Ezekieli 11

Ezekieli 11

Hukumu kwa viongozi wa Israeli

1Ndipo Roho akaniinua na kunileta hadi kwenye lango la nyumba ya Bwana linalotazama upande wa mashariki. Pale kwenye ingilio la lango palikuwa na wanaume ishirini na watano. Nami nikaona miongoni mwao Yaazania mwana wa Azuri na Pelatia mwana wa Benaya, viongozi wa watu.

2Bwana akaniambia, “Mwanadamu, hawa ndio wafanyao hila na kutoa mashauri potovu katika mji huu.

3Wao husema, ‘Je, hivi karibuni hautakuwa wakati wa kujenga nyumba? Mji huu ni chungu cha kupikia, nasi ndio nyama.’

4Kwa hiyo tabiri dhidi yao; tabiri, ewe mwanadamu.”

5Kisha Roho wa Bwana akaja juu yangu, naye akaniambia niseme: “Hili ndilo asemalo Bwana : Hili ndilo ninyi mnalosema, ee nyumba ya Israeli, lakini ninajua mnalowaza mioyoni mwenu.

6Mmewaua watu wengi katika mji huu na kujaza barabara zake maiti.

7“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: Maiti mlizozitupa huko ndizo nyama, na mji huu ndio chungu, lakini nitawaondoa mtoke huko.

8Mnaogopa upanga, nao upanga huo ndio nitakaouleta dhidi yenu, asema Bwana Mwenyezi.

9Nitawaondoa mtoke katika mji na kuwatia mikononi mwa wageni nami nitawaadhibu.

10Mtaanguka kwa upanga, nami nitatimiza hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana .

11Mji huu hautakuwa chungu kwa ajili yenu, wala hamtakuwa nyama ndani yake. Nitatoa hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli.

12Nanyi mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana , kwa kuwa hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu, bali mmefuata mwenendo wa mataifa yanayowazunguka.”

13Basi nilipokuwa nikitoa unabii, Pelatia mwana wa Benaya akafa. Ndipo nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kuu, nikasema, “Ee Bwana Mwenyezi! Je, utaangamiza kabisa mabaki ya Israeli?”

Ahadi ya Wayahudi kurejeshwa

14Neno la Bwana likanijia, kusema:

15“Mwanadamu, ndugu zako, ndugu zako ambao ni wa uhusiano wa damu nawe pamoja na nyumba yote ya Israeli, ndio wale ambao watu wa Yerusalemu wamesema kuwahusu, ‘Wako mbali na Bwana ; nchi hii tulipewa sisi kuwa milki yetu.’

16“Kwa hiyo sema, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: Ingawa niliwapeleka mbali miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali, hata hivyo, kwa kitambo kidogo, nimekuwa mahali patakatifu kwao katika nchi walizoenda.’

17“Kwa hiyo sema: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: Nitawakusanya kutoka mataifa na kuwarudisha kutoka nchi ambazo mmetawanywa, nami nitawarudishia nchi ya Israeli.’

18“Watairudia nchi na kuondoa vinyago vyote vya upotovu na sanamu zote za kuchukiza.

19Nitawapa moyo usiogawanyika na kuweka roho mpya ndani yao; nitaondoa ndani yao moyo wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama.

20Kisha watafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii sheria zangu. Watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao.

21Lakini kwa wale ambao mioyo yao imeambatana na vinyago vyao vya upotovu na sanamu zao za kuchukiza, nitawalipa kikamilifu kulingana na matendo yao,” asema Bwana Mwenyezi.

22Ndipo wale makerubi, wenye magurudumu pembeni mwao, wakakunjua mabawa yao, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.

23Basi utukufu wa Bwana ukapaa juu kwanzia katika mji na kutua juu ya mlima ulio mashariki mwa mji.

24Roho akaniinua na kunileta kwa watu wa uhamisho huko Ukaldayo nikiwa katika yale maono niliyopewa na Roho wa Mungu.

Ndipo maono niliyokuwa nimeyaona yakanitoka,

25nami nikawaeleza wale watu wa uhamisho kila kitu Bwana alichokuwa amenionesha.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.