Habakuki 3

Habakuki 3

Maombi ya Habakuki

2Bwana , nimezisikia sifa zako;

nami naogopa kwa matendo yako, Ee Bwana .

Fufua kazi yako katika siku hizi zetu,

tangaza habari yako wakati huu wetu;

katika ghadhabu kumbuka rehema.

3Mungu alitoka Temani,

yeye Aliye Mtakatifu kutoka Mlima Parani.

Utukufu wake ulifunika mbingu,

na sifa zake zikaifunika dunia.

4Mngʼao wake ulikuwa kama jua linapochomoza;

miali ilimulika kutoka mkononi mwake,

ambako nguvu zake zilifichwa.

5Tauni ilimtangulia;

maradhi ya kuambukiza yalifuata nyayo zake.

6Alisimama, akaitikisa dunia;

alitazama, na kuyafanya mataifa yatetemeke.

Milima ya zamani iligeuka mavumbi

na vilima vilivyozeeka vikaanguka.

Njia zake ni za milele.

7Niliona watu wa Kushani katika dhiki,

na makazi ya Midiani katika maumivu makali.

8Ee Bwana , uliikasirikia mito?

Je, ghadhabu yako ilikuwa dhidi ya vijito?

Je, ulighadhibikia bahari

ulipoendesha farasi wako

na magari yako ya vita ili ushinde?

9Uliufunua upinde wako

na kuitisha mishale mingi.

Uliigawa dunia kwa mito;

10milima ilikuona ikatetemeka.

Mafuriko ya maji yakapita huko;

vilindi vilinguruma

na kuinua mawimbi yake juu.

11Jua na mwezi vilisimama kimya mbinguni

katika mngʼao wa mishale yako inayoruka,

na katika mngʼao wa mkuki wako umeremetao.

12Kwa ghadhabu ulipitia kwenye dunia,

na katika hasira ulikanyaga mataifa.

13Ulikuja kuwaokoa watu wako,

kumwokoa uliyempaka mafuta.

Ulimponda kiongozi wa nchi ya uovu,

ukamvua toka kichwani hadi wayo.

14Kwa mkuki wake mwenyewe ulitoboa kichwa chake

wakati mashujaa wake walifurika nje kwa kishindo kututawanya,

wakifurahi kama walio karibu kutafuna

wale wanyonge waliokuwa mafichoni.

15Ulikanyaga bahari kwa farasi wako,

ukisukasuka maji makuu.

16Nilisikia na moyo wangu ukagonga kwa nguvu,

midomo yangu ikatetemeka kwa hofu niliposikia sauti;

uchakavu ukanyemelea mifupa yangu,

na miguu yangu ikatetemeka.

Hata hivyo nitasubiri kwa uvumilivu siku ya maafa

kuyajilia mataifa yaliyotuvamia.

17Ingawa mtini hauchanui maua

na hakuna zabibu juu ya mizabibu,

ingawaje mzeituni hauzai,

na hata mashamba hayatoi chakula,

iwapo hakuna kondoo katika banda,

wala ngʼombe katika zizi,

18hata hivyo nitashangilia katika Bwana ,

nitamfurahia Mungu Mwokozi wangu.

19Bwana Mwenyezi ni nguvu yangu;

huifanya miguu yangu kama miguu ya ayala,

huniwezesha kupita juu ya vilima.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.