The chat will start when you send the first message.
1Wakati huu Abrahamu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, naye Bwana alikuwa amembariki katika mambo yote.
2Abrahamu akamwambia mtumishi wake mkuu katika nyumba yake, aliyekuwa msimamizi wa mali yake yote, “Weka mkono wako chini ya paja langu.
3Ninataka uape kwa Bwana , Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke kutoka binti za Wakanaani, ambao ninaishi miongoni mwao.
4Bali nenda katika nchi yangu na jamaa zangu umpatie Isaka mwanangu mke.”
5Yule mtumishi akamuuliza, “Je, itakuwaje huyo mwanamke akikataa kuja nami katika nchi hii? Je, nimrudishe mwanao katika hiyo nchi uliyotoka?”
6Abrahamu akasema, “Hakikisha kwamba hutamrudisha mwanangu huko.
7Bwana , Mungu wa mbingu, alinitoa nyumbani mwa baba yangu na nchi yangu niliyozaliwa. Ndiye alisema nami na akaniahidi kwa kiapo, akasema, ‘Nitawapa uzao wako nchi hii.’ Yeye atatuma malaika wake akutangulie ili umtwalie mwanangu mke kutoka huko.
8Huyo mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi utafunguliwa kutoka kiapo nilichokuapisha. Ila usimrudishe mwanangu huko.”
9Basi yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la bwana wake Abrahamu, akamwapia kuhusu shauri hili.
10Ndipo huyo mtumishi akachukua ngamia kumi miongoni mwa ngamia wa bwana wake, akaondoka, akiwa amechukua aina zote za vitu vizuri kutoka kwa bwana wake. Akaelekea Mesopotamia, akaenda hadi mji wa Nahori.
11Akawapigisha ngamia magoti karibu na kisima cha maji nje ya mji; ilikuwa inaelekea jioni, wakati wanawake huteka maji.
12Kisha akaomba, “Ee Bwana , Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nipatie ushindi leo, uoneshe ukarimu kwa bwana wangu Abrahamu.
13Tazama, nimesimama karibu na kisima hiki cha maji, nao binti za watu wa mji huu wanakuja kuteka maji.
14Basi na iwe hivi, nitakapomwambia binti mmoja, ‘Tafadhali tua mtungi wako nipate kunywa maji’; naye akisema, ‘Kunywa, nitawanywesha na ngamia wako pia’: basi na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka. Kwa hili nitajua umemtendea bwana wangu ukarimu.”
15Ikawa kabla hajamaliza kuomba, Rebeka akatokea akiwa na mtungi begani mwake. Alikuwa binti Bethueli. Bethueli alikuwa mwana wa Milka, aliyekuwa mke wa Nahori ndugu wa Abrahamu.
16Huyu msichana alikuwa mzuri sana wa sura, bikira, ambaye hakuna mwanaume aliyekuwa amekutana naye kimwili. Aliteremka kisimani, akajaza mtungi wake, tena akapanda juu.
17Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye, akamwambia, “Tafadhali nipe maji kidogo katika mtungi wako.”
18Yule msichana akasema, “Kunywa, bwana wangu.” Akashusha kwa haraka mtungi mkononi mwake na akampa, akanywa.
19Baada ya kumpa yule mtumishi yale maji, akamwambia, “Nitawatekea ngamia wako maji pia hadi wote watosheke.”
20Akafanya haraka kumimina maji kwenye birika ya kunyweshea wanyama, akakimbia kisimani kuteka maji mengine, na akateka ya kuwatosha ngamia wake wote.
21Pasipo kusema neno, yule mtumishi akamtazama kwa makini aone kama Bwana ameifanikisha safari yake, au la.
22Ikawa ngamia walipokwisha kunywa wote, yule mtumishi akampa huyo msichana pete ya puani ya dhahabu yenye uzito wa beka moja, na bangili mbili za dhahabu zenye uzito wa shekeli kumi.[#24:22 Beka moja ya dhahabu ni sawa na gramu 5.5.; #24:22 Shekeli 10 za dhahabu ni sawa na gramu 110.]
23Kisha akamuuliza, “Wewe ni binti ya nani? Tafadhali niambie. Je, kuna nafasi katika nyumba ya baba yako tunapoweza kulala?”
24Yule msichana akamjibu, “Mimi ni binti ya Bethueli, mwana wa Milka aliyemzalia Nahori.”
25Akaendelea kusema, “Kwetu kuna majani mengi na malisho, tena kuna nafasi kwa ajili yenu kulala.”
26Yule mtumishi akasujudu na kumwabudu Bwana ,
27akisema, “Atukuzwe Bwana , Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hakuondoa wema na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mimi nami, Bwana ameniongoza safarini, akanifikisha nyumbani kwa jamaa za bwana wangu.”
28Yule msichana akakimbia, akawaeleza watu wa nyumbani mwa mama yake kuhusu mambo haya.
29Rebeka alikuwa na kaka aliyeitwa Labani; huyo akaharakisha kukutana na yule mtumishi kule kisimani.
30Mara alipoiona ile pete puani, na bangili mikononi mwa dada yake, na kusikia yale maneno Rebeka aliyoambiwa na huyo mtumishi, alimwendea huyo mtumishi, akamkuta amesimama karibu na ngamia wake pale karibu na kisima.
31Akamwambia, “Karibu nyumbani wewe uliyebarikiwa na Bwana . Kwa nini unasimama huko nje? Mimi nimekuandalia nyumba na mahali kwa ajili ya ngamia.”
32Hivyo yule mtumishi akaingia nyumbani, nayo mizigo ikaondolewa juu ya ngamia. Majani na malisho yakaletwa kwa ajili ya ngamia, na maji kwa ajili yake na watu wake ili kunawa miguu.
33Ndipo chakula kikaandaliwa kwa ajili yake, lakini akasema, “Sitakula hadi niwe nimewaambia yale niliyo nayo ya kusema.”
Labani akasema, “Basi tuambie.”
34Hivyo akasema, “Mimi ni mtumishi wa Abrahamu.
35Bwana amembariki sana bwana wangu, amekuwa tajiri. Amempa kondoo na ngʼombe, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda.
36Sara mkewe bwana wangu amemzalia mwana katika uzee wake, naye amempa kila kitu alichokuwa nacho.
37Naye bwana wangu ameniapisha na akasema, ‘Kamwe usimtwalie mwanangu mke katika binti za Wakanaani, ambao ninaishi katika nchi yao,
38ila uende hadi kwa jamaa ya baba yangu na ukoo wangu mwenyewe, ukamtwalie mwanangu mke huko.’
39“Kisha nikamuuliza bwana wangu, ‘Je, kama huyo mwanamke hatakubali kurudi nami?’
40“Akanijibu, ‘Bwana , ambaye nimetembea mbele zake, atatuma malaika wake pamoja nawe, na kuifanikisha safari yako, ili uweze kupata mke kwa ajili ya mwanangu katika ukoo wangu na kutoka jamaa ya baba yangu.
41Kisha, utakapoenda kwenye ukoo wangu, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu. Hata wakikataa kukupa huyo binti, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu.’
42“Nilipokuja kisimani leo nilisema, ‘Ee Bwana , Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ikikupendeza, naomba uifanikishe safari niliyoijia.
43Tazama, ninasimama kando ya kisima hiki. Mwanamwali akija kuteka maji, nami nikimwambia: Tafadhali niruhusu ninywe maji kidogo kutoka mtungi wako.
44Naye akiniambia, “Kunywa, nami nitawatekea ngamia wako maji pia,” basi huyo awe ndiye mke Bwana amemchagulia mwana wa bwana wangu.’
45“Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani, akateka maji, nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ninywe.’
46“Akafanya haraka kushusha mtungi wake begani na kusema, ‘Kunywa, na nitawanywesha ngamia wako pia.’ Basi nikanywa, naye akawanywesha na ngamia pia.
47“Nikamuuliza, ‘Wewe ni binti ya nani?’
“Akasema, ‘Mimi ni binti ya Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia.’
“Ndipo nilipotia pete puani mwake na bangili mikononi mwake,
48nikasujudu na nikamwabudu Bwana . Nikamtukuza Bwana , Mungu wa bwana wangu Abrahamu, aliyeniongoza katika njia sahihi ili nimtwalie mwana na bwana wangu mke katika jamaa zake.
49Ikiwa mtaonesha wema na uaminifu kwa bwana wangu, mniambie; la sivyo, mniambie, ili niweze kujua njia ya kugeukia.”
50Labani na Bethueli wakajibu, “Jambo hili limetoka kwa Bwana ; hatuwezi kukuambia jambo lolote baya au jema.
51Rebeka yuko hapa, mchukue na uende, awe mke wa mwana wa bwana wako, sawasawa na Bwana alivyoongoza.”
52Ikawa huyo mtumishi wa Abrahamu aliposikia waliyosema, alisujudu, uso wake ukagusa chini mbele za Bwana .
53Ndipo huyo mtumishi akatoa vitu vilivyotengenezwa kwa dhahabu na kwa fedha, pamoja na mavazi, akampa Rebeka; pia akawapa zawadi za thamani kubwa nduguye na mamaye.
54Kisha yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye wakala, wakanywa na kulala palepale.
Walipoamka asubuhi, yule mtumishi akasema, “Nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”
55Lakini ndugu yake Rebeka pamoja na mama yake wakajibu, “Acha binti akae kwetu siku kumi au zaidi, ndipo mwondoke.”
56Lakini yule mtumishi akawaambia, “Msinicheleweshe, kwa kuwa Bwana amefanikisha safari yangu. Nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”
57Ndipo wakasema, “Acha tumwite huyo binti tumuulize, tusikie atakavyosema.”
58Kwa hiyo wakamwita Rebeka na kumuuliza, “Je, utaenda na mtu huyu?”
Akasema, “Nitaenda.”
59Hivyo wakamwaga ndugu yao Rebeka aondoke, pamoja na mjakazi wake, na mtumishi wa Abrahamu na watu wake.
60Wakambariki Rebeka, wakamwambia,
“Ndugu yetu, uwe wewe kumi elfu,
mara elfu nyingi;
nao wazao wako wamiliki
malango ya adui zao.”
61Rebeka na vijakazi wake wakajiandaa, wakapanda ngamia wao, wakafuatana na yule mtu. Hivyo yule mtumishi akamchukua Rebeka, wakaondoka.
62Basi Isaka alikuwa ametoka Beer-Lahai-Roi, kwa kuwa alikuwa akiishi nchi ya Negebu.
63Isaka akaenda shambani kutafakari wakati wa jioni; alipoinua macho yake, akaona ngamia wanakuja.
64Rebeka pia akainua macho, akamwona Isaka. Akashuka kutoka ngamia wake,
65akamuuliza yule mtumishi, “Ni nani mtu yule kule shambani anayekuja kutulaki?”
Yule mtumishi akajibu, “Huyu ndiye bwana wangu.” Hivyo Rebeka akachukua shela yake, akajifunika.
66Kisha yule mtumishi akamweleza Isaka mambo yote aliyoyatenda.
67Isaka akamwingiza Rebeka katika hema la Sara mama yake. Isaka akamchukua Rebeka, hivyo akawa mke wake. Isaka akampenda; akafarijika baada ya kifo cha mama yake.