Zaburi 101

Zaburi 101

Mwongozo mzuri wa mfalme

1Utenzi wangu kuhusu uaminifu na haki;

ninauimba kwa heshima yako, ee Mwenyezi-Mungu.

2Nitazingatia mwenendo usio na hatia.

Je, utakuja kwangu lini?

Nitaishi kwa unyofu nyumbani kwangu;

3sitavumilia kamwe upuuzi.

Nayachukia matendo ya watu wapotovu,

mambo yao hayataambatana nami.

4Upotovu wowote ule uwe mbali nami;

sitahusika kabisa na uovu.

5Anayemsengenya jirani nitamfutilia mbali;

sitamvumilia mwenye majivuno na kiburi.

6Nitawaangalia kwa wema watu walio waaminifu,

wapate kuishi pamoja nami.

Watu wanyofu ndio watakaonitumikia.

7Mwongo yeyote hatakaa nyumbani mwangu;

hakuna msema uongo atakayekaa kwangu.

8Siku kwa siku nitawaangamiza waovu wote nchini;

nitawaangamiza wabaya wote mjini mwa Mwenyezi-Mungu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania