The chat will start when you send the first message.
1Baada ya Daudi kumaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi, naye akampenda kama nafsi yake mwenyewe.
2Kuanzia siku ile Sauli akamchukua Daudi naye hakumruhusu kurudi nyumbani mwa baba yake.
3Yonathani akafanya agano na Daudi kwa sababu alimpenda kama nafsi yake mwenyewe.
4Yonathani akavua joho alilokuwa amevaa na kumpa Daudi, pamoja na koti lake, silaha zake, hata pamoja na upanga wake, upinde wake na mshipi wake.
5Lolote Sauli alilomtuma Daudi kufanya, alifanikiwa sana, hata Sauli akampa cheo cha juu katika jeshi. Jambo hili likawapendeza watu wote, hata maafisa wa Sauli pia.
6Watu walipokuwa wanarudi nyumbani baada ya Daudi kumuua yule Mfilisti, wanawake wakaja kutoka pande zote za miji ya Israeli kumlaki Mfalme Sauli kwa kuimba na kucheza, kwa nyimbo za furaha na kwa matari na zeze.
7Walipokuwa wanacheza, wakaimba:
“Sauli amewaua elfu zake,
naye Daudi makumi elfu yake.”
8Sauli akakasirika sana; sehemu hii ya kurudia rudia ya wimbo huu ilimkasirisha sana. Akafikiri kuwa, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa elfu tu. Apate nini zaidi isipokuwa ufalme?”
9Kuanzia wakati ule na kuendelea Sauli akawa na jicho la wivu juu ya Daudi.
10Kesho yake roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikaja kwa nguvu juu ya Sauli. Alikuwa akitabiri nyumbani mwake, wakati Daudi alikuwa akipiga kinubi, kama alivyozoea. Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake;
11akautupa kwa nguvu, akijiambia mwenyewe, “Nitamchoma kwa mkuki abaki hapo ukutani.” Lakini Daudi akamkwepa mara mbili.
12Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja na Daudi, lakini alikuwa amemwacha yeye.
13Kwa hiyo Sauli akamwondoa Daudi mbele yake na kumpa kuwa kiongozi wa watu elfu moja, naye Daudi akatoka na kuingia akiongoza vikosi katika vita.
14Katika kila kitu alichofanya, Daudi alipata mafanikio makubwa, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye.
15Sauli alipoona jinsi alivyokuwa akifanikiwa, akamwogopa.
16Lakini Israeli wote na Yuda walimpenda Daudi, kwa sababu ndiye alikuwa akiwaongoza katika vita vyao.
17Sauli akamwambia Daudi, “Huyu hapa binti yangu mkubwa Merabu. Nitakupa umwoe, endapo tu utanitumikia kwa ushujaa na kupigana vita vya Bwana .” Kwa maana Sauli alisema moyoni mwake, “Sitainua mkono wangu dhidi yake. Acha mkono wa Wafilisti uwe juu yake.”
18Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mimi ni nani, nayo jamaa yangu ni nini au ukoo wa baba yangu katika Israeli, kwamba mimi niwe mkwewe mfalme?”
19Basi ulipofika wakati wa Daudi kupewa Merabu, binti Sauli, huyo binti aliozwa kwa Adrieli, Mmeholathi.
20Basi Mikali binti Sauli alimpenda Daudi, nao walipomwambia Sauli kuhusu jambo hili, likampendeza.
21Sauli akawaza, “Nitampa Daudi binti yangu, ili apate kuwa mtego kwake, ili mkono wa Wafilisti upate kuwa juu yake.” Hivyo Sauli akamwambia Daudi, “Sasa unayo nafasi ya pili ya kuwa mkwe wangu.”
22Ndipo Sauli akawaagiza watumishi wake, akisema, “Zungumzeni na Daudi kwa siri na kumwambia, ‘Tazama, mfalme amependezwa nawe, nao watumishi wake wote wanakupenda. Basi na uwe mkwewe mfalme.’ ”
23Watumishi wa Sauli wakarudia hayo maneno kwa Daudi. Lakini Daudi akasema, “Je, mnafikiri ni jambo dogo kuwa mkwewe mfalme? Mimi ni mtu maskini tu, na nisiyejulikana sana.”
24Watumishi wa Sauli walipomweleza vile Daudi alivyosema,
25Sauli akajibu, “Mwambieni Daudi, ‘Mfalme hataki zawadi nyingine kuwa mahari, isipokuwa magovi mia moja ya Wafilisti, ili kulipiza kisasi juu ya adui zake.’ ” Mawazo ya Sauli yalikuwa Daudi akaanguke mikononi mwa Wafilisti.
26Watumishi walipomwambia Daudi mambo haya, ikampendeza kuwa mkwewe mfalme. Basi kabla siku iliyopangwa haijafika,
27Daudi na watu wake walitoka na kuwaua Wafilisti mia mbili. Akayaleta magovi yao na kupeleka hesabu kamilifu kwa mfalme, ili apate kuwa mkwewe mfalme. Ndipo Sauli akamwoza Daudi Mikali binti yake.
28Sauli alipotambua kuwa Bwana alikuwa pamoja na Daudi na kwamba Mikali binti yake anampenda Daudi,
29Sauli akazidi kumwogopa Daudi, naye Sauli akabaki kuwa adui yake siku zote za maisha yake.
30Majemadari wa jeshi la Wafilisti waliendelea kupigana vita na kadiri walivyoendelea kupigana, Daudi akazidi kutenda kwa hekima kuliko maafisa wengine wa Sauli, nalo jina lake likajulikana sana.