Waamuzi 9

Waamuzi 9

Abimeleki ajaribu kuanzisha ufalme

1Siku moja Abimeleki mwana wa Yerub-Baali akaenda kwa ndugu za mama yake huko Shekemu, akawaambia wao na ukoo wote wa mama yake,

2“Waulizeni watu wote wa Shekemu, ‘Lipi lililo bora kwenu: Kutawaliwa na wana wote sabini wa Yerub-Baali, au mtu mmoja peke yake?’ Kumbukeni kwamba mimi ni mwili wenu na damu yenu.”

3Ndugu za mama yake walipowaeleza watu wote wa Shekemu, wakaelekea kumkubali Abimeleki, kwa kuwa walisema, “Yeye ni ndugu yetu.”

4Wakampa shekeli sabini za fedha kutoka hekalu la Baal-Berithi, naye Abimeleki akazitumia kuajiri watu ovyo na wasiojali, wakawa ndio wafuasi wake.[#9:4 Shekeli 70 za fedha ni sawa na gramu 800.]

5Akaenda nyumbani mwa baba yake huko Ofra, na juu ya jiwe moja akawaua ndugu zake sabini, ambao ni wana wa Yerub-Baali. Lakini Yothamu, mwana mdogo kwa wote wa Yerub-Baali, akaokoka kwa kujificha.

6Ndipo wenyeji wa Shekemu na Beth-Milo wakakusanyika pamoja chini ya mwaloni mkubwa, penye nguzo iliyo Shekemu, wakamtawaza Abimeleki kuwa mfalme.

7Yothamu alipoambiwa hayo, akapanda juu ya kilele cha mlima Gerizimu, akapaza sauti, akawaambia, “Nisikilizeni enyi wenyeji wa Shekemu, ili Mungu naye apate kuwasikiliza.

8Siku moja miti ilitoka ili kwenda kujitawazia mfalme. Ikauambia mzeituni, ‘Wewe uwe mfalme wetu.’

9“Lakini mzeituni ukaijibu, ‘Je, niache kutoa mafuta yangu ambayo kwake miungu na wanadamu huheshimiwa, ili nikatawale miti?’

10“Kisha miti ikauambia mtini, ‘Njoo na uwe mfalme wetu!’

11“Lakini mtini ukaijibu, ‘Je, niache kutoa matunda yangu mazuri na matamu, ili nikatawale miti?’

12“Ndipo miti ikauambia mzabibu, ‘Njoo na uwe mfalme wetu.’

13“Lakini mzabibu ukaijibu, ‘Je, niache kutoa divai yangu inayofurahisha miungu na wanadamu ili nikatawale miti?’

14“Mwishoni miti yote ikauambia mchongoma, ‘Njoo na uwe mfalme wetu.’

15“Nao mchongoma ukaijibu, ‘Kama kweli mnataka kunitawaza niwe mfalme wenu, basi njooni mpate kupumzika chini ya kivuli changu. Lakini kama sivyo, moto na utoke kwenye mchongoma ukateketeze mierezi ya Lebanoni!’

16“Basi, je, mmetenda kwa uaminifu na heshima kwa kumtawaza Abimeleki kuwa mfalme? Je, mmetendea mema Yerub-Baali na jamaa yake, na mkamtendea kama alivyostahili?

17Baba yangu aliwapigania na kuhatarisha nafsi yake ili kuwaokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani,

18lakini leo mmeasi dhidi ya jamaa ya baba yangu, na kuwaua wanawe sabini juu ya jiwe moja. Nanyi mmemtawaza Abimeleki mwana wa mjakazi wake kuwa mfalme juu ya wenyeji wa Shekemu, kwa kuwa yeye ni ndugu yenu.

19Ikiwa kweli mmemtendea Yerub-Baali na jamaa yake kwa heshima na uaminifu, basi Abimeleki na awe furaha yenu, nanyi mwe furaha yake pia!

20Lakini kama sivyo, moto na utoke kwa Abimeleki na uwateketeze, ninyi wenyeji wa Shekemu na Beth-Milo; nao moto utoke kwenu, wenyeji wa Shekemu na Beth-Milo, na umteketeze Abimeleki!”

21Ndipo Yothamu akakimbia, akatoroka akaenda Beeri, akaishi huko, kwa sababu alimwogopa ndugu yake Abimeleki.

22Baada ya Abimeleki kutawala Israeli kwa muda wa miaka mitatu,

23Mungu akaruhusu roho mbaya kati ya Abimeleki na wenyeji wa Shekemu, nao wenyeji wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa hila.

24Hili lilitendeka ili ule ukatili waliotendewa hao wana sabini wa Yerub-Baali upatilizwe, na damu yao iwe juu ya Abimeleki ndugu yao aliyewaua, na pia iwe juu ya wenyeji wa Shekemu, ambao walimsaidia kuua ndugu zake.

25Hivyo, kutokana na uadui juu yake, wenyeji wa Shekemu wakaweka watu wa kumvizia katika vilele vya milima. Wakawanyangʼanya watu wote waliopita karibu nao, nayo haya yakaarifiwa kwa Abimeleki.

26Basi Gaali mwana wa Ebedi akaenda pamoja na ndugu zake wakaingia Shekemu, nao wenyeji wa huko wakawa na imani naye.

27Wakaenda mashambani mwao kuvuna zabibu na kuzisindika hizo zabibu, baadaye wakafanya sherehe katika hekalu la mungu wao. Walipokuwa wakila na kunywa, wakamlaani Abimeleki.

