The chat will start when you send the first message.
2Alfajiri na mapema Yesu akaja tena Hekaluni; watu wote wakakusanyika, naye akaketi, akaanza kuwafundisha.
3Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta mwanamke mmoja aliyefumaniwa akizini. Wakamsimamisha katikati ya umati wa watu wote.
4Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, huyu mwanamke amekutwa akizini.
5Katika sheria, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake wa namna hii, hadi wafe. Sasa wewe wasemaje?”
6Walimuuliza swali hili kama mtego ili wapate sababu ya kumshtaki.
Lakini Yesu akainama akaanza kuandika ardhini kwa kidole chake.
7Walipoendelea kumuulizauliza akainuka, akawaambia, “Kama kuna mtu yeyote miongoni mwenu ambaye hana dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.”
8Akainama tena na kuandika ardhini.
9Waliposikia haya, wakaanza kuondoka mmoja mmoja, wakianzia wazee, hadi Yesu akabaki peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake.
10Yesu akainuka na kumwambia, “Mwanamke, wako wapi wale waliokuwa wanakuhukumu kuwa mwenye hatia?”
11Yule mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja, Bwana.”
Yesu akamwambia, “Hata mimi sikuhukumu. Nenda zako. Kuanzia sasa usitende dhambi tena.”]
12Kisha Yesu akasema nao tena, akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata, hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”
13Mafarisayo wakamwambia, “Ushuhuda wako haukubaliki, kwa kuwa unajishuhudia mwenyewe.”
14Yesu akawajibu, “Hata kama najishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli, kwa sababu najua nilikotoka na ninakoenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakoenda.
15Ninyi mnahukumu kwa kufuata vipimo vya kibinadamu; mimi simhukumu mtu yeyote.
16Lakini hata nikihukumu, uamuzi wangu ni sahihi kwa sababu sitoi hukumu yangu peke yangu, bali niko pamoja na Baba, aliyenituma.
17Imeandikwa katika Sheria yenu kwamba ushahidi wa watu wawili ni thabiti.
18Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia.”
19Ndipo wakamuuliza, “Huyo Baba yako yuko wapi?”
Yesu akawajibu, “Ninyi hamnifahamu mimi ni nani, wala hammfahamu Baba yangu. Kama mngenifahamu mimi, mngemfahamu na Baba yangu.”
20Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika chumba cha hazina Hekaluni. Lakini hakuna mtu aliyemkamata kwa kuwa saa yake ilikuwa haijawadia.
21Yesu akawaambia tena, “Ninaenda zangu, nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kuja.”
22Ndipo wale Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Je, hii ndiyo sababu amesema, ‘Niendako mimi ninyi hamwezi kuja’?”
23Akawaambia, “Ninyi mmetoka chini; mimi nimetoka juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu; mimi si wa ulimwengu huu.
24Niliwaambia kuwa mtakufa katika dhambi zenu; kwa maana msipoamini kwamba ‘Mimi Ndiye,’ mtakufa katika dhambi zenu.”
25Wakamuuliza, “Wewe ni nani?”
Naye Yesu akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nimekuwa nikiwaambia tangu mwanzo.
26Nina mambo mengi ya kusema kuwahusu ya kuwahukumu. Lakini yeye aliyenituma ni wa kuaminika, nami nanena na ulimwengu niliyoyasikia kutoka kwake.”
27Hawakuelewa kuwa alikuwa akiwaambia kuhusu Baba yake wa Mbinguni.
28Kisha Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha kumwinua Mwana wa Adamu juu, ndipo mtajua kuwa mimi ndiye yule niliyesema, na kwamba mimi sitendi jambo lolote peke yangu, bali ninasema yale tu Baba yangu amenifundisha.
29Yeye aliyenituma yu pamoja nami; hajaniacha, kwa kuwa siku zote nafanya mapenzi yake.”
30Wengi waliomsikia Yesu akisema maneno haya wakamwamini.
31Kisha Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli.
32Ndipo mtaijua kweli, nayo kweli itawaweka huru.”
33Wao wakamjibu, “Sisi tu wazao wa Abrahamu, nasi hatujakuwa watumwa wa mtu yeyote. Wawezaje kusema kwamba tutawekwa huru?”
34Yesu akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.
35Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima.
36Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli.
37Ninajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Abrahamu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno langu.
38Ninasema yale niliyoyaona nikiwa mbele za Baba yangu, nanyi mnafanya yale mliyosikia kutoka kwa baba yenu.”
39Wakajibu, “Baba yetu ni Abrahamu.”
Yesu akawaambia, “Kama mngekuwa wazao wa Abrahamu, mngefanya mambo yale aliyofanya Abrahamu.
40Lakini sasa ninyi mnatafuta kuniua, mtu ambaye nimewaambia kweli ile niliyosikia kutoka kwa Mungu. Abrahamu hakufanya jambo la namna hii.
41Ninyi mnafanya mambo afanyayo baba yenu.”
Wakamjibu, “Sisi hatukuzaliwa kwa uzinzi. Tunaye Baba mmoja, Mungu pekee.”
42Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.
43Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho.
44Ninyi ni watoto wa baba yenu, ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli, maana hamna kweli ndani yake. Anaposema uongo, yeye husema lugha yake ya asili kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo.
45Lakini kwa sababu nimewaambia kweli, hamkuniamini!
46Je, kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini?
47Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.”
48Wayahudi wakamjibu Yesu, “Je, hatuko sahihi tunaposema kwamba wewe ni Msamaria, na kwamba una pepo mchafu?”
49Yesu akawajibu, “Mimi sina pepo mchafu, bali ninamheshimu Baba yangu, nanyi mnanidharau.
50Lakini mimi sitafuti utukufu wangu mwenyewe, bali yuko anayetaka kunitukuza, naye ndiye mwamuzi.
51Amin, amin nawaambia, mtu yeyote akilitii neno langu, hataona mauti milele.”
52Ndipo Wayahudi wakapaza sauti, wakamwambia, “Sasa tumejua kwamba una pepo mchafu! Abrahamu alikufa, na manabii vilevile, nawe unasema kuwa mtu akitii neno lako hatakufa milele.
53Je, wewe ni mkuu kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa, na manabii ambao pia walikufa? Unafikiri wewe ni nani?”
54Yesu akawajibu, “Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu hauna maana. Baba yangu, huyo ambaye ninyi mnadai kuwa ni Mungu wenu, ndiye anitukuzaye mimi.
55Ingawa hamkumjua, mimi ninamjua. Kama ningesema simjui, ningekuwa mwongo kama ninyi, lakini mimi ninamjua na ninalitii neno lake.
56Baba yenu Abrahamu alishangilia kwamba angeiona siku yangu, naye akaiona na akafurahi.”
57Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza hata miaka hamsini, nawe wasema umemwona Abrahamu?”
58Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, kabla Abrahamu hajakuwa, Mimi niko.”
59Ndipo wakaokota mawe ili kumpiga, lakini Yesu akajificha, naye akatoka Hekaluni.