The chat will start when you send the first message.
1Akaniambia, “Wewe mtu, kula unachopewa; kula kitabu hiki kisha uende ukawaeleze Waisraeli.”[#3:1 Taz 2:1 maelezo.]
2Kwa hiyo nilifumbua kinywa changu, naye akanilisha hicho kitabu.
3Halafu akaniambia, “Wewe mtu, kula kitabu hiki ninachokupa, ujaze tumbo lako.” Basi, nilikula kitabu hicho, nacho kikawa kitamu mdomoni kama asali.
4Kisha akaniambia, “Wewe mtu, waendee Waisraeli, ukawaambie maneno yangu.[#3:4-11 Aya hizi zahusu kutumwa kwa Ezekieli. Namna hii ya kuwatuma wajumbe wa Mungu inapatikana pia katika Isa 6:8-9; Yer 1:7,17.]
5Sikutumi kwa taifa lenye lugha ngeni na ngumu, bali kwa Waisraeli.
6Sikutumi kwa mataifa mengi yenye lugha ngeni na ngumu ambayo huifahamu. Kwani ningelikutuma kwa watu kama hao, hakika wao wangekusikiliza.
7Lakini Waisraeli hawatakusikiliza, kwani hawana nia ya kunisikiliza mimi. Watu wote wa Israeli ni wenye kichwa kigumu na moyo mkaidi.
8Nimekufanya uwe mgumu dhidi yao, na kichwa chako kitakuwa kigumu dhidi ya vichwa vyao vigumu.
9Kama almasi ilivyo ngumu kuliko jiwe gumu, ndivyo nilivyokufanya uwe kichwa kigumu. Usiwaogope wala usitishwe na nyuso zao, kwani hao ni watu waasi.”
10Tena aliniambia, “Wewe mtu, maneno yote nitakayokuambia yatie moyoni mwako, na uyasikilize kwa makini.
11Kisha nenda kwa watu wako waliopelekwa uhamishoni, ukawaambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi na hivi. Waambie hata kama watakusikiliza au watakataa kukusikiliza.”
12Kisha roho ya Mungu ikaninyanyua, nami nikasikia nyuma yangu sauti kama ya tetemeko kubwa. “Na usifiwe utukufu wa Mwenyezi-Mungu mbinguni.”[#3:12 Hapa “Roho” inamaanisha nguvu ya Mungu (taz 2:2). Pengine neno hilo hilo hutumika kwa maana ya “upepo”. “Na usifiwe utukufu wa Mwenyezi-Mungu kutoka makao yake”: Sehemu ya aya hii ya 12 Kiebrania ni ngumu.]
13Pia nilisikia sauti ya mabawa ya wale viumbe hai yalipokuwa yanagusana, pamoja na sauti ya mgongano wa yale magurudumu kandokando yao.
14Basi, roho ya Mungu ikaninyanyua juu na kunipeleka mbali. Nikaenda nikiwa na uchungu na ukali rohoni mwangu, nao mkono wa Mwenyezi-Mungu ulikuwa na nguvu juu yangu.
15Nikawafikia wale watu waliokuwa uhamishoni, waliokuwa wakikaa karibu na mto Kebari huko Tel-abibu. Nikakaa nao kwa muda wa siku saba nikiwa nimepigwa bumbuazi.[#3:15 Ezekieli yuko katika hali ya mshtuko mkubwa, labda hata kutoweza kuongea na wale wenzake waliopelekwa uhamishoni.]
16Baada ya siku saba, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
17“Wewe mtu nimekuweka kuwa mlinzi wa Waisraeli. Kila utakaposikia neno kutoka kwangu utawaonya watu kwa niaba yangu.[#3:17 Mlinzi katika mazingira haya alikuwa mtu ambaye daima alikuwa macho kuwaashiria watu hatari inayokuja. Picha hii inatolewa kikamilifu katika sura ya 18 ambapo Ezekieli ana jukumu la kuwaambia watu ujumbe wa Mungu kuhusu kuwajibika kwa kila mtu binafsi.]
18Nikimwambia mtu mwovu kwamba hakika atakufa, nawe humwonyi au kumwambia aache njia yake potovu ili kuyaokoa maisha yake, basi, mtu huyo mwovu atakufa kwa uovu wake; lakini damu yake nitakudai wewe.
19Lakini, ukimwonya mtu huyo mwovu naye hauachi uovu wake au njia yake potovu, mtu huyo atakufa kwa uovu wake, lakini wewe utakuwa umeyaokoa maisha yako.
20Tena, kama mtu mwadilifu anauacha uadilifu wake na kutenda uovu, nami nikamwekea kikwazo, mtu huyo atakufa. Kwa vile hukumwonya, atakufa kwa sababu ya dhambi yake, nayo matendo yake ya uadilifu hayatakumbukwa. Lakini damu yake nitakudai wewe.
21Lakini, ukimwonya mtu mwadilifu asitende dhambi, naye akaacha kutenda dhambi, hakika mtu huyo ataishi, kwa kuwa amepokea maonyo yako, nawe utakuwa umeyaokoa maisha yako.”
22Nguvu ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa juu yangu; naye akaniambia, “Inuka uende mpaka sehemu tambarare nami nitaongea nawe huko.”
23Basi, nikainuka na kwenda sehemu tambarare. Lo! Nikiwa huko nikauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukiwa umesimama huko kama utukufu ule niliokuwa nimeuona karibu na mto Kebari; nami nikaanguka kifudifudi.
24Lakini roho iliniingia na kunisimamisha wima. Kisha Mungu akaongea nami, akaniambia, “Nenda ukajifungie nyumbani mwako.
25Ewe mtu, utafungwa kwa kamba ili usiweze kutoka na kuwaendea watu.
26Nitaufanya ulimi wako uwe mzito nawe utakuwa bubu ili usiweze kuwakemea kwa sababu ni waasi.
27Lakini kila nitakapoongea nawe nitakifungua kinywa chako, nawe utawaambia kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi na hivi, atakayekusikiliza, na akusikilize; atakayekataa kukusikiliza na akatae; maana hao ni watu waasi.[#3:27 Ezekieli ataongea tu pale Mungu atakapomwezesha. Katika 24:27; 33:22 kizuizi alichowekewa nabii cha kutoongea kitaondolewa mara tu baada ya kuteketezwa kwa mji wa Yerusalemu.]