The chat will start when you send the first message.
1Mimi Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo naandika. Mimi nimechaguliwa kuijenga imani ya wateule wa Mungu na kuwaongoza waufahamu ukweli wa dini yetu[#1:1-4 Huu utangulizi, kama kawaida ya barua za nyakati hizo (taz Rom 1:1-7 maelezo, na Utangulizi kwa Barua za Agano Jipya), unaongezea hapa taarifa fulani kuhusu Mungu na uhai wa milele.]
2ambayo msingi wake ni tumaini la kupata uhai wa milele. Mungu ambaye hasemi uongo, alituahidia uhai huo kabla ya mwanzo wa nyakati,[#1:2 2Tim 2:13 ambapo inasemwa kuwa yeye ni mwaminifu daima. Neno la Kigiriki ambalo linatumika tu hapa katika Tito 1:2 linachukua pia maana ya “wa kuaminika”, na “wa kutegemewa”.]
3na wakati ufaao ulipowadia, akaudhihirisha katika ujumbe wake. Mimi nilikabidhiwa ujumbe huo niutangaze kufuatana na amri ya Mungu, Mwokozi wetu.[#1:3 1Tim 2:6 na pia 6:12; yaani yahusu wakati uliopangwa na Mungu. Huo wakati ni sawa na wakati wa kudhihirisha upendo wake (Rom 5:6-8).; #1:3 Mojawapo ya mafungu ya maneno yanayotumika mara nyingi katika barua hizi zijulikanazo kama za kichungaji (1Tim 1:1; 2:3; Tito 2:10; 3:4).]
4Ninakuandikia wewe Tito, mwanangu wa kweli katika imani tunayoshiriki. Nakutakia neema na amani kutoka kwa Mungu Baba, na kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wetu.[#1:4 Mwenzi na msaidizi wa Paulo katika kuhubiri Injili. Tito alikuwa Mgiriki (2Kor 7:6; 8:6,16-17,23; Gal 2:1,3; 2Tim 4:10). Kuhusu maneno: “mwanangu wa kweli katika imani”, tazama 1Tim 1:2 maelezo.]
5Nilikuacha Krete ili urekebishe yale mambo ambayo hayakuwa yamekamilika bado, na kuwateua wazee wa kanisa katika kila mji. Kumbuka maagizo yangu:[#1:5 Kisiwa katika bahari ya Mediteranea Kusini Mashariki mwa Ugiriki.]
6mzee wa kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na watoto wake wanapaswa kuwa waumini, wasiojulikana kuwa wakorofi au wakaidi.[#1:5-7 Jina la sifa linalomtaja “Kiongozi wa kanisa” (Kigiriki: “presbuteros”). Katika aya ya 7 neno “askofu” (Kigiriki: “episkopos”) linatumika kuhusu wadhifa huohuo wa mwenye madaraka juu ya jumuiya ya waumini au Kanisa (taz 1Tim 3:1 maelezo, na pia Mate 20:28 maelezo).; #1:6 Taz 1Tim 3:2.; #1:6-9 Rejea sifa zinazotakiwa kwa hao viongozi katika 1Tim 3:2-13.]
7Maana kwa vile kiongozi wa kanisa ni mkurugenzi wa kazi ya Mungu, anapaswa kuwa mtu asiye na hatia. Asiwe mwenye majivuno, mwepesi wa hasira, mlevi, mkorofi au mchoyo.
8Anapaswa kuwa mkarimu na anayependa mambo mema. Anapaswa kuwa mtu mtaratibu, mwadilifu, mtakatifu na mwenye nidhamu.[#1:8 Taz 1Tim 3:2 maelezo.]
9Ni lazima ashike kikamilifu ujumbe ule wa kuaminika kama unavyofundishwa. Ndivyo atakavyoweza kuwatia wengine moyo kwa mafundisho sahihi na kuyafichua makosa ya wale wanaoyapinga mafundisho hayo.[#1:9 Maneno yanayotumiwa mara nyingi katika hizi barua zinazojulikana kama za kichungaji; taz 1Tim 1:10 maelezo.]
10Maana, wako watu wengi, hasa wale walioongoka kutoka dini ya Kiyahudi, ambao ni wakaidi, na wanawapotosha wengine kwa upumbavu wao.
11Lazima kukomesha maneno yao, kwani wanavuruga jumuiya nzima kwa kufundisha mambo ambayo hawapaswi kufundisha; wanafanya hivyo kwa nia mbaya ya kupata faida ya fedha.
12Hata mmoja wa manabii wao, ambaye naye pia ni Mkrete, alisema: “Wakrete husema uongo daima; ni kama wanyama wabaya, walafi na wavivu!”[#1:12 Nukuu kutoka kwa mwanamashairi mmoja wa Krete kwa jina Epimenide wa karne ya 6 K.K. Maneno yanayotajwa juu ya tabia ya Wakrete ni yaleyale matatu yaliyotajwa kuhusu waalimu wa uongo katika aya 10 na 11 zilizotangulia.]
13Naye alitoboa ukweli; na kwa sababu hiyo, unapaswa kuwakaripia vikali, ili wawe na imani kamilifu.
14Wasiendelee kushikilia hadithi tupu za Kiyahudi na maagizo ya kibinadamu yanayozuka kwa watu walioukataa ukweli.[#1:14 Taz 1Tim 1:4 maelezo; rejea 1Tim 1:6; 4:7; 2Tim 2:14.; #1:14 1Tim 6:5; 2Tim 3:8; 4:4. “Maagizo ya kibinadamu”: Kwa maelezo ya aya inayofuata, yaani aya ya 15, hayo maagizo ya kibinadamu yamkini yahusu wale ambao walikataza kuoa na kula vyakula fulanifulani (1Tim 4:3-5), vitu ambavyo ni safi kwa sababu vilikuwa vimepangwa na Mungu (Mat 15:11; Marko 7:18-19; Rom 14:14,20).]
15Kila kitu ni safi kwa watu walio safi; lakini hakuna chochote kilicho safi kwa wale waliochafuliwa na wasioamini, maana dhamiri na akili zao zimechafuliwa.[#1:15 Rejea Hag 2:10-14.]
16Watu kama hao hujidai kwamba wanamjua Mungu, lakini kwa matendo yao humkana. Ni watu wa kuchukiza mno na wakaidi, hawafai kwa jambo lolote jema.[#1:16 2Tim 3:5; rejea Mat 7:21; 1Yoh 1:6; 2:4.]