Yoshua 6

Yoshua 6

Yeriko yaangamizwa

1Basi malango ya Yeriko yalifungwa kwa uthabiti kwa sababu ya Waisraeli. Hakuna mtu yeyote aliyetoka au kuingia.

2Kisha Bwana akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na wapiganaji wake.

3Zunguka mji mara moja pamoja na watu wote wenye silaha. Fanya hivi kwa siku sita.

4Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo dume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo.

5Utakapowasikia wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na wapiganaji watapanda, kila mtu akielekea mbele yake.”

6Ndipo Yoshua mwana wa Nuni akaita makuhani na kuwaambia, “Chukueni Sanduku la Agano la Bwana na makuhani saba wachukue baragumu za pembe za kondoo dume mbele yake.”

7Naye akawaagiza watu, “Songeni mbele! Mkauzunguke mji, na walinzi wenye silaha watangulie mbele ya Sanduku la Bwana .”

8Baada ya Yoshua kuzungumza na watu, wale makuhani saba waliozibeba zile baragumu saba mbele za Bwana , wakatangulia mbele, wakipiga baragumu zao na Sanduku la Agano la Bwana likawafuata.

9Walinzi waliokuwa na silaha wakaenda mbele ya hao makuhani waliopiga hizo baragumu na hao walinzi wa nyuma wakafuata Sanduku. Wakati wote huu baragumu zilikuwa zikipigwa.

10Bali Yoshua alikuwa amewaagiza watu, “Msipige ukelele wa vita; msipaze sauti zenu, wala kusema neno lolote hadi siku ile nitakayowaambia mpige kelele. Ndipo mtapiga kelele!”

11Basi akalipeleka Sanduku la Bwana kuzungushwa huo mji, likizungushwa mara moja. Kisha watu wakarudi kambini kulala.

12Yoshua akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, nao makuhani wakalichukua Sanduku la Bwana .

13Wale Makuhani saba waliobeba zile baragumu saba wakatangulia mbele ya Sanduku la Bwana wakizipiga. Watu wenye silaha wakatangulia mbele yao na walinzi wa nyuma wakalifuata Sanduku la Bwana , huku baragumu hizo zikiendelea kulia.

14Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja na kurudi kambini. Wakafanya hivi kwa siku sita.

15Siku ya saba, wakaamka asubuhi na mapema wakauzunguka mji kama walivyokuwa wakifanya, isipokuwa siku ile waliuzunguka mji mara saba.

16Walipouzunguka mara ya saba, makuhani walipiga baragumu kwa sauti kubwa, naye Yoshua akawaamuru watu akisema, “Pigeni kelele! Kwa maana Bwana amewapa mji huu!

17Mji huu pamoja na vyote vilivyomo utatengewa Bwana kwa ajili ya kuangamizwa. Rahabu yule kahaba atasalimishwa, pamoja na wote walio naye nyumbani mwake, kwa sababu aliwaficha wale wapelelezi tuliowatuma.

18Lakini mjiepushe na vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, msije mkajiletea maangamizi kwa kuchukua chochote katika hivyo; la sivyo, mtailetea kambi ya Israeli maangamizi na taabu.

19Fedha yote na dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa Bwana , lazima viletwe katika hazina yake.”

20Baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele; kwa ile sauti ya baragumu na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akapanda akiendelea mbele na kuuteka mji.

21Wakauweka mji wakfu kwa Bwana , na kila chenye uhai ndani yake walikiangamiza kwa upanga: wanaume na wanawake, vijana kwa wazee, ngʼombe, kondoo na punda.

22Yoshua akawaambia wale watu wawili waliokuwa wameipeleleza nchi, “Nendeni nyumbani mwa yule kahaba; mleteni pamoja na wote walio nyumbani mwake, kulingana na kiapo chenu kwake.”

23Basi wale vijana waliofanya upelelezi wakaenda kumleta Rahabu, baba yake na mama yake, na ndugu zake na watu wote waliokuwa pamoja naye. Wakaleta jamaa yake yote na kuwaweka mahali nje ya kambi ya Israeli.

24Kisha wakauchoma mji wote na kila kitu kilichokuwa ndani yake. Lakini fedha, dhahabu, na vyombo vya shaba na vya chuma wakaviweka katika hazina ya nyumba ya Bwana .

25Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu yule kahaba, jamaa yake yote na vyote alivyokuwa navyo, kwa sababu aliwaficha watu waliotumwa na Yoshua kuipeleleza Yeriko, naye anaishi miongoni mwa Waisraeli hata leo.

26Wakati ule Yoshua akatamka kiapo hiki akasema, “Na alaaniwe mbele za Bwana mtu atakayeinuka kuujenga tena mji huu wa Yeriko:

“Kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza wa kiume

ataiweka misingi yake;

kwa gharama ya mtoto wake wa mwisho

atayaweka malango yake.”

27Hivyo Bwana alikuwa pamoja na Yoshua, na sifa zake zikaenea katika nchi yote.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.