The chat will start when you send the first message.
1Kila kuhani mkuu ambaye huchaguliwa miongoni mwa watu hupewa jukumu la kushughulikia mambo ya Mungu kwa niaba ya watu, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi.
2Maadamu yeye mwenyewe ni dhaifu, anaweza kuwatendea kwa huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa.
3Kwa sababu hiyo anapaswa kutoa tambiko si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.
4Hakuna mtu awezaye kujifanya mwenyewe kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni.
5Hali kadhalika naye Kristo; yeye hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu alimteua na kumwambia:
“Wewe ni Mwanangu;
mimi leo nimekuwa baba yako.”
6Alisema pia mahali pengine:
“Wewe ni kuhani milele,
kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.”
7Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kifoni; naye alisikilizwa kwa sababu ya kumcha Mungu.[#5:7 Yahusu mateso ya Yesu kule Gethsemane (taz Mat 26:36-46 na sehemu sambamba katika Injili nyingine).]
8Lakini, ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kutii kwa njia ya mateso.[#5:7-8 Fil 2:8; rejea Mat 26:39 na sambamba zake.]
9Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii,
10naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.
11Tunayo mengi ya kusema juu ya jambo hili, lakini ni vigumu kuwaelezeni, kwa sababu nyinyi si wepesi wa kuelewa.[#5:11 Yaani kuhusu ukuhani wa Kristo na wadhifa wake.]
12Kwa wakati huu nyinyi mngalipaswa kuwa waalimu tayari, lakini mnahitaji bado mtu wa kuwafundisheni mafundisho ya mwanzo juu ya neno la Mungu. Mnahitaji maziwa badala ya chakula kigumu.[#5:12-13 Namna hii ya kusema juu ya kukomaa na kutokomaa katika maisha ya Kikristo tunaikuta pia katika 1Kor 3:1-2; rejea pia 1Pet 2:2.]
13Kila anayepaswa kunywa maziwa ni mtoto bado, hajui uadilifu ni nini.
14Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu waliokomaa, waliofunzwa kwa vitendo kubainisha mema na mabaya.