Yohane 8

Yohane 8

Yesu mwanga wa ulimwengu

12Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, “Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uhai.”[#8:12 Yesu anatetea ukweli wa ujumbe wake na kwamba amekuja ulimwenguni kusudi watu waone jinsi Mungu alivyo. Itakumbukwa pia kwamba katika Mat 5:14 wale wanafunzi wake pia wanasemwa kuwa ni mwanga wa ulimwengu. Taz pia Yoh 9:5.]

13Basi, Mafarisayo wakamwambia, “Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi wako si halali.”

14Yesu akawajibu, “Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini nyinyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda.

15Nyinyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu.

16Hata nikihukumu, hukumu yangu ni halali kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami.

17Imeandikwa katika sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali.

18Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia.”

19Hapo wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?” Yesu akawajibu, “Nyinyi hamnijui mimi wala hammjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia.”

20Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.[#8:20 Huenda mahali hapo palikuwa katika ukumbi wa wanawake, karibu na mahali palipokuwa na vijisanduku vya kuweka sadaka. Taz Luka 21:1.; #8:20 Taz 2:4 maelezo.]

Niendako nyinyi hamwezi kufika

21Yesu akawaambia tena, “Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, nyinyi hamwezi kufika.”[#8:21 Yaani watakufa wakiwa hawajaachana na dhambi zao au hawajasamehewa (taz pia aya ya 24; ling Kumb 6:23; 8:10).]

22Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Mbona anasema: ‘Niendako nyinyi hamwezi kufika?’”

23Yesu akawaambia, “Nyinyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; nyinyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.[#8:23 Yesu anadokezea kwa maneno hayo kwamba yeye ametoka kwa Mungu. Lakini pia matumizi ya “ulimwengu” ambako hao wanaompinga wametoka ni ya kimfano kuelezea eneo ambalo katika Maandiko Matakatifu ni eneo la wenye kumpinga Mungu (15:18-19; Gal 6:14).]

24Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba ‘Mimi Ndimi Niliye’, mtakufa katika dhambi zenu.”[#8:24 Maneno ambayo, kulingana na maana yake, karibu ni sawa na yale yaliyotumiwa katika Kut 3:14 pale Mungu alipojitambulisha kwa Mose na watu wa Israeli kama “Mimi Ndimi”. Katika sehemu hiyo ya Kut 3 Mwenyezi-Mungu (Kiebrania: “Yahweh”) ndiye aliye kweli au ndiye mwenye kusababisha kuweko. Yaani yewye ni chanzo cha chochote kilichopo. Katika Injili ya Yohane Yesu anatumia msemo huo kujiunga na dhana au mawazo hayo juu ya Mungu na kueleza yale ambayo Mungu alimwagiza ayatekeleze ulimwenguni.]

25Nao wakamwuliza, “Wewe ni nani?” Yesu akawajibu, “Nimewaambieni tangu mwanzo![#8:25 Au: “Ya nini hata niongee nanyi?”]

26Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake.”

27Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba.

28Basi, Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu, hapo ndipo mtakapojua kwamba ‘Mimi Ndimi Niliye’, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu yale Baba aliyonifundisha.[#8:28 Wazo linalogusiwa hapa ni lile la kifo cha Yesu msalabani (taz Yoh 3:14). Katika 3:14 Yesu anasema atainuliwa juu kama Mose alipoinua juu yule nyoka wa shaba kusudi waliotazama nyoka huyo waweze kuponywa, na kwa namna hiyo hiyo wale wanaomtazama Yesu katika hali yake ya kuinuliwa juu msalabani wataweza nao kuponywa.; #8:28 Taz 8:24 maelezo.]

29Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza.”

30Baada ya kusema hayo watu wengi walimwamini.

Ukweli utawapeni uhuru

31Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu.

32Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru.”

33Nao wakamjibu, “Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: ‘Mtakuwa huru?’”

34Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi.[#8:34 Baadhi ya hati za kale zina: Kila mtu atendaye dhambi ni mtumwa.]

35Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu.

36Mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli.

37Najua kwamba nyinyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamyakubali mafundisho yangu.

38Mimi nasema yale aliyonionesha Baba, lakini nyinyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu.”

39Wao wakamjibu, “Sisi ni watoto wa Abrahamu!” Yesu akawaambia, “Kama nyinyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu.

40Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, nyinyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo!

41Nyinyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya baba yenu.” Wao wakamwambia, “Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu.”

42Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.

43Kwa nini hamuelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamuezi kuusikiliza ujumbe wangu.

44Nyinyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo.[#8:44 Maneno haya ni upeo wa ubishi kati ya Yesu na hao waliotajwa katika aya ya 30. Ibilisi au Shetani ni kiongozi wa nguvu zote zinazopingana na Mungu. Yesu alikuja ulimwenguni kushinda nguvu hizo za Shetani au Ibilisi.]

45Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana nyinyi hamniamini.

46Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini?

47Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini nyinyi hamsikilizi kwa sababu nyinyi si watu wa Mungu.”

Yesu alikuwako kabla ya Abrahamu

48Wayahudi wakamwambia, “Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena una pepo?”[#8:48 Walitumia msemo huo kwa kumdharau kwani Wayahudi na Wasamaria hawakushirikiana.]

49Yesu akajibu, “Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini nyinyi hamniheshimu.

50Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo, naye ni hakimu.

51Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele.”

52Basi, Wayahudi wakasema, “Sasa tunajua kweli kwamba wewe una pepo! Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, ‘Anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele!’[#8:52 Hapa ni dhahiri watu hawakuelewa maana ya yale aliyosema Yesu kwamba hawatakufa kama wakimtii yeye. Walifikiri kwamba alikuwa anasema juu ya kuishi daima hapa duniani. Tazama 3:4 ambapo pana kutokuelewa kwa namna hiyo hiyo.]

53Je, unajifanya mkuu kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na manabii walikufa. Wewe unajifanya kuwa nani?”

54Yesu akawajibu, “Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Baba yangu ambaye nyinyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza.

55Nyinyi hamjapata kumjua, lakini mimi namjua. Na, nikisema simjui, nitakuwa mwongo kama nyinyi. Mimi namjua na ninashika neno lake.

56Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona, akafurahi.”

57Basi, Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona Abrahamu?”[#8:57 Baadhi ya hati za kale zina: Abrahamu amekuona?]

58Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi niko.”[#8:58 Au: “Mimi ndimi” kama 8:24.]

59Hapo wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania