The chat will start when you send the first message.
1Wakati huo wanawake saba watamvamia mwanamume mmoja na kumwambia, “Chakula na mavazi tutajitafutia wenyewe, lakini wewe utuondolee aibu yetu, uturuhusu tuitwe kwa jina lako.”[#4:1 Mume alikuwa na jukumu la kumpatia mkewe (na hata hawara wake) mahitaji yake. Lakini kutokana na maangamizi na kupotea vitani kwa wanaume, wanawake waliachilia haki hizo zao kama wake ili kuepa aibu ya kubaki bila waume na watoto (rejea Mwa 30:23; 1Sam 1:6).]
2Siku ile, tawi atakalochipusha Mwenyezi-Mungu litakuwa zuri na tukufu, nayo matunda ya nchi yatakuwa ya fahari na utukufu kwa wale Waisraeli watakaosalia. Waisraeli watakaobaki watayaonea fahari na kujivunia mazao ya nchi yao.[#4:2-6 Katika maandishi ya manabii mara nyingi ujumbe wa matumaini ya hali njema hufuata ujumbe wa hukumu na adhabu. Maneno: “Waisraeli watakaobaki”, au: “mabaki ya Waisraeli” (aya 2), yanaingiza hapa dhamira muhimu katika vitabu vya manabii, yaani: Mungu atajisalimishia sehemu ya watu wake na hatawaacha waangamizwe wote. Hao “wachache” ambao Mungu, kwa kupenda kwake, atawaokoa wanatajwa mara kwa mara (rejea Isa 1:9; 10:20-22; 11:10-16; 28:5; 37:4,30-32). Taz pia Isa 6:13; 7:3 (na pia 1Fal 19:18; Ezra 9:15).]
3Wale watakaosalia hai mjini Yerusalemu, naam, wale watakaobaki huko Siyoni, wataitwa “Wateule wa Mungu”; hao ndio wale wote watakaokuwa wameandikwa kitabuni mwake waishi huko Yerusalemu.
4Kwa roho yake, Bwana atawaweka sawa na kuwatakasa. Na atakapokwisha kuwatakasa wanawake wa Siyoni uchafu wao na kufuta madoa ya damu yaliyomo humo Yerusalemu,
5hapo atafanya kila mahali juu ya mlima Siyoni na juu ya mikutano ya watu kuwe na wingu wakati wa mchana, na moshi na moto uwakao vizuri wakati wa usiku. Zaidi ya hayo utukufu wa Mungu utaufunika na kuulinda mji wote.[#4:5-6 Kama ilivyotukia njiani jangwani baada ya Waisraeli kuokolewa kutoka Misri (Kut 13:21-22; 40:34-38; rejea pia Kut 24:16).]
6Utukufu wake utakuwa kwao kivuli kuwakinga na joto la mchana; na kimbilio na kinga yao wakati wa dhoruba na mvua.