1 Samweli 16

1 Samweli 16

Samweli ampaka Daudi mafuta

1Bwana akamwambia Samweli, “Utamlilia Sauli hadi lini, maadamu nimemkataa asiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli? Jaza pembe yako mafuta, ushike njia uende; ninakutuma kwa Yese huko Bethlehemu. Nimemchagua mmoja wa wanawe kuwa mfalme.”

2Lakini Samweli akasema, “Nitaendaje? Sauli atasikia kuhusu jambo hili na ataniua.”

Bwana akamwambia, “Chukua ndama jike, useme, ‘Nimekuja kumtolea Bwana dhabihu.’

3Mwalike Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonesha utakalofanya. Utanipakia mafuta yule nitakuonesha.”

4Samweli akafanya kile Bwana alichosema. Alipofika Bethlehemu, wazee wa mji wakatetemeka walipomlaki. Wakauliza, “Je, umekuja kwa amani?”

5Samweli akajibu, “Ndiyo, kwa amani; nimekuja kumtolea Bwana dhabihu. Jiwekeni wakfu na mje kwenye dhabihu pamoja nami.” Ndipo akamweka Yese wakfu pamoja na wanawe na kuwaalika kwenye dhabihu.

6Walipofika, Samweli akamwona Eliabu, naye akafikiri, “Hakika mpakwa mafuta wa Bwana anasimama hapa mbele za Bwana .”

7Lakini Bwana akamwambia Samweli, “Usitazame sura yake wala kimo chake, kwa kuwa nimemkataa. Bwana hatazami katika vile vitu mwanadamu avitazamavyo. Mwanadamu hutazama katika sura ya nje, lakini Bwana hutazama moyoni.”

8Kisha Yese akamwita Abinadabu na kumpitisha mbele ya Samweli. Lakini Samweli akasema, “Hata huyu Bwana hakumchagua.”

9Kisha Yese akampitisha Shama, lakini Samweli akasema, “Wala huyu Bwana hakumchagua.”

10Yese alikuwa na wana saba aliowapitisha mbele ya Samweli, lakini Samweli akamwambia, “Bwana hajawachagua hawa.”

11Hivyo akamuuliza Yese, “Je, hawa ndio wana pekee ulio nao?”

Yese akajibu, “Bado yuko mdogo kuliko wote, lakini anachunga kondoo.”

Samweli akasema, “Tuma aitwe; hatutaketi hadi afike.”

12Basi akatuma aitwe, naye akaletwa. Alingʼaa kwa afya, na mwenye sura nzuri na umbo la kupendeza.

Ndipo Bwana akasema, “Inuka na umpake mafuta; huyu ndiye.”

13Basi Samweli akachukua ile pembe ya mafuta na kumpaka mafuta mbele ya ndugu zake. Kuanzia siku ile na kuendelea Roho wa Bwana akaja juu ya Daudi kwa nguvu. Kisha Samweli akaenda zake Rama.

Daudi katika utumishi kwa Sauli

14Basi Roho wa Bwana alikuwa ameondoka kwa Sauli, nayo roho mbaya ikaachiwa nafasi na Bwana ili imtese.

15Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Tazama, roho mbaya imeachiwa nafasi na Bwana nayo inakutesa.

16Basi bwana wetu na aamuru watumishi wake walio hapa watafute mtu anayeweza kupiga kinubi. Atakipiga kinubi wakati roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikujiapo, nawe utajisikia vizuri.”

17Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Mtafuteni mtu apigaye kinubi vizuri mkamlete kwangu.”

18Mmoja wa watumishi wake akajibu, “Nimemwona mwana wa Yese Mbethlehemu ambaye anajua kupiga kinubi. Yeye ni mtu hodari na shujaa. Ni mwenye busara katika kunena, mtu mzuri wa umbo. Bwana yu pamoja naye.”

19Ndipo Sauli akatuma wajumbe kwa Yese na kumwambia, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.”

20Kwa hiyo Yese akamchukua punda aliyepakizwa mikate, kiriba cha divai na mwana-mbuzi, na kuvipeleka vitu hivyo kwa Sauli pamoja na Daudi mwanawe.

21Daudi akafika kwa Sauli na kuingia kwenye kazi yake. Sauli akampenda sana, naye Daudi akawa mmoja wa wabeba silaha wake.

22Basi Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akisema, “Mruhusu Daudi abaki katika utumishi wangu, kwa kuwa ninapendezwa naye.”

23Kila mara roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ilipomjia Sauli, Daudi alichukua kinubi chake na kupiga. Ndipo Sauli angetulizwa na kujisikia vizuri, nayo ile roho mbaya ingemwacha.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.