Matendo 9

Matendo 9

Kuokoka kwa Sauli

(Mdo 22:6‑16; 26:12‑18)

1Wakati ule ule, Sauli alikuwa bado anazidisha vitisho vya kuua wanafunzi wa Bwana, akamwendea kuhani mkuu,

2naye akamwomba kuhani mkuu ampe barua za kwenda kwenye masinagogi huko Dameski, ili akimkuta mfuasi yeyote wa Njia Ile, akiwa mwanaume au mwanamke, aweze kuwafunga na kuwaleta Yerusalemu.[#9:2 maana yake wafuasi wa Yesu (Yn 14:6; Mdo 24:14); walichukuliwa kuwa dhehebu la dini ya Wayahudi.]

3Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza pande zote.

4Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?”

5Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?”

Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu unayemtesa.

6Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa unachopaswa kufanya.”

7Watu waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza.

8Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu chochote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza hadi Dameski.

9Kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu; naye hakula wala kunywa chochote.

10Huko Dameski kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana alimwita katika maono, “Anania!”

Akajibu, “Mimi hapa Bwana.”

11Bwana akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba,

12katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”

13Anania akajibu, “Bwana, nimesikia kutoka kwa watu wengi habari nyingi kuhusu mtu huyu na madhara yote aliyowatendea watakatifu wako huko Yerusalemu.

14Naye amekuja hapa Dameski akiwa na mamlaka kutoka kwa viongozi wa makuhani ili awakamate wote wanaotaja jina lako.”

15Lakini Bwana akamwambia Anania, “Nenda! Mtu huyu ni chombo nilichochagua kutangaza jina langu kwa watu wa Mataifa na wafalme wao na watu wa Israeli.

16Nami nitamwonesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya Jina langu.”

17Kisha Anania akaenda kwenye ile nyumba, akaingia ndani. Akaweka mikono yake juu ya Sauli akasema, “Ndugu Sauli, Bwana Yesu aliyekutokea njiani amenituma kwako ili upate kuona tena na ujazwe Roho Mtakatifu.”

18Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa.

19Baada ya kula chakula, akapata nguvu tena. Sauli akakaa siku kadhaa pamoja na wanafunzi huko Dameski.

Sauli ahubiri Dameski

20Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.

21Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu huko Yerusalemu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wafungwa mbele ya viongozi wa makuhani?”

22Sauli akazidi kuwa hodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Yesu ndiye Kristo.[#9:22 maana yake Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.]

23Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi wakapanga njama kumuua Sauli.

24Lakini Sauli akagundua njama yao. Wayahudi wakawa wanalinda malango yote ya mji, usiku na mchana ili wapate kumuua.

25Lakini wafuasi wake wakamchukua usiku wakamshusha akiwa ndani ya kapu kupitia mahali penye nafasi ukutani.

Sauli huko Yerusalemu

26Sauli alipofika Yerusalemu akajaribu kujiunga na wanafunzi lakini wote walimwogopa, kwa maana hawakuamini kwamba kweli naye alikuwa mwanafunzi.

27Lakini Barnaba akamchukua, akampeleka kwa wale mitume. Akawaeleza jinsi Sauli akiwa njiani alivyomwona Bwana, jinsi Bwana alivyosema naye na jinsi alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Yesu huko Dameski.

28Kwa hiyo Sauli akakaa nao akitembea kwa uhuru kila mahali huko Yerusalemu, akihubiri kwa ujasiri katika jina la Bwana.

29Alinena na kuhojiana na Wayahudi wenye asili ya Kiyunani, lakini wao walijaribu kumuua.

30Wale ndugu walipopata habari wakampeleka hadi Kaisaria, wakamsafirisha kwenda Tarso.

31Ndipo kanisa katika Yudea yote, Galilaya na Samaria likawa na wakati wa amani. Likatiwa nguvu; na kwa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu, idadi yake ikaongezeka, na likaendelea kudumu katika kumcha Bwana.

Matendo ya Petro

Kuponywa kwa Ainea

32Petro alipokuwa akisafiri sehemu mbalimbali, alienda kuwatembelea watakatifu walioishi huko Lida.

33Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea, aliyekuwa amepooza na kwa muda wa miaka nane alikuwa hajatoka kitandani.

34Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya, inuka utandike kitanda chako.” Mara Ainea akainuka.

35Watu wote wa Lida na Sharoni walipomwona Ainea akitembea wakamgeukia Bwana.

Petro amfufua Dorkasi

36Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini.[#9:36 kwa Kiaramu na Dorkasi kwa Kiyunani yote yamaanisha Paa.]

37Wakati huo akaugua, akafa, na wakauosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani.

38Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.”

39Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao. Alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao.

40Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi.

41Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai.

42Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana.

43Petro akakaa Yafa kwa siku nyingi akiishi na Simoni mtengenezaji ngozi.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.