The chat will start when you send the first message.
1Hapo mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu.[#1:1 Yaani kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu.]
2Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu.
3Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye.
4Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu.[#1:4 Au, “Kilichoumbwa kilikuwa na uhai kwa kuungana na Neno.”; #1:4 Yesu Kristo aliwaangazia waamini watoke gizani (taz aya ya 5). Mwanga huo unawawezesha watu kuwa na uhai (1:9,13; Zab 36:9) na kujua matakwa ya Mungu kuhusu maisha yao. Mwanga na giza ni mada muhimu kabisa katika Injili ya Yohane. Yohane anatumia maneno hayo mawili yaliyo kinyume kueleza mapambano kati ya wale wanaompokea Yesu Kristo na wale wanaokataa kumwamini (1:19-21; 8:12-20).]
5Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.[#1:5 Au, “halikuweza kuutambua.”]
6Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane,[#1:6 Yoh 6-8 inatuletea habari za Yohane Mbatizaji ambaye, kwa mahubiri yake na ubatizo, alitayarisha njia kwa ajili ya Yesu (1:19-34; Mat 3:1; Marko 1:4; Luka 1:17,76; 3:1-2).]
7ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini.
8Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga.
9Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote.
10Basi, Neno alikuwako ulimwenguni, na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua.[#1:10 Matumizi ya “ulimwengu”, hapa mara tatu, yaweza kuwa na vitofauti vidogo vya maana. Kwanza “Neno … ulimwenguni” bado tupo katika mazingira kama yale ambayo yanahusu ulimwengu ulioumbwa, pili, ulimwengu unaokaliwa na binadamu, na tatu ulimwengu, yaani binadamu wenyewe na udhaifu wao. Hali hii ya tatu ndiyo inayohusika na kukosa kumtambua huyo Neno.]
11Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea.[#1:11 Nchi ya watu wa Israeli ambao kwa jumla hawakumpokea Yesu.]
12Lakini wale waliompokea, wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu,[#1:12 Yohane anatilia mkazo sana umuhimu wa kumwamini Yesu Kristo. Kuamini ndilo jibu linalotakiwa kwa bnadamu kuhuusu kitendo cha Mungu cha kuwaokoa watu kwa njia ya Yesu Kristo. Jibu hilo sharti lifanyike kwa moyo wote, kwa akili yote na nafsi yake yote. Mtu anapoamini anapokea uhai wa milele (rejea Yoh 3:14-16; 6:40; 11:25-26; 20:31).]
13ambao walizaliwa si kwa maumbile ya kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala mapenzi ya mtu, bali kutokana na Mungu mwenyewe.
14Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli.[#1:14 Neno linalotumika katika Kigiriki na ambalo limetafsiriwa hapa kama “mwanaadamu” ni “Sarks” ambalo latilia mkazo hali hafifu ya watu na hivyo kuonesha kwamba Neno alikuwa mtu kwelikweli na sio alionekana kama mtu (taz Rom 1:3; Gal 4:4; Fil 2:7; 1Tim 3:16; Ebr 2:14; 1Yoh 4:2).; #1:14 Tafsiri ya neno ambalo lakumbusha makao (Hema) ya Mungu na utukufu wake miongoni mwa watu wa Israeli (Kut 40:34). Neno “Utukufu” hapa linadhihirisha siyo tu kuweko kwake Mungu bali na kitendo chake cha fahari kwa ajili ya kuwaokoa watu wake (1Fal 8:10-11; Isa 6:3; 58:8; 60:1; Yoh 2:11; 17:5).; #1:14 Mwana wa pekee kimaana ni sambamba na mwana mpendwa au mwana mpenzi.; #1:14 “Neema na Kweli” yanatukumbusha “fadhili na ukweli” ambayo yasemwa juu ya Mungu mwenyewe katika A.K. (khesed we’imet). Tazama Kut 34:6; Zab 25:10; 26:3; 36:5; 57:3,10; 85:10 ambamo yanaeleza uhusiano wa Mwenyezi-Mungu na watu wake.]
15Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: ‘Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.’”
16Kutokana na ukamilifu wake sisi sote tumepokea neema kupita neema.
17Maana Mungu alitoa sheria kwa njia ya Mose, nayo neema na kweli vimetujia kwa njia ya Yesu Kristo.
18Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.[#1:18 A.K. kama vile A.J. yanapatana kuhusu wazo kwamba Mwenyezi-Mungu haonekani kwa macho ya binadamu (Kut 33:20; Yoh 6:46; 1Tim 6:16; 1Yoh 4:12). Lakini kumwona Yesu Kristo ni kumwona Mungu (Yoh 14:9).; #1:18 Mat 11:27; Luka 10:22; 1Yoh 1:2.; #1:18 Maneno yanayojaribu kutafsiri kile kinachosemwa neno kwa neno: “ambaye yuko kifuani mwa Baba” msemo ambao una lengo la kuonesha uhusiano wa karibu mno na Baba.]
19Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani na Walawi, wamwulize: “Wewe u nani?”[#1:19 Hapa na mahali pengine katika Injili hii, viongozi ni neno linalowataja wakuu wa kidini wa Wayahudi kama vile Mafarisayo (taz aya 24 na 2:18; 5:10; 7:1).]
20Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.”
21Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Elia?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!”[#1:21 Nabii wa Kiyahudi ambaye aliaminiwa kuwa angerudi tena duniani kutayarisha njia ya Bwana (Mal 4:5-6). Katika Mat 11:4; 17:11-13 na Marko 9:13 Yesu anasema juu ya Yohane Mbatizaji kana kwamba ndiye Elia ambaye alikuwa aje.; #1:21 Kulingana na Kumb 18:15,18 Mose aliahidi kuwa Mungu angemtuma nabii mwingine kama yeye.]
22Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.”
23Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake:
‘Sauti ya mtu anaita jangwani:
Nyosheni njia ya Bwana.’”
24Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo.[#1:24 Au: Hao walikuwa Mafarisayo. Hawa viongozi wa dini walizingatia sana kufuata sheria ya Mungu.]
25Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Masiha, wala Elia, wala yule nabii, mbona wabatiza?”
26Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado.
27Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.”[#1:27 Kumfungulia mtu kamba za viatu vyake ilikuwa kazi duni iliyofanywa na mtumwa.]
28Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng'ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.[#1:28 Mahali hapo hapajulikani vizuri; huenda palikuwa upande wa mashariki wa Mto Yordani. Mji wa jina hilo hilo unatajwa katika Agano Jipya nao ni ule ulio kilomita tatu kutoka Yerusalemu.]
29Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu![#1:29 Yohane Mbatizaji alisema Yesu alikuwa kama yule mwanakondoo ambaye angepelekwa kuchinjwa ili kurekebisha watu wa Mungu kwa kuiondoa dhambi yao (1:29). Taz pia Isa 1:29; 53:4-12. Maana inayoambatana zaidi na wazo la Isaya ndiyo inayoonekana kueleweka na wale wanafunzi wa Yohane. Yaani, Yesu ndiye yule aliye kama mwanakondoo atakayerejesha upya hali njema ya watu wa Mungu na kutokana na kuelewa huko wale wanafunzi wa Yohane wakamfuata Yesu. Paulo anamtaja Yesu pia kama Mwanakondoo wa Pasaka “Kristo Pasaka yetu amekwisha tolewa kuwa sadaka” (1Kor 5:7). Taz pia Rom 3:24-25; Ebr 10:2-14 na Ufu 5:6-6:3. Katika mazingira hayo ya Ufunuo, huyo Mwanakondoo ndiye aliye pia “simba wa kabila la Yuda” na “chipukizi wa Daudi”. Mwanakondoo wa Mungu anajumuisha hayo yote.; #1:29 Yaani uasi wa binadamu, ulimwengu ukitumika hapa kwa maana ya wakazi wake.]
