The chat will start when you send the first message.
1“Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda;
nilimwita mwanangu kutoka Misri.
2Lakini kadiri nilivyomwita Israeli,
ndivyo walivyoenda mbali nami.
Walitoa dhabihu kwa Mabaali
na kufukiza uvumba kwa vinyago.
3Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea,
nikiwashika mikono;
lakini hawakutambua
kuwa ni mimi niliyewaponya.
4Niliwaongoza kwa kamba za huruma ya kibinadamu,
kwa vifungo vya upendo;
niliondoa nira shingoni mwao
nami nikainama kuwalisha.
5“Je, hawatarudi Misri,
nayo Ashuru haitawatawala
kwa sababu wamekataa kutubu?
6Upanga utavurumishwa katika miji yao,
nao utaharibu makomeo ya malango yao
na kukomesha mipango yao.
7Watu wangu wamedhamiria kuniacha.
Hata wakimwita Yeye Aliye Juu Sana,
kwa vyovyote hatawainua.
8“Efraimu, ninawezaje kukuacha?
Ee Israeli, ninawezaje kukutoa?
Nitawezaje kukutendea kama Adma?
Nitawezaje kukufanya kama Seboimu?
Moyo wangu umegeuka ndani yangu,
huruma zangu zote zimeamshwa.
9Sitatimiza hasira yangu kali,
wala sitageuka na kumharibu Efraimu.
Kwa kuwa mimi ndimi Mungu,
wala si mwanadamu,
Aliye Mtakatifu miongoni mwenu.
Sitakuja kwa ghadhabu.
10Watamfuata Bwana ;
atanguruma kama simba.
Anaponguruma,
watoto wake watakuja wakitetemeka
kutoka magharibi.
11Watakuja wakitetemeka
kama ndege wakitoka Misri,
kama hua wakitoka Ashuru.
Nitawafanya waishi katika nyumba zao,”
asema Bwana .
12Efraimu amenizunguka kwa uongo,
nyumba ya Israeli kwa udanganyifu.
Naye Yuda ni mkaidi dhidi ya Mungu,
hata kinyume cha yule mwaminifu Aliye Mtakatifu.