The chat will start when you send the first message.
1Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, nyinyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa.
2Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo.[#6:2 Rejea Rom 15:1. Na kuhusu “mizigo” taz 6:5 maelezo.; #6:2 Yaani, sheria ya upendo. Rejea Yoh 13:34; 15:12,17; 1Yoh 3:23.]
3Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe.
4Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine.
5Maana kila mmoja anapaswa kuubeba mzigo wake mwenyewe.[#6:5 Ingawa tafsiri hii ina “mzigo”, hapa na katika aya ya 2, huenda hapa katika aya ya tano, mzigo unaotajwa unajumuisha chochote kigumu ambacho kinamkabili Mkristo. Kwa hiyo matatizo ya maisha na hata udhaifu. Wengine wanafikiri katika aya hii ya tano ni mambo ambayo yanamfikia mtu kutokana na mwenendo wake, kwa maana ya kila mtu anawajibika kwa mwenendo wake.]
6Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake.
7Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna.[#6:7 Hapa kuna misemo miwili “Mungu hafanyiwi dhihaka” na “Alichopanda mtu ndicho atakachovuna”, misemo ambayo inafafanuliwa zaidi katika 6:8-10. Rejea Meth 22:8; Hos 8:7.]
8Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uhai wa milele.
9Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake.
10Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu.
11Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe.[#6:11 Rejea 1Kor 16:21. Baadhi wanafikiri Paulo alitamka maneno ya barua yote tangu mwanzo na huyo aliyekuwa anamsadia kuandika akayaandika mpaka hapa, kisha Paulo akaandika yaliyofuata yeye mwenyewe. “Herufi kubwa” madhumuni yake hapa labda ni kwa ajili ya kutilia mkazo kilichosemwa au ni namna tu ya Paulo ya kuandika.]
12Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha nyinyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo.
13Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; huwataka nyinyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu.
14Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu.[#6:14 Kwa maana ya “kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo msalabani” ndicho kinachoweza kumfanya Paulo ajivunie chochote.]
15Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya.[#6:15 Gal 5:6; rejea 1Kor 7:19. Na kuhusu “kiumbe kipya” rejea 2Kor 5:17.]
16Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli — watu wa Mungu.[#6:16 Yamkini maneno hayo yanatumika kutaja jumla ya kanisa lote la Mungu.]
17Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu.[#6:17 Yamkini ni mateso ambayo yalimpata kutokana na kazi yake ya kitume (rejea 2Kor 11:23-27), kama kushiriki katika mateso ya Kristo (rejea 2Kor 1:5; Kol 1:24).]
18Ndugu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amina.