30Huyu ndiye niliyeongea juu yake niliposema: ‘Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!’
31Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua.”
32Yohane alishuhudia hivi: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.[#1:32-34 Mat 3:11,16-17 na sambamba zake; Mate 1:5; 2:1-4 (rejea Isa 11:1-2; 42:1; 61:1).]
33Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma kubatiza watu kwa maji alikuwa ameniambia: ‘Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’[#1:33 Kama vile Mungu alivyommiminia Yesu Roho wake vivyo hivyo naye Yesu mwenyewe atawamiminia Roho wote watakaomfuata.]
34Mimi nimeona na nimeshuhudia kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu.”[#1:34 Baadhi ya hati za kale zina “Mteule wa Mungu.” Na kuhusu “Mwana wa Mungu” taz Fahirisi.]
35Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili.[#1:35 Mmoja alikuwa Andrea, aya 40.]
36Alipomwona Yesu akipita, akasema, “Tazameni! Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu.”
37Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu.
38Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, “Mnatafuta nini?” Nao wakamjibu, “Rabi, (yaani Mwalimu), unakaa wapi?”
39Yesu akawaambia, “Njoni, nanyi mtaona.” Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni.
40Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu.
41Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, “Tumemwona Masiha” (maana yake Kristo).
42Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa” (Kigiriki ni Petro, yaani, “Mwamba”).[#1:42 Jina la Kiaramu “Kefa” na Kigiriki “Petro” yote yana maana ya mwamba.]
43Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
44Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro.[#1:44 Ni Bethsaida Yulia, mji kaskazini ya ziwa Galilaya ambao ulijengwa na Filipo mtawala wa mikoa ya Iturea na Trakoniti.]
45Naye Filipo akamkuta Nathanaeli, akamwambia, “Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti.”[#1:45 Yaani Maandiko Matakatifu ya Wayahudi ambayo yajulikana kwa Wakristo kama Agano la Kale.; #1:45 Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida na huenda aliwajua Andrea na Simoni. Jina Nathanaeli katika Kiebrania lina maana ya “Mungu hupeana”. Yeye anamtambua Yesu kama Mwana wa Mungu na mfalme wa Israeli (1:49). Na kuhusu “Mwana wa Yosefu kutoka Nazareti” itakumbukwa kwamba Mathayo na Luka wanazo habari kwamba Maria, mama yake Yesu, alikuwa bikira wakati alipomchukua mimba (Mat 1:18; Luka 1:30-35). Katika orodha ya ukoo wake Yesu (Luka 3:23-33) Luka anaanza kwa kutamka wazi kwamba watu walidhani kuwa Yesu alikuwa mtoto wa Yosefu (Luka 3:23).]
46Naye Nathanaeli akamwuliza Filipo, “Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.”
47Yesu alipomwona Nathanaeli akimjia, alisema juu yake, “Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake.”
48Naye Nathanaeli akamwuliza, “Umepataje kunijua?” Yesu akamwambia, “Ulipokuwa chini ya mtini, hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona.”
49Hapo Nathanaeli akamwambia, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!”[#1:49 Fungu hili la maneno ni jina la sifa linalotumiwa kumtaja Masiha. Yohane analitumia kwa maana ya pekee. Rejea 6:15; 18:33-36; 19:19.]
50Yesu akamwambia, “Je, umeamini kwa kuwa nimekuambia kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya.”
51Yesu akaendelea kusema, “Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu.”[#1:51 Taz Mwa 28:12. Yamkini hapa, kama vile pale katika A.K., Mwana wa Mtu yaani Yesu amekuwa sababu ya kuwafungulia binadamu uzi wa kufikia mambo ya mbinguni. Kuna mawasiliano sasa kati ya mbinguni na dunia kwa njia ya Mwana wa Mtu.]