1 Samweli 1

1 Samweli 1

Kuzaliwa kwa Samweli

1Kulikuwa na mtu mmoja kutoka Rama, Msufi kutoka nchi ya vilima ya Efraimu, aliyeitwa Elkana mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu Mwefraimu.

2Alikuwa na wake wawili; mmoja aliitwa Hana na mwingine Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na mtoto.

3Kila mwaka mtu huyu alikwea kutoka mji wake ili kuabudu na kutoa dhabihu kwa Bwana wa majeshi huko Shilo, ambapo Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwa makuhani wa Bwana .

4Kila mara ilipofika siku ya Elkana kutoa dhabihu, aliwapa mafungu Penina mkewe na wanawe wote wa kiume na wa kike.

5Lakini alimpa Hana fungu maradufu kwa sababu alimpenda, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo.

6Kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo, mke mwenzake alikuwa anamchokoza ili kumuudhi.

7Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipoenda katika nyumba ya Bwana , mke mwenzake alikuwa akimkasirisha hadi analia na kushindwa kula.

8Elkana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?”

9Siku moja walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alisimama. Wakati huo kuhani Eli alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni mwa mwimo wa mlango wa Hekalu la Bwana .

10Kwa uchungu wake mwingi Hana alimwomba Bwana , akilia kwa uchungu.

11Naye akaweka nadhiri, akisema, “Ee Bwana wa majeshi, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwa Bwana kwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.”

12Alipokuwa anaendelea kumwomba Bwana , Eli alichunguza kinywa chake.

13Hana alikuwa akiomba moyoni mwake, midomo yake ikiwa inachezacheza lakini sauti haikusikika. Eli akafikiri alikuwa amelewa

14naye akamwambia, “Utaendelea kulewa hadi lini? Achilia mbali mvinyo wako.”

15Hana akajibu, “Si hivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye huzuni kubwa. Mimi sijanywa mvinyo wala kileo, nilikuwa ninaumimina moyo wangu kwa Bwana .

16Usimdhanie mtumishi wako kuwa mwanamke mwovu; nimekuwa nikiomba hapa kutokana na uchungu mkuu na huzuni.”

17Eli akamjibu, “Nenda kwa amani, naye Mungu wa Israeli na akujalie kile ulichomwomba.”

18Hana akasema, “Mtumishi wako na apate kibali machoni pako.” Kisha akaondoka zake na kula chakula, wala uso wake haukuwa na huzuni tena.

19Kesho yake asubuhi na mapema waliamka wakaabudu mbele za Bwana na kisha wakarudi nyumbani mwao huko Rama. Elkana akakutana kimwili na mkewe Hana, naye Bwana akamkumbuka.

20Hivyo wakati ulipotimia, Hana akapata mimba na akamzaa mwana. Hana akamwita jina Samweli, akisema, “Kwa kuwa nilimwomba kwa Bwana .”

Hana amweka Samweli wakfu

21Huyo mtu Elkana alipopanda pamoja na jamaa yake yote kutoa dhabihu ya mwaka kwa Bwana na kutimiza nadhiri yake,

22Hana hakuenda. Alimwambia mume wake, “Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, nitamchukua na kumpeleka mbele za Bwana , naye ataishi huko daima.”

23Elkana mumewe akamwambia, “Fanya lile unaloona ni bora zaidi kwako. Ukae hapa hadi utakapomwachisha kunyonya, Bwana na akujalie kutimiza nadhiri yako.” Hivyo huyo mwanamke akakaa nyumbani na kumnyonyesha mwanawe hadi alipomwachisha kunyonya.

24Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, Hana akamchukua huyo mtoto, akiwa mdogo hivyo hivyo, pamoja na fahali wa miaka mitatu, efa ya unga na kiriba cha divai, naye akamleta mtoto kwenye nyumba ya Bwana huko Shilo.[#1:24 Efa moja ya unga ni sawa na kilo 22.]

25Walipokwisha kumchinja yule fahali, wakamleta mtoto kwa Eli,

26naye Hana akamwambia Eli, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu, mimi ndiye yule mama ambaye alisimama hapa karibu nawe akiomba kwa Bwana .

27Niliomba mtoto huyu, naye Bwana amenijalia kile nilichomwomba.

28Hivyo sasa ninamtoa kwa Bwana . Kwa maana maisha yake yote atakuwa ametolewa kwa Bwana .” Naye akamwabudu Bwana huko.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.