Wagalatia 4

Wagalatia 4

1Basi, nasema hivi: mrithi, akiwa bado mtoto, hawi tofauti na mtumwa ingawaje mali yote ni yake.[#4:1 Au, “Yule ambaye baba yake atamkabidhi mali yake” na sio kwa maana ya kwamba atarithi baada ya kifo cha baba yake. Muhimu katika simulizi la Paulo ni kwamba sheria inahusikana na utumwa; Kristo, kwa kifo chake, amewatoa binadamu kutoka utumwa huo wa sheria na dhambi na kuwapa uhuru.]

2Wakati huo wote yuko chini ya walezi na wadhamini mpaka wakati ule uliowekwa na baba yake.

3Hali kadhalika na sisi tulipokuwa bado watoto, tulikuwa watumwa wa pepo watawala wa ulimwengu.[#4:3 Paulo hapa na katika aya ya 9 anataja hali isiyofaa ya binadamu kabla ya kuja kwake Yesu Kristo, hali ambayo nguvu zilizoutawala ulimwengu ndizo zilizoongoza. Kadiri ya Paulo sheria nayo ilichukua nafasi yake katika hali hiyo na kuwafanya watu kama watumwa, wakishikilia pia kanuni zilizoambatana na sayari za angani.]

4Lakini wakati ule maalumu ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini ya sheria,[#4:4 Yaani wakati uliowekwa na Mungu. Taz Marko 1:14-15.; #4:4-5 Ingawa aya hizi mbili ni ngumu kuzielewa vizuri, hoja ya Paulo inashika bado. Katika mazingira na hali ambamo utumwa wa sheria ulitawala, Mungu anamtuma mwanawe (aliyezaliwa kama sisi) kuikabili hali na mazingira hayo, ili tupate kukombolewa.]

5apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya sheria ili sisi tufanywe wana wa Mungu.

6Kwa vile sasa nyinyi ni wanawe, Mungu amemtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwenu, Roho ambaye hulia “Aba,” yaani “Baba.”[#4:6 Yamkini lengo la Paulo ni kutilia mkazo kwamba sisi kweli ni watoto wa Mungu na tunaweza kumwita kwa jina lile ambalo mtoto humwita nalo baba yake mzazi. Taz Rom 8:15 maelezo; rejea Marko 14:36; Luka 11:2.]

7Basi, wewe si mtumwa tena, bali mwana. Na ikiwa ni mwana, basi, wewe utapokea yote Mungu aliyowawekea watoto wake.

Wasiwasi wa Paulo juu ya Wagalatia

8Zamani hamkumjua Mungu na hivyo mliitumikia miungu isiyo miungu kweli.

9Lakini sasa, kwa vile mnamjua Mungu, au tuseme mnajulikana na Mungu, mnawezaje tena kurudi kwa wale pepo maskini na dhaifu hata kutaka kuwatumikia tena?[#4:9-10 Taz Gal 4:3 maelezo.]

10Bado mnaadhimisha siku, miezi na miaka!

11Nahofu kwamba labda kazi niliyoifanya kwa ajili yenu imepotea bure!

12Ndugu, nawasihi muwe kama mimi, kwa vile hata mimi nimekuwa kama nyinyi. Hamkunitendea ubaya wowote.

13Mnajua kwamba ugonjwa wangu ndio ulionipatia fursa ya kuwahubirieni Injili kwa mara ya kwanza.[#4:13-14 Kwa sababu ya ugonjwa fulani ilimbidi Paulo akae kwa muda huko Galatia na hivyo akapata fursa ya kuwahubiria Wagalatia Habari Njema kwa mara ya kwanza. Rejea Mate 16:6.]

14Hata hivyo, wakati ule hamkunidharau wala kunikataa kwa sababu ya udhaifu wangu ingawa mlishawishiwa kufanya hivyo; lakini mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama vile ningekuwa Kristo Yesu mwenyewe.

15Mlikuwa wenye furaha; sasa kumetokea nini? Naapa kwamba wakati ule mngaliweza hata kuyang'oa macho yenu na kunipa mimi.[#4:15 Kuna kitu kama methali hapa ambayo inatumika kuelezea kwamba Wagalatia walimpenda Paulo sana hata wangeweza kumpa chochote (kwa watu wa kale macho yalikuwa sehemu ya mwili iliyokuwa muhimu sana kupita zote).]

16Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa sababu ya kuwaambieni ukweli?

17Hao watu wengine wanawahangaikia nyinyi, lakini nia yao si njema. Wanataka kuwatenganisha nami ili nyinyi muwahangaikie wao.

18Kwa kweli ni jambo jema daima kuwahangaikia wengine katika mambo mema, na si tu wakati mimi nipo pamoja nanyi.

