Isaya 38

Isaya 38

Ugonjwa wa Hezekia

(2Fal 20:1‑11; 2Nya 32:24‑26)

1Katika siku hizo Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana : Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”

2Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana :

3“Ee Bwana , kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.

4Ndipo neno la Bwana likamjia Isaya, kusema:

5“Nenda ukamwambie Hezekia, ‘Hili ndilo asemalo Bwana , Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako. Nitakuongezea miaka kumi na tano katika maisha yako.

6Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu.

7“ ‘Hii ndiyo ishara ya Bwana kwako kwamba Bwana atafanya kile alichoahidi:

8Nitafanya kivuli cha jua kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi kirudi nyuma madaraja kumi.’ ” Hivyo jua likarudi nyuma madaraja kumi ambayo lilikuwa limeshuka.

9Maandiko ya Hezekia mfalme wa Yuda baada ya kuugua kwake na kupona:

10Nilisema, “Katika ustawi wa maisha yangu,

je, ni lazima nipite katika malango ya mauti,

na kupokonywa miaka yangu iliyobaki?”

11Nilisema, “Sitamwona tena Bwana ,

Bwana katika nchi ya walio hai,

wala sitamtazama tena mwanadamu,

wala kuwa na wale ambao sasa wanakaa katika ulimwengu huu.

12Kama hema la mchunga mifugo,

nyumba yangu imebomolewa na kutwaliwa kutoka kwangu.

Kama mfumaji nimevingirisha maisha yangu,

naye amenikatilia mbali kutoka kitanda cha mfumi.

Mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu.

13Nilingoja kwa uvumilivu hadi mapambazuko,

lakini alivunja mifupa yangu yote kama simba.

Mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu.

14Nililia kama mbayuwayu au korongo,

niliomboleza kama hua aombolezaye.

Macho yangu yalififia nilipotazama mbinguni.

Ee Bwana, ninataabika, njoo unisaidie!”

15Lakini niseme nini?

Amesema nami, naye yeye mwenyewe amelitenda hili.

Nitatembea kwa unyenyekevu

katika miaka yangu yote

kwa sababu ya haya maumivu makali

ya nafsi yangu.

16Bwana, kwa mambo kama haya watu huishi,

nayo roho yangu hupata uzima katika hayo pia.

Uliniponya

na kuniacha niishi.

17Hakika ilikuwa ya faida yangu

ndiyo maana nikapata maumivu makali.

Katika upendo wako ukaniokoa

kutoka shimo la uharibifu;

umeziweka dhambi zangu zote

nyuma yako.

18Kwa maana kaburi haliwezi kukusifu,[#38:18 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu ; kwa Kiebrania ni Sheol.]

mauti haiwezi kuimba sifa zako;

wale wanaoshuka shimoni

hawawezi kuutarajia uaminifu wako.

19Walio hai, walio hai: hao wanakusifu,

kama ninavyofanya leo.

Baba huwaambia watoto wao

habari za uaminifu wako.

20Bwana ataniokoa,

nasi tutaimba kwa vyombo vya nyuzi

siku zote za maisha yetu

katika Hekalu la Bwana .

21Isaya alikuwa amesema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini, mweke juu ya jipu, naye atapona.”

22Hezekia alikuwa ameuliza, “Kutakuwa na ishara gani kwamba nitapanda kwenda Hekalu la Bwana ?”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.