The chat will start when you send the first message.
1Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama kunao wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno,
2kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu.
3Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi.
4Badala yake, kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa moyoni, yaani uzuri usioharibika wa roho ya upole na utulivu, ambayo ni ya thamani sana machoni pa Mungu.
5Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao,
6kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, hata akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara mkitenda yaliyo mema, bila kuogopa jambo lolote.
7Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa kuwajali, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu, na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha neema cha uzima, ili kusiwepo na chochote cha kuzuia maombi yenu.
8Hatimaye, ninyi nyote kuweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, mkijaliana, na wanyenyekevu.
9Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka.
10Kwa maana,
“Yeyote apendaye uzima
na kuona siku njema,
basi auzuie ulimi wake usinene mabaya,
na midomo yake isiseme hila.
11Mtu huyo lazima aache uovu, akatende mema;
lazima aitafute amani na kuifuatilia sana.
12Kwa maana macho ya Bwana
huwaelekea wenye haki,
na masikio yake yako makini
kusikiliza maombi yao.
Bali uso wa Bwana uko kinyume
na watendao maovu.”
13Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye juhudi katika kutenda mema?
14Lakini hata ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki, mmebarikiwa. “Msiogope vitisho vyao, wala msiwe na wasiwasi.”[#3:14 Isa 8:12]
15Bali mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu yeyote atakayewauliza kuhusu sababu ya tumaini lililo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima,
16mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo waaibike kwa ajili ya masingizio yao.
17Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema, ikiwa ni mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu.
18Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili ya wasio haki, ili awalete ninyi kwa Mungu. Mwili wake ukauawa, lakini akafanywa hai katika Roho.
19Baada ya kufanywa hai, alienda na kuzihubiria roho zilizokuwa kifungoni:
20roho ambazo zamani hazikutii, wakati ule uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja katika siku za Nuhu, wakati wa kujenga safina, ambamo watu wachache tu, yaani watu wanane, waliokolewa ili wasiangamie kwa gharika.
21Nayo maji hayo ni kielelezo cha ubatizo ambao sasa unawaokoa ninyi pia: si kwa kuondoa uchafu kwenye mwili, bali kama ahadi ya dhamiri safi kwa Mungu. Inatuokoa kupitia kwa ufufuo wa Yesu Kristo.
22Yeye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu; nao malaika, mamlaka na nguvu zote zimetiishwa chini yake.