19Watoto wangu, kama vile mama mjamzito anavyotaabika wakati wa kujifungua, mimi nataabika tena kwa ajili yenu mpaka hapo hali yake Kristo itakapoundwa ndani yenu.

20Laiti ningekuwa pamoja nanyi sasa, maana ningalipata msimamo ufaao juu yenu! Nina wasiwasi sana nanyi!

Mfano wa Hagari na Sara

21Niambieni, enyi mnaopenda kutawaliwa na sheria: Je, mnasikia isemavyo sheria?[#4:21-31 Paulo anatumia historia ya Hagari na Sara pamoja na watoto wao Ishmaeli na Isaka (Mwa 16:1-15) kama mfano au picha ya vikundi viwili ambavyo vina msingi wake katika maagano mawili (aya 24). Agano la kwanza ni la utumwa wa sheria; la pili ni la uhuru. Taz Gal 4:31 maelezo.]

22Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Abrahamu alikuwa na watoto wawili: mmoja kwa mwanamke mtumwa, na wa pili kwa mwanamke huru.[#4:22 Yaani Hagari ambaye alikuwa mtumwa wa Abrahamu.]

23Yule wa mwanamke mtumwa alizaliwa kama kawaida, lakini yule wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu.[#4:23 Rejea Rom 9:7-9. Ishmaeli, mwanawe Hagari na Abrahamu, alizaliwa kama kawaida ya maumbile, hali Isaka, mwanawe Sara na Abrahamu, alizaliwa wakati ambapo uwezo wa maumbile ulikwisha koma, alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu (Mwa 17:15-21; 18:10-15).]

24Mambo hayo yamekuwa mfano; mama hao wawili ni mfano wa maagano mawili; la kwanza ni lile lililofanyika mlimani Sinai, mwakilishi wake ni Hagari, na watoto wake wanazaliwa utumwani.[#4:24-30 Kuanzia aya ya 24 Paulo anataja wazi kwamba anayoyaeleza hapa ni kisa chenye maneno ambayo yanaweza kutumiwa kuwa na maana nyingine, na ndivyo anavyofanya. Sehemu hii ni ngumu na imewatatiza wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu. Tatizo hilo linaonekana hapa hapa katika aya hii Paulo anapoanza kubainisha kati ya hao mama wawili na kusema ni wawakilishi wa maagano mawili.]

25Hagari anawakilisha mlima Sinai ulioko Arabia, na ni mfano wa Yerusalemu ya sasa, ulio mtumwa pamoja na watoto wake.[#4:25 Ugumu wa maelezo ya Paulo unaongezeka hapa. Kuna pia hati kadhaa za kale ambazo hazina Hagari hapa.]

26Lakini Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu.[#4:26 Picha au mfano wa watu wapya wa Mungu (Fil 3:20; Ebr 12:22-23).]

27Maana imeandikwa:

“Furahi, ewe uliye tasa usiyezaa;

paza sauti wewe usiyepata kujifungua mtoto;

maana watoto wa yule aliyeachwa ni wengi

kuliko wa yule aliye na mume.”

28Sasa, basi, ndugu zangu, nyinyi ni watoto wa Mungu kutokana na ahadi yake kama alivyokuwa Isaka.

29Lakini kama vile siku zile yule mtoto aliyezaliwa kwa njia ya kawaida alimdhulumu yule aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho wa Mungu, vivyo hivyo na siku hizi.[#4:29 Yaani Ishmaeli, mtoto wa Hagari (4:23 maelezo).; #4:29 Yaani Isaka, mtoto wa Sara. Rejea Mwa 21:9.]

30Lakini Maandiko Matakatifu yasemaje? Yasema: “Mfukuze mama mtumwa pamoja na mwanawe; maana mtoto wa mtumwa hatarithi pamoja na mtoto wa mama huru.”

31Hivyo basi, ndugu, sisi si watoto wa mtumwa bali wa mama huru.[#4:31 Aya hii inamalizia wazo lote lililoshikilia sura 3—4 pamoja. Itakumbukwa kwamba Wayahudi walijigamba kuwa wazawa wa Abrahamu na mkewe Sara, tofauti na Waishmaili ambao walikuwa wazawa wa Abrahamu na Hagari. Lakini Paulo katika kufafanua kwake kwa kutumia lugha ya kimfano (aya 24-31) anapindua namna hiyo ya kufikiri kwa kuwafanya Wayahudi wawe ndio wazawa (kiroho) wa Hagari ambaye ni mtumwa, hali Wakristo ambao wanamwamini Kristo kuwa ndio hasa walio wazawa wa Sara, ambaye ni huru. Jambo hili au namna hiyo yote ya kufikiri inawiana na kilichosemwa katika Rom 4:13-25 na Gal 3:7,9,29, yaani wale wanaomwamini Yesu ndio wazawa halisi wa Abrahamu, wawe Wayahudi au watu wa mataifa mengine.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania