2“Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekutoa nchini Misri, ambako ulikuwa mtumwa.[#20:2 Amri kumi yamkini zina muundo wa kimsingi wa mtindo wa mkataba wa kale kati ya mtawala na watawaliwa, mtindo ambao mtawala anajitambulisha pamoja na kutaja mambo aliyoyafanya kwa faida ya watawaliwa, kisha mtawala anataja sheria ambazo watawaliwa wanapaswa kuzishika.]

3“Usiwe na miungu mingine ila mimi.[#20:3 Au: “Usiabudu mungu mwingine isipokuwa mimi”. Taz Kumb 6:4-5; Mat 22:37.]

4“Usijifanyie sanamu ya miungu wa uongo, au kinyago cha chochote kilicho mbinguni, katika nchi au majini chini ya dunia.

5Usiisujudie wala kuitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu. Nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha hao wanichukiao.[#20:5 Upendo mkuu wa Mungu kwa watu wake hauwezi kustahimili au kuruhusu watu wake waamini au wategemee miungu mingine wala kuwa na chochote ambacho kinaweza kuchukua nafasi yake. Watu hao ni wake yeye mwenyewe. Taz Kut 34:14.; #20:5 Maneno haya yaanadhihirisha kuweko kwa imani kwamba mtoto huadhibiwa kwa madhambi ya wazee wao (taz Eze 18:2 na aya zinazofuata ambazo zinatupilia mbali imani hiyo na kulenga kuwajibika kwa kila mtu binafsi). Kwamba wazawa wanaathirika kutokana na makosa ya babu zao ni imani iliyokithiri sana katika mataifa na jamii nyingi hata katika nchi zetu. Kutokana na imani hiyo kuna mshikamano wa kushikilia maadili ya taifa, kabila au ukoo.]

6Lakini nawafadhili maelfu ya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.[#20:6 Au: “Nafadhili vizazi elfu na elfu vya watu wanipendao”. Yaonekana kwamba aya hii inabainisha kitendo cha Mungu cha kufadhili kuwa kinazidi au kupita kile cha kupatiliza. Yaani huruma yake huwafikia watu “maelfu” na sio tu mpaka kizazi cha tatu au cha nne kama aya iliyotangulia. Idadi “maelfu” hapa ni ya upeo.]

7“Usilitaje bure jina langu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Maana mimi Mwenyezi-Mungu sitaacha kumwadhibu anayetumia jina langu vibaya.

8“Usisahau kuiweka takatifu siku ya Sabato.

9Siku sita fanya kazi na tenda mambo yako yote.

10Lakini siku ya saba ni Sabato ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala watumishi wako wa kike, wala mnyama wako wa kufugwa, wala mgeni aliye nyumbani mwako.

11Maana kwa siku sita mimi Mwenyezi-Mungu niliziumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo, kisha nikapumzika siku ya saba. Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu niliibariki siku ya Sabato, nikaitakasa.

12“Waheshimu baba yako na mama yako, ili uishi maisha marefu katika nchi ninayokupa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.[#20:12 Watoto walitazamiwa kuwastahi wazazi wao (Zab 91:15). Amri hiyo inaambatana na ahadi. Taz Kumb 27;16; Mat 15:4; 19:19; Marko 7:10; 10:19; Luka 18:20; Efe 6:2.]

13“Usiue.[#20:13 Neno hili katika Kiebrania linakataza mauaji ya kukusudia (rejea Zab 94:6) na wakati mwingine pia mauaji yasiyokusudiwa kwa kutokujali. Kwa jumla basi amri hii inakataza kumwaga damu ya mtu asiye na hatia.]

14“Usizini.

15“Usiibe.

16“Usimshuhudie jirani yako uongo.

17“Usiitamani nyumba ya jirani yako, wala mke wake, wala mtumwa wake wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala chochote kilicho mali ya jirani yako.”[#20:17 Kitenzi cha neno la Kiebrania linalotafsiriwa hapa kwa “usitamani” hakihusu tu mawazo au kufikiri, bali pia msukumo wa kutoka ndani ya mtu ambao unamwongoza mtu na kumfanya atake kukichukua kitu kisicho halali kwake. Taz pia Rom 7:7; 13:9.]

18Watu waliposikia ngurumo na kuona umeme ukiwaka na kuisikia sauti ya parapanda juu ya mlima uliokuwa unafuka moshi, wote waliogopa na kutetemeka. Wote walisimama mbali,

19wakamwambia Mose, “Ongea nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza, lakini Mwenyezi-Mungu asiongee nasi, tusije tukafa.”

20Mose akawaambia, “Msiogope, maana Mungu amekuja kuwajaribu ili mpate kumcha yeye daima na msitende dhambi.”

21Watu wote walisimama mbali wakati Mose alipokaribia lile wingu zito alimokuwamo Mungu.

Sheria kuhusu madhabahu

22Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli: ‘Mmejionea nyinyi wenyewe kwamba nimeongea nanyi kutoka mbinguni.

23Mtaniheshimu mimi peke yangu wala msijifanyie miungu ya fedha wala ya dhahabu.

24Nyinyi mtanijengea madhabahu ya udongo ambayo juu yake mtanitambikia kondoo wenu na ng'ombe wenu kama sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Mahali popote nitakapowakumbusha watu jina langu, papo hapo mimi mwenyewe nitawajia na kuwabariki.

25Kama mkinijengea madhabahu ya mawe, msiitengeneze kwa mawe ya kuchonga, maana mkitumia vyombo vya kuchongea mawe, mtaitia najisi.

26Wala msitengeneze madhabahu yenye ngazi za kupandia, mtu asije akauona uchi wa huyo anayepanda juu yake.’[#20:26 Makuhani walitakiwa kuvaa nguo ndefu na chupi za namna ya pekee. Dini ya watu wa Israeli haikuruhusu namna yoyote ya desturi za mataifa mengine kuhusu ukahaba wa kidini.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania