Ezekieli 4

Ezekieli 4

Mji wa Yerusalemu utazingirwa

1“Wewe mtu, chukua tofali, uliweke mbele yako; kisha chora juu yake ramani ya mji wa Yerusalemu.[#4:1 Taz 2:1 maelezo.]

2Onesha kuwa umezingirwa. Chora ngome dhidi yake na maboma kandokando yake, makambi ya askari kandokando yake, na magogo ya kuubomolea.

3Kisha, chukua bamba la chuma ulisimamishe liwe kama ukuta wa chuma kati yako na mji. Kisha uelekee mji huo unaozingirwa, uoneshe kana kwamba unazingirwa. Fanya alama ya kuuzingira. Hii itakuwa ishara kwa taifa la Israeli.[#4:1-3 Katika sehemu ya kwanza ya huduma yake ya kinabii Ezekieli anatangaza kwamba kuangamizwa kwa mji wa Yerusalemu na hekalu takatifu ni jambo lisiloepukika kutokana na madhambi waliyotenda wakazi wake. Kwa hiyo anapiga vita mawazo ya wale waliopelekwa uhamishoni kwa mara ya kwanza (tazama 2Fal 24:8-17) kwamba fikira zao za kurudi upesi ni ndoto tu.]

4“Kisha, nenda ukalale kwa upande wako wa kushoto. Muda wote utakapokaa katika hali hiyo utabeba uovu wa Waisraeli kama mzigo mzito.[#4:4 Kiebrania “utaweka”.]

5Nimekupangia muda wa siku 390 muda ambao ni sawa na miaka ya adhabu yao. Siku moja ni sawa na mwaka mmoja. Utabeba adhabu ya Waisraeli.[#4:5 Labda idadi hiyo yagusia miaka iliyohusika kuanzia wakati utawala wa Solomoni ulipogawanyika mpaka wakati mji wa Yerusalemu ulipotekwa (yapata mwaka 587 K.K.).; #4:4-5 Neno hili latumika hapa kutaja ufalme wa kaskazini ambao uliangamizwa mwaka 722 (utawala wa kusini, yaani Yuda, unatajwa katika aya ya 6).]

6Utakapotimiza siku hizo, utalala kwa upande wa kulia, na hapo utabeba adhabu ya watu wa Yuda kwa muda wa siku arubaini; nimekupangia siku moja kuwa sawa na mwaka mmoja.[#4:6 Nambari 40 hutumika mara kwa mara kimfano kuashiria wakati wa majaribu, kama vile siku arubaini za gharika kuu au ile miaka arubaini katika kitabu cha Kutoka.]

7“Kisha, utauelekea mji wa Yerusalemu uliozingirwa na kuunyoshea mkono mtupu na kutabiri dhidi yake.

8Nitakufunga kamba ili usiweze kugeuka toka upande mmoja hadi upande mwingine, mpaka hapo kuzingirwa kwa Yerusalemu kutakapomalizika.

9“Chukua ngano, shayiri, maharagwe, choroko, mtama na mawele, uvitie vyote katika chombo kimoja, ujitengenezee mkate. Mkate huo ndio utakaokuwa chakula chako wakati unapolala kwa upande mmoja, siku zote 390.

10Chakula utakachokula lazima kipimwe, nacho kitakuwa gramu 230 kwa siku; nawe utakula mara moja tu kwa siku.

11Maji nayo utakunywa kwa kipimo: vikombe viwili, mara moja kwa siku.

12Utachukua mavi ya mtu, uwashe moto, uoke mkate, na kuula mbele ya watu.”[#4:12 Kutumia mavi ya mtu kama kuni za kupikia kulifikiriwa kuwa jambo najisi na ambalo lilifanya chakula nacho kuwa najisi (taz aya 13). Kwa watu kula hata chakula ambacho ni najisi inaonesha ukali wa hali ya kuzingirwa kwa Yerusalemu.]

13Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Hivyo ndivyo Waisraeli watakavyokula mkate wao unajisi wakiwa kati ya mataifa ninakowapeleka.”

14Ndipo nikamwambia, “Ee, Bwana Mwenyezi-Mungu, kamwe sijajitia najisi kwa kula kilichokufa chenyewe au kilichouawa na mnyama wa porini, wala sijapata kuonja nyama ya mnyama najisi tangu ujana wangu.”

15Kisha akaniambia, “Basi, nakuruhusu utumie mavi ya ng'ombe badala ya mavi ya mtu ili kuokea mkate wako.”

16Tena akaniambia, “Wewe mtu, mimi nitaharibu akiba ya chakula mjini Yerusalemu; wakazi wake watakula chakula watakachopimiwa kwa hofu. Watakunywa maji watakayopimiwa kwa kufadhaika.[#4:16 Taz 2:1 maelezo.]

17Nitafanya hivyo ili wakose chakula na maji, na kila mmoja atamwangalia mwenzake kwa kufadhaika; nao watadhoofika kwa adhabu yao.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania