The chat will start when you send the first message.
1Neno la Bwana ambalo lilimjia Yoeli mwana wa Pethueli.
2Sikilizeni hili, enyi wazee;
sikilizeni, ninyi nyote mnaoishi katika nchi.
Je, jambo kama hili lilishawahi kutokea
katika siku zenu au katika siku za babu zenu?
3Waelezeni watoto wenu,
na watoto wenu wawaambie watoto wao,
na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata.
4Kilichosazwa na kundi la tunutu
nzige wakubwa wamekula,
kilichosazwa na nzige wakubwa
parare wamekula,
kilichosazwa na parare
madumadu wamekula.
5Amkeni, enyi walevi, mlie!
Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo,
pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya,
kwa kuwa mmenyangʼanywa
kutoka midomoni mwenu.
6Taifa limevamia nchi yangu,
lenye nguvu tena lisilo na idadi;
lina meno ya simba,
magego ya simba jike.
7Limeharibu mizabibu yangu
na kuangamiza mitini yangu.
Limebambua magome yake
na kuyatupilia mbali,
likayaacha matawi yake yakiwa meupe.
8Omboleza kama bikira aliyevaa gunia
akimwomboleza mume wa ujana wake.
9Sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji
zimekatiliwa mbali kutoka nyumba ya Bwana .
Makuhani wanaomboleza,
wale wanaohudumu mbele za Bwana .
10Mashamba yameharibiwa,
ardhi imekauka;
nafaka imeharibiwa,
mvinyo mpya umekauka,
mafuta yamekoma.
11Kateni tamaa, enyi wakulima,
lieni, enyi mlimao mizabibu;
huzunikeni kwa ajili ya ngano na shayiri,
kwa sababu mavuno ya shambani yameharibiwa.
12Mzabibu umekauka
na mtini umenyauka;
mkomamanga, mtende na mtofaa,
miti yote shambani, imekauka.
Hakika furaha yote ya mwanadamu
imeondoka.
13Vaeni gunia, enyi makuhani, muomboleze;
pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni.
Njooni, vaeni gunia usiku kucha,
enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu;
kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji
zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu.
14Tangazeni saumu takatifu;
liiteni kusanyiko takatifu.
Waiteni wazee
na wote wanaoishi katika nchi
waende katika nyumba ya Bwana Mungu wenu,
wakamlilie Bwana .
15Ole kwa siku hiyo!
Kwa kuwa siku ya Bwana iko karibu;
itakuja kama uharibifu
kutoka kwa Mwenyezi.
16Je, chakula hakikukatiliwa mbali
mbele ya macho yetu:
furaha na shangwe
kutoka nyumba ya Mungu wetu?
17Mbegu zinakauka
chini ya mabonge ya udongo.
Maghala yameachwa katika uharibifu,
maghala ya nafaka yamebomolewa,
kwa maana hakuna nafaka.
18Jinsi gani ngʼombe wanavyolia!
Makundi ya mifugo yanahangaika
kwa sababu hawana malisho;
hata makundi ya kondoo yanateseka.
19Kwako, Ee Bwana , naita,
kwa kuwa moto umeteketeza
malisho ya mbugani
na miali ya moto imeunguza
miti yote shambani.
20Hata wanyama pori wanakuonea shauku;
vijito vya maji vimekauka,
na moto umeteketeza
malisho yote ya mbugani.