Kutoka 12

Kutoka 12

Pasaka na pigo la mwisho

1Bwana akamwambia Musa na Haruni katika nchi ya Misri,

2“Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu, yaani mwezi wa kwanza wa mwaka wenu.

3Iambie jumuiya yote ya Israeli kwamba katika siku ya kumi ya mwezi huu, kila mtu atatwaa mwana-kondoo mmoja kwa ajili ya jamaa yake, mmoja kwa kila nyumba.

4Ikiwa nyumba yoyote ina watu wachache wasioweza kumaliza huyo mwana-kondoo mzima, nyumba hiyo itabidi ishirikiane na nyumba ya jirani wa karibu, baada ya kuzingatia idadi ya watu waliomo. Mtaangalia ni kiasi gani cha nyama kitahitajika kulingana na mahitaji ya kila mtu.

5Wanyama mtakaowachagua, lazima wawe wa kiume wa umri wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari, mwaweza kuwachukua kati ya kondoo au mbuzi.

6Tunzeni wanyama hao hadi siku ya kumi na nne ya mwezi, ambapo lazima watu wa jumuiya yote ya Israeli wachinje wanyama hao wakati wa jioni.

7Ndipo watakapochukua sehemu ya hiyo damu na kuipaka kwenye vizingiti vya juu, na miimo ya milango ya nyumba ambamo watakula wana-kondoo hao.

8Usiku huo huo watakula nyama iliyookwa kwenye moto, pamoja na mboga chungu za majani na mikate isiyotiwa chachu.

9Msile nyama mbichi wala iliyochemshwa, lakini iwe imeokwa kwenye moto, kichwa, miguu na nyama zake za ndani.

10Msibakize nyama yoyote hadi asubuhi; nazo kama zitabakia hadi asubuhi, lazima mziteketeze kwa moto.

11Hivi ndivyo mtakavyokula: Mtajifunga mikanda viunoni, mtakuwa mmevaa viatu vyenu miguuni na kushika fimbo zenu mkononi mwenu. Mle kwa haraka; hii ni Pasaka ya Bwana .

12“Usiku huo huo nitapita katika nchi yote ya Misri na kumuua kila mzaliwa wa kwanza, wa wanadamu na wa wanyama, nami nitaihukumu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Bwana .

13Damu itakuwa ishara kwa ajili yenu ya kuonesha nyumba ambazo mtakuwamo; nami nitakapoiona damu, nitapita juu yenu. Hakuna pigo la uharibifu litakalowagusa ninyi nitakapoipiga Misri.

14“Siku hii itakuwa kumbukumbu kwenu, mtaiadhimisha kuwa sikukuu kwa Bwana , katika vizazi vyenu vyote: mtalishika kuwa agizo la kudumu.

15Kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza mtaondoa chachu yote ndani ya nyumba zenu, kwa maana yeyote atakayekula chochote chenye chachu kuanzia siku ya kwanza hadi ya saba lazima akatiliwe mbali kutoka Israeli.

16Katika siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu, na kusanyiko jingine katika siku ya saba. Katika siku hizo msifanye kazi kamwe isipokuwa kutayarisha chakula cha kila mmoja; hilo ndilo tu mtakalofanya.

17“Mtaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, kwa sababu hiyo ndiyo siku ile niliyovitoa vikosi vyenu kutoka Misri. Mtaiadhimisha siku hii kwa vizazi vyenu vyote kuwa agizo la kudumu.

18Katika mwezi wa kwanza mtakula mikate isiyotiwa chachu, kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne hadi jioni ya siku ya ishirini na moja.

19Kwa muda wa siku saba isionekane chachu yoyote katika nyumba zenu. Yeyote alaye chochote chenye chachu ndani yake, lazima akatiliwe mbali kutoka jumuiya ya Israeli, akiwa ni mgeni au mzawa.

20Msile chochote kilichotiwa chachu. Popote mnapoishi, ni lazima mle mikate isiyotiwa chachu.”

21Ndipo Musa akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka.

22Chukueni kitawi cha hisopo, mkichovye kwenye damu iliyopo kwenye sinia, na kuipaka sehemu ya hiyo damu kwenye vizingiti, na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu yeyote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake hadi asubuhi.

23Bwana apitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi.

24“Shikeni maagizo haya yawe kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu.

25Mtakapoingia katika nchi Bwana atakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii.

26Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’

27Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa Bwana , ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri, na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo Waisraeli walisujudu na kuabudu.

28Waisraeli wakafanya kama vile Bwana alivyomwagiza Musa na Haruni.

29Ilipofika usiku wa manane, Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika Misri, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa, aliyekuwa gerezani, na wazaliwa wa kwanza wa mifugo yote pia.

30Farao, na maafisa wake wote, na Wamisri wote wakaamka usiku, na kulikuwa na kilio kikubwa katika nchi ya Misri, kwa kuwa hapakuwa nyumba hata moja ambayo hakufa mtu.

Kutoka

31Wakati huo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, “Ondokeni! Tokeni kwa watu wangu, ninyi pamoja na Waisraeli! Nendeni mkamwabudu Bwana kama mlivyoomba.

32Chukueni makundi yenu ya kondoo na mbuzi pamoja na ngʼombe, kama mlivyosema, nanyi mwende zenu. Nanyi pia mnibariki.”

33Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke kwa haraka na kuacha nchi yao. Kwa kuwa walisema, “La sivyo, tutakufa wote!”

34Hivyo watu wakachukua donge lao la unga kabla ya kutiwa chachu, wakaweka ndani ya mabakuli ya kukandia, wakayaviringisha katika mavazi na kuyabeba mabegani mwao.

35Waisraeli wakafanya kama Musa alivyowaelekeza, nao wakawaomba Wamisri wawapatie vitu vya fedha, dhahabu na mavazi.

36Basi Bwana alikuwa amewafanya Wamisri kuwa wakarimu kwa hawa watu, wakawapatia Waisraeli vile walivyotaka kwao; kwa hiyo wakawateka nyara Wamisri.

37Waisraeli wakasafiri kutoka Ramesesi hadi Sukothi. Walikuwa wanaume wapatao elfu mia sita waliotembea kwa miguu, bila kuhesabu wanawake na watoto.

38Watu wengine wengi wakafuatana nao, pamoja na makundi makubwa ya mifugo, wakiwemo kondoo, mbuzi na ngʼombe.

39Wakatengeneza maandazi yasiyotiwa chachu kwa ule unga uliokandwa waliokuwa wameutoa Misri, donge hilo la unga halikuwa limetiwa chachu, kwa kuwa walikuwa wameondolewa Misri kwa haraka nao hawakuwa na muda wa kujiandalia chakula.

40Waisraeli waliishi Misri kwa muda wa miaka mia nne na thelathini (430).

41Siku ya mwisho ya hiyo miaka mia nne na thelathini (430), vikosi vyote vya Bwana viliondoka Misri.

42Kwa sababu Bwana aliutenga usiku ule ili kuwatoa Waisraeli katika nchi ya Misri, basi Waisraeli wote wanapaswa kuadhimisha usiku huu kwa kukesha ili kumheshimu Bwana katika vizazi vijavyo.

Masharti kwa ajili ya Pasaka

43Bwana akawaambia Musa na Haruni, “Haya ndio masharti kwa ajili ya Pasaka:

“Mgeni hataruhusiwa kula Pasaka.

44Mtumwa yeyote ambaye mmemnunua aweza kuila kama mmemtahiri,

45lakini kibarua yeyote au msafiri haruhusiwi kula.

46“Sharti iliwe ndani ya nyumba; msichukue nyama yoyote nje ya nyumba hiyo. Msiuvunje mfupa wowote.

47Jumuiya yote ya Israeli ni lazima waiadhimishe Pasaka hiyo.

48“Mgeni aishiye miongoni mwenu ambaye anataka kuadhimisha Pasaka ya Bwana ni lazima wanaume wote waliomo nyumbani mwake wawe wametahiriwa, ndipo aweze kushiriki kama mzawa. Mwanaume yeyote asiyetahiriwa haruhusiwi kuila.

49Sheria hiyo hiyo itamuhusu mzawa na mgeni anayeishi miongoni mwenu.”

50Waisraeli wote walifanya kama vile Bwana alivyomwagiza Musa na Haruni.

51Siku ile ile Bwana akawatoa Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.