28Gaali mwana wa Ebedi akasema, “Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tumtumikie? Je, yeye si mwana wa Yerub-Baali? Naye Zebuli si ndiye msaidizi wake? Basi watumikieni watu wa Hamori, babaye Shekemu. Kwa nini tumtumikie Abimeleki?

29Laiti watu hawa wangekuwa chini ya amri yangu! Basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Ningemwambia Abimeleki, ‘Ondoa jeshi lako lote.’ ”

30Zebuli aliyekuwa mtawala wa mji aliposikia aliyosema Gaali mwana wa Ebedi, akakasirika sana.

31Akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, na kusema, “Gaali mwana wa Ebedi na ndugu zake wamekuja Shekemu, na wanauchochea mji huu kinyume chako.

32Sasa basi, usiku huu wewe uondoke na watu wako ili mje kuwavizia mashambani.

33Kisha asubuhi wakati wa kuchomoza jua, amka mapema na ujipange dhidi ya huo mji. Gaali na jeshi lililo pamoja naye watakapotoka kukabiliana nanyi, mwaweza kuwatendea kwa kadiri mnavyoweza.”

34Kwa hiyo Abimeleki pamoja na jeshi lake lote wakaondoka usiku na kujificha karibu na Shekemu wakiwa vikosi vinne.

35Basi Gaali mwana wa Ebedi alikuwa ametoka nje akawa amesimama katika ingilio la mji wakati ule ule ambao Abimeleki na watu wake walipokuwa wanatoka sehemu zao za maficho.

36Gaali alipowaona, akamwambia Zebuli, “Tazama, watu wanashuka kutoka vilele vya milima!”

Zebuli akajibu, “Wewe unaona vivuli vya milima kana kwamba ni watu.”

37Lakini Gaali akasema tena, “Tazama, watu wanashuka kutoka katikati ya nchi na kikosi kimoja kinakuja kutoka Tabur-Ezeri na kikosi kingine kutoka upande wa mwaloni wa Meonenimu.”

38Ndipo Zebuli akamwambia, “Kuko wapi kujivuna kwako sasa, wewe uliyesema, ‘Huyo Abimeleki ni nani hata tumtumikie?’ Hawa si wale watu uliowadharau? Toka nje sasa ukapigane nao!”

39Basi Gaali akawaongoza wenyeji wa Shekemu kupigana na Abimeleki.

40Abimeleki akamfukuza, naye akatoroka. Nao watu wengi wakaanguka njia yote hadi kwenye ingilio la lango, wakiwa wamejeruhiwa katika kule kutoroka.

41Abimeleki akaishi Aruma, naye Zebuli akawafukuza Gaali na ndugu zake watoke Shekemu.

42Kesho yake watu wa Shekemu wakatoka wakaenda mashambani, Abimeleki akaambiwa jambo hilo.

43Hivyo akawachukua watu wake, akawagawanya katika vikosi vitatu na kuwaweka waviziaji huko mashambani. Alipowaona watu wanatoka kwenda nje ya mji, akainuka dhidi yao na kuwashambulia.

44Abimeleki pamoja na vikosi vyake wakaharakisha kwenda mbele kwenye nafasi iliyokuwa katika ingilio la lango la mji. Vikosi viwili vikawashambulia wale waliokuwa mashambani, na kuwaua.

45Siku hiyo nzima Abimeleki akazidisha mashambulizi yake dhidi ya mji hadi akawa ameuteka na kuwaua watu wa mji huo. Kisha akauangamiza mji na kusambaza chumvi juu yake.

46Kwa kusikia jambo hilo, watu wote katika mnara wa Shekemu wakaingia kwenye ngome ya hekalu la El-Berithi.

47Abimeleki aliposikia kuwa wamekusanyika huko,

48yeye na watu wake wote wakakwea kwenye Mlima Salmoni. Abimeleki akachukua shoka, akakata baadhi ya matawi, ambayo aliyachukua begani mwake. Akawaagiza wale watu waliokuwa pamoja naye kuwa, “Haraka! Fanyeni kile mmeona nikifanya!”

49Basi watu wote wakakata matawi na kumfuata Abimeleki. Wakayakusanya hayo matawi juu ya ngome, na kuitia moto ili kuwachoma watu wote waliokuwa ndani. Hivyo watu wote katika mnara wa Shekemu, yamkini wanaume na wanawake elfu moja, pia wakafa.

50Baadaye Abimeleki akaenda Thebesi na kuuzingira kwa jeshi na kuuteka.

51Hata hivyo, ndani ya huo mji kulikuwa na mnara imara, ambako watu wote wa mji, wanaume na wanawake, walikimbilia ndani yake. Wakajifungia ndani, na kupanda juu ya paa la mnara.

52Abimeleki akaja kwenye ule mnara na kuushambulia. Lakini alipokaribia kwenye ingilio la mnara ili kuuchoma kwa moto,

53mwanamke mmoja akaangusha sehemu ya juu ya jiwe la kusagia kwa kichwa cha Abimeleki, likapasua fuvu la kichwa chake.

54Akamwita kwa haraka kijana yule aliyechukua silaha zake, na kumwambia, “Chukua upanga wako na uniue, watu wasije wakasema, ‘Mwanamke amemuua.’ ” Basi yule kijana akamchoma upanga, naye akafa.

55Waisraeli walipoona kuwa Abimeleki amekufa, kila mtu akaenda nyumbani mwake.

56Hivyo ndivyo Mungu alivyolipiza uovu ule ambao Abimeleki alikuwa ameutenda kwa baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini.

57Mungu akawapatiliza wanaume wa Shekemu uovu wao juu ya vichwa vyao, na juu yao ikaja laana ya Yothamu mwana wa Yerub-Baali.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.