The chat will start when you send the first message.
1Ndugu, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanyika kwetu pamoja mbele zake, tunawasihi,
2msiyumbishwe kwa urahisi wala msitiwe wasiwasi na roho, wala neno la unabii, au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu, kusema kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwepo.
3Mtu yeyote asiwadanganye kwa namna yoyote kwa maana siku ile haitakuja hadi uasi utokee kwanza, na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa.
4Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.
5Je, hamkumbuki kwamba nilipokuwa pamoja nanyi niliwaambia mambo haya?
6Nanyi sasa mnajua kinachomzuia, ili apate kudhihirishwa wakati wake utakapowadia.
7Maana ile nguvu ya siri ya uasi tayari inatenda kazi, lakini yule anayeizuia ataendelea kufanya hivyo hadi atakapoondolewa.
8Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Yesu atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake.
9Kuja kwa yule mwasi kutalingana na vile Shetani hufanya kazi. Atatumia nguvu za aina mbalimbali katika miujiza, na ishara na ajabu za uongo,
10na katika njia zote ambazo uovu hudanganya wanaoangamia. Wanaangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli ili wapate kuokolewa.
11Kwa sababu hii, Mungu anawatumia nguvu ya udanganyifu, ili waamini uongo,
12na hivyo wahukumiwe wote ambao hawakuiamini ile kweli, bali wamefurahia uovu.
13Lakini inatupasa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana, kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe kwa kutakaswa na Roho kwa kuiamini kweli.
14Kwa kusudi hili Mungu aliwaita ninyi kupitia Injili tuliyowahubiria, ili mpate kushiriki katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.
15Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua.
16Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu, aliyetupenda na kwa neema yake akatupatia faraja ya milele na tumaini jema,
17awafariji mioyo yenu na kuwaimarisha katika kila neno na tendo jema.