The chat will start when you send the first message.
1Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote nchini kote wahesabiwe.[#2:1 Katika Mathayo tunadokezewa kwamba Yesu alizaliwa muda mfupi kabla ya kufa kwake Herode (Mat 2:15,19-20); #2:1 Mfalme wa Kiroma alitawala tangu mwaka 27 K.K. mpaka 14 B.K.; #2:1 Yaani katika dola yote ya utawala wa Waroma.]
2Sensa hiyo ilikuwa mara ya kwanza, wakati Kurenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria.[#2:2 Au: ilikuwa kwa lengo la kuweza kutoa makadirio ya kodi.; #2:2 Tafsiri nyingine yamkini: Kulingana na kumbukumbu za kihistoria, Kurenio alifanya sensa mwaka 6 au 7 B.K. wakati alipokuwa mkuu wa mkoa wa Kiroma wa Siria; si dhahiri ni sensa ipi anayotaja Luka. Lengo la sensa lilikuwa kufanya makadirio ya kodi.]
3Basi, wote waliohusika walikwenda kuhesabiwa kila mtu katika mji wake.[#2:3 Bila shaka mji wa wazee wake.]
4Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya, na kwa vile alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi, alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yudea, alikozaliwa mfalme Daudi.[#2:4 Karibu na Yerusalemu, kijiji alikozaliwa mfalme Daudi.; #2:4 Daudi mwenyewe anajulikana kama mwana wa Mwefrathi mmoja wa Bethlehemu katika Yuda (1Sam 17:12) au kama mwanawe Yese wa Bethlehemu (1Sam 17:58).]
5Alikwenda kuhesabiwa pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mjamzito.[#2:5 Kama katika Luka 1:27; angalia pia Mat 1:18-25.]
6Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia,
7akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.[#2:7 Kijadi mzaliwa wa kwanza wa kiume alikuwa na haki na majukumu ya namna kwa namna kuhusu urithi. Yesu anaitwa mzaliwa wa kwanza katika Rom 8:29; Kol 1:15; Ebr 1:6; Ufu 1:5 kuonesha kwamba yeye anayo mamlaka juu ya ulimwengu wote na viumbe vyake vyote.; #2:7 Neno la Kigiriki lililotafsiriwa hapa laweza kuwa na maana ya zizi lenyewe au hori yaani pale ambapo paliwekwa majani ili wanyama wapate kula.]
8Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao.[#2:8 Wa kwanza kupata habari za kuzaliwa kwake Yesu Kristo ni watu ambao walionekana kuwa wa tabaka la chini - wachungaji. Kama ilivyo mahali kadha wa kadha katika Injili hii, maskini, wanyonge na wasio na makuu, yaani wanyenyekevu ndio wanaochaguliwa kupokea zawadi na fadhili za Mungu. Angalia pia 4:18-19; 6:20-26]
9Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana.[#2:9 Tazama maelezo ya 1:11.; #2:9 Utukufu ni tafsiri ya neno la Kigiriki ambalo lina maana kadha wa kadha kulingana na jinsi linavyotumika. Hapa lina maana ya “fahari” au “mng'ao” unaoandamana na kutokea kwa Mungu ambako kunaonekana kwa watu wake (taz Kut 16:7,10; 24:17 n.k.).]
10Malaika akawaambia, “Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kubwa itakayowapata watu wote.[#2:10 (Nawatangazieni) habari njema: (taz 1:19).]
11Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana.[#2:11 Neno hili lilitumiwa kama kisifa cha Mungu (1:47) na sasa latumiwa kumtaja Yesu ambaye katika 1:67 alitajwa kama Mwokozi shujaa. Wayahudi wengi walimtazamia mtu atakayewaokoa kutoka udhalimu wa maadui, yaani mwokozi wa kisiasa. Lakini tangazo hili lahusu kuokolewa kutoka dhambi na kifo (Mat 1:21; Yoh 4:42).; #2:11 Jina lingine la cheo ambalo linamtaja Yesu. Kigiriki maana yake “Aliyepakwa mafuta”; kupakwa mafuta kwa ajili ya kazi maalumu. Kiebrania ni “Masiha” neno ambalo latumika kumtaja mtu aliyepakwa mafuta na kutumwa kwa kazi maalumu na Mungu. Kitendo hicho walifanyiwa wafalme, baadhi ya manabii na makuhani kuwasimika katika nyadhifa zao. Katika Mate 2:3 tunaambiwa dhahiri kwamba Mungu amemfanya Yesu kuwa Bwana na (au: Yeye ndiye Mkombozi wa watu ambaye alitumwa rasmi na Mungu.; #2:11 Neno ambalo katika Kigiriki lilitumika kumtaja mwanamume kwa heshima. Biblia ya Septuajinta ilitumia neno hilo (Kurios) pale jina la Mungu (Yahweh) lilipotumika hali kadhalika pia pale neno: Adon (Adonay), lilipotumika. Katika tafsiri hii mpya jina la Mungu ni Mwenyezi-Mungu na Adon/Adonay ni Hapa katika Luka 2:11, Bwana ingawa lingeweza kumtaja Mwenyezi-Mungu, linamtaja Yesu na mara nyingi katika A.J. Yesu anatajwa kwa neno hilo la heshima (Mate 2:36; Rom 10:9; Fil 2:11).]
12Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini.”
13Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema:
14“Utukufu kwa Mungu juu mbinguni,[#2:14 “Juu” ni mbinguni kwa Mungu na kwa sababu hiyo tafsiri hii ina: “mbinguni”. Matumizi ya utukufu hapa ni kumsifu Mungu - kusema na kutambua fahari kuu ya Mungu.]
na amani duniani kwa watu anaowafadhili!”
15Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: “Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha.”
16Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini.
17Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake.
18Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji.
19Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake.
20Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa.
21Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.[#2:21 Tazama maelezo ya Luka 1:59.; #2:21 Taz 1:31,59. Mkazo hapa ni juu ya jina na sio juu ya kutahiriwa.]
22Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na sheria, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele za Bwana.[#2:22 Neno kwa neno: (yaani wingi, kwa maana ya walau Yosefu na Maria). Baadhi ya hati za mkono za kale zina: (umoja) yaani Maria. Kadiri ya Lawi 12:2-4 ibada hiyo ya utakaso ilimhusu tu mama mtoto ambaye kwa kujifungua mtoto alisemekana kuwa najisi kidini. Luka anapendelea kutumia wingi kwa kumjumuisha pia Yosefu na hata mtoto Yesu, ambaye alikwenda nao wamwoneshe hekaluni kwa Bwana, yaani Mwenyezi-Mungu.; #2:22 Yaani kuteuliwa au kuzinguliwa. Baada ya kujifungua mtoto desturi ya Kiyahudi ilimtaka mama mtoto akae siku 40 kabla ya kwenda hekaluni kutoa tambiko ya kutakaswa, na kwa mujibu wa sheria ya Mose mtoto huyo wa kiume akiwa wa kwanza ilikuwa lazima akombolewe (Kut 13:11-12). Mtoto alikombolewa kwa kutoa tambiko: mwanakondoo na njiwa au hua wawili ikiwa aliyehusika hakuweza kupata mwanakondoo na njiwa (Lawi 12:2-8).; #2:22 Yafaa kukumbuka kwamba kadiri ya Kutoka 13:1-2, Mungu alimwambia Mose kumweka wakfu kwa Mungu kila mzaliwa wa kwanza na kwamba kiasi cha fedha (shekeli) apewe kuhani aliyehudumu wakati huo, mtoto alipokuwa na umri wa mwezi mmoja.]
23Katika sheria ya Bwana imeandikwa: “Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana.”
24Pia walikwenda ili watoe sadaka: hua wawili au makinda mawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika sheria ya Bwana.[#2:24 Yaani sheria ambayo Bwana (Mungu) alimpa Mose.]
25Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye.[#2:25 Wafafanuzi mbalimbali huelewa maneno haya kwa namna tofautitofauti. Lakini yafaa kutazama maandishi ya Luka kuonesha ni maana ipi inayoafiki zaidi hapa. Angalia na kulinganisha: 2:38 (watu wanaongojea kukombolewa kwa Yerusalemu), na 23:50-51 (Yosefu wa Arimathaya alikuwa anangojea ufalme wa Mungu). Kwa jumla ndilo tumaini walilokuwa nalo watu kuhusu Masiha (ling Isa 40:1-2; 49:13; 57:18; 61:2 na Mat 5:4). Kadhalika, tazama 2:29.]
26Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Kristo wa Bwana.
27Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na sheria,[#2:27 Neno kwa neno: Yaani Luka anataka kusema kuja kwake Simeoni hekaluni wakati huu kulikuwa kwa msukumo au uongozi wa Roho Mtakatifu. Kwa kuwa hapa ni dhahiri yahusu Roho wa Mungu tafsiri hii yasema wazi ni Roho Mtakatifu.]
28Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu, akisema:
29“Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako,
umruhusu mtumishi wako aende kwa amani.
30Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu ulioleta,
31ambao umeutayarisha uonekane na watu wote:
32Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa,
na utukufu kwa watu wako Israeli.”
33Baba yake Yesu na mama yake walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto.[#2:33 Ndivyo, kulingana na hati za mkono za awali maarufu zaidi (taz aya 48). Yosefu kama mchumba wake Maria aliitwa baba yake Yesu kisheria.]
34Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu;[#2:34 Yaani akawaombea baraka na furaha kutoka kwa Mungu au akawatakia heri.; #2:34 Neno kwa neno; Kwa wale watakaomwamini watasalimishwa, ila wengine wasioamini watapotea (taz 20:17-18).]
35na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako.”[#2:35 Matamshi haya yanaelekezwa kwa Maria labda kwa vile Luka anayo kumbukumbu ya mapokeo kuhusu tukio linalosimuliwa na Yoh 19:25.]
36Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa.[#2:36 Wanawake kadhaa wanasemwa kuwa manabii katika Biblia: Miriamu (Kut 15:20), Debora (Amu 4:4), Hulda (2Fal 22:14) na binti za Filipo (Mate 21:9). Yesu anajulishwa sio tu kwa wanaume bali pia kwa wanawake.]
37Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana.[#2:37 Au:; #2:37 Yafaa kutaja hapa kwamba hekalu lenyewe, licha ya kuwa na sehemu zile maalumu za ibada lilikuwa pia na vyumba kadha wa kadha na huenda Ana aliishi katika chumba kimojawapo, au kwamba alitumia muda wake wote kuhudhuria ibada hekaluni.]
38Saa hiyohiyo, alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na kueleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu.
39Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, wilayani Galilaya.
40Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa naye.
41Wazazi wake walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka.[#2:41 Hiyo ilikuwa sikukuu ya kidini iliyoadhimishwa kukumbuka tukio la kuokolewa Waisraeli kutoka utumwani Misri. Jina lenyewe Pasaka latokana na neno la Kigiriki lilotumiwa kutaja sikukuu ya Kiebrania katika Kut 12:13 (taz pia aya 23,27). Sikukuu hiyo iliadhimishwa tarehe 14 Mwezi wa Nisani (yapata Machi/Aprili katika kalenda yetu).]
42Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi.[#2:42 Kulingana na mila na desturi za kidini za Wayahudi mtoto wa miaka kumi na miwili alitakiwa kujiweka tayari kuingia na kufuata maadili ya jumuiya ya kidini. Kuingizwa rasmi kulifanyika mtoto akiwa na umri wa miaka kumi na mitatu.]
43Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari.
44Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki.
45Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta.
46Siku ya tatu, walimkuta hekaluni kati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.
47Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima.
48Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, “Mwanangu, kwa nini umetutendea hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni.”
49Yeye akawajibu, “Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?”[#2:49 Tafsiri nyingine yamkini: …]
50Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia.
51Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake.
52Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.[#2:52 Ling na na 1Sam 2:26; Meth 3:4.]