Yohana 21

Yohana 21

Yesu awatokea wanafunzi saba

1Baada ya haya Yesu akawatokea tena wanafunzi wake kando ya Bahari ya Tiberia. Yeye alijionesha kwao hivi:[#21:1 yaani Bahari ya Galilaya]

2Simoni Petro, Tomaso (aitwaye Didimasi), Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo, na wanafunzi wengine wawili walikuwa pamoja.[#21:2 yaani Pacha]

3Simoni Petro akawaambia wenzake, “Mimi naenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Tutaenda pamoja nawe.” Wakatoka, wakaingia ndani ya mashua, lakini usiku ule hawakupata chochote.

4Mara baada ya kupambazuka, Yesu akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Yesu.

5Yesu akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wowote?”

Wakamjibu, “La.”

6Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu, na tazama, wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua.

7Basi yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia kwamba ni Bwana, akajifunga nguo yake (kwa kuwa alikuwa ameitoa), naye akajitosa baharini.

8Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa mia mbili.[#21:8 Dhiraa 200 ni kama mita 90.]

9Walipofika ufuoni, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake, na mikate.

10Yesu akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.”

11Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu ufuoni. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa mia moja hamsini na watatu (153). Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika.

12Yesu akawaambia, “Njooni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wa wanafunzi aliyethubutu kumuuliza, “Wewe ni nani?” Walijua kuwa ni Bwana.

13Yesu akaja, akachukua ule mkate, akawapa, na vivyo hivyo akawagawia wale samaki.

14Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada yake kufufuliwa kutoka kwa wafu.

Yesu amrejesha Petro

15Walipokwisha kula, Yesu akamuuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?”

Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”

Yesu akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.”

16Yesu akamuuliza tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?”

Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”

Yesu akamwambia, “Chunga kondoo wangu.”

17Kwa mara ya tatu Yesu akamuuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?”

Petro akahuzunika sana kwa kuwa Yesu alimuuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.”

Yesu akamwambia, “Lisha kondoo wangu.

18Amin, amin nakuambia, ulipokuwa kijana ulivaa na kwenda unakotaka. Lakini utakapokuwa mzee, utanyoosha mikono yako na mtu mwingine atakuvika na kukupeleka usipotaka kwenda.”

19Yesu alisema haya ili kuashiria aina ya kifo ambacho Petro angemtukuza nacho Mungu. Kisha Yesu akamwambia Petro, “Nifuate!”

20Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akiwafuata. (Huyu ndiye yule mwanafunzi aliyeegama kifuani mwa Yesu walipokula naye chakula cha mwisho na kuuliza, “Bwana, ni nani atakayekusaliti?”)

21Petro alipomwona huyo mwanafunzi, akamuuliza Yesu, “Bwana, na huyu je?”

22Yesu akamjibu, “Ikiwa nataka aishi hadi nitakaporudi, inakuhusu nini? Wewe inakupasa unifuate!”

23Kwa sababu ya maneno haya ya Yesu, uvumi ukaenea miongoni mwa ndugu kwamba huyu mwanafunzi hangekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa hangekufa. Yeye alisema tu kwamba, “Ikiwa nataka aishi hadi nitakaporudi, inakuhusu nini?”

24Huyu ndiye yule mwanafunzi anayeshuhudia mambo haya, na ndiye ameandika habari hizi. Nasi tunajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli.

25Lakini kuna mambo mengine mengi ambayo Yesu alifanya. Kama yote yangeandikwa, nadhani hata ulimwengu wote haungekuwa na nafasi ya kutosha kuweka vitabu ambavyo vingeandikwa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.