The chat will start when you send the first message.
1Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilikuja kutoka kwa Bwana :
2“Hili ndilo asemalo Bwana : Simama katika ua wa nyumba ya Bwana na useme na watu wote wa miji ya Yuda wanaokuja kuabudu katika nyumba ya Bwana . Waambie kila kitu nitakachokuamuru, usipunguze neno.
3Huenda watasikia na kugeuka, kisha kila mmoja kutubu na kuacha njia yake mbaya. Nami nitaghairi kuleta maafa niliyopanga kufanya dhidi yao kwa sababu ya matendo yao maovu.
4Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana : Ikiwa hamtanisikiliza na kuifuata sheria yangu niliyoiweka mbele yenu,
5na msipoyasikiliza maneno ya watumishi wangu manabii, ambao nimewatuma kwenu tena na tena (ijapokuwa hamkuwasikiliza),
6ndipo nitaifanya nyumba hii kama Shilo na mji huu kuwa kitu cha kulaaniwa na mataifa yote ya dunia.’ ”
7Makuhani, manabii na watu wote wakamsikia Yeremia akiyasema maneno haya ndani ya nyumba ya Bwana .
8Lakini mara tu Yeremia alipomaliza kuwaambia watu kila kitu Bwana alichomwamuru kukisema, basi makuhani, manabii na watu wote walimkamata wakisema, “Ni lazima ufe!
9Kwa nini unatoa unabii katika jina la Bwana kwamba nyumba hii itakuwa kama Shilo na mji huu utakuwa ukiwa na kuachwa tupu?” Nao watu wote wakamkusanyikia na kumzunguka Yeremia ndani ya nyumba ya Bwana .
10Maafisa wa Yuda waliposikia kuhusu mambo haya, wakapanda kutoka jumba la kifalme, wakaenda katika nyumba ya Bwana na kushika nafasi zao kwenye ingilio la Lango Jipya la nyumba ya Bwana .
11Kisha makuhani na manabii wakawaambia maafisa pamoja na watu wote, “Mtu huyu anastahili ahukumiwe kifo kwa sababu ametoa unabii mbaya dhidi ya mji huu. Mmesikia kwa masikio yenu wenyewe!”
12Kisha Yeremia akawaambia maafisa wote na watu wote: “Bwana amenituma kutoa unabii dhidi ya nyumba hii na mji huu mambo yote mliyoyasikia.
13Sasa tengenezeni njia zenu na matendo yenu, na kumtii Bwana Mungu wenu. Ndipo Bwana atawahurumia na kuacha kuleta maafa aliyokuwa ameyatamka dhidi yenu.
14Lakini mimi niko mikononi mwenu; nifanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki.
15Hata hivyo, jueni kwa hakika, ikiwa mtaniua, kwa kumwaga damu isiyo na hatia, mtakuwa mmejipatia dhambi juu yenu wenyewe, juu ya mji huu, na juu ya wote wanaoishi ndani yake, kwa kuwa ni kweli Bwana amenituma kwenu ili niseme maneno haya masikioni mwenu.”
16Kisha maafisa na watu wote wakawaambia makuhani na manabii, “Mtu huyu asihukumiwe kifo! Amesema nasi katika jina la Bwana Mungu wetu.”
17Baadhi ya wazee wa nchi wakasogea mbele, wakaliambia kusanyiko lote la watu,
18“Mika Mmoreshethi alitoa unabii katika siku za Hezekia mfalme wa Yuda. Akawaambia watu wote wa Yuda, ‘Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi:
“ ‘Sayuni italimwa kama shamba,
Yerusalemu itakuwa lundo la kokoto,
na kilima cha Hekalu kitakuwa kichuguu
kilichofunikwa na vichaka.’
19Je, Hezekia mfalme wa Yuda au mtu mwingine yeyote katika Yuda alimhukumu Mika kufa? Je, Hezekia hakumcha Bwana na kuhitaji msaada wake? Je, Bwana hakuwahurumia na kughairi maafa aliyokuwa ametamka dhidi yao? Tunakaribia sana kujiletea maangamizi ya kutisha sisi wenyewe!”
20Wakati huu, Uria mwana wa Shemaya kutoka mji wa Kiriath-Yearimu alikuwa mtu mwingine aliyetoa unabii kwa jina la Bwana . Alitoa unabii juu ya mambo yaliyofanana na haya dhidi ya mji huu na nchi hii kama alivyofanya Yeremia.
21Mfalme Yehoyakimu na wakuu wake wote na maafisa waliposikia maneno yake, mfalme alitafuta kumuua. Lakini Uria alipata habari, na kwa kuogopa akakimbilia Misri.
22Hata hivyo, Mfalme Yehoyakimu alimtuma Elnathani mwana wa Akbori huko Misri, pamoja na watu wengine ili kwenda kumkamata Uria.
23Wakamrudisha Uria kutoka Misri na kumpeleka kwa Mfalme Yehoyakimu, ambaye alimuua kwa upanga, na mwili wake kutupwa kwenye eneo la makaburi ya watu wasio na cheo.
24Zaidi ya hayo, Ahikamu mwana wa Shafani akamuunga mkono Yeremia, kwa hiyo hakutiwa tena mikononi mwa watu ili auawe.