The chat will start when you send the first message.
1Neno la unabii: Neno la Bwana kwa Israeli kupitia kwa Malaki.
2Bwana asema, “Nimewapenda ninyi.
“Lakini ninyi mnauliza, ‘Wewe umetupendaje?’ ”
Bwana asema, “Je, Esau hakuwa ndugu yake Yakobo? Hata hivyo nimempenda Yakobo,
3lakini nikamchukia Esau, nami nimeifanya nchi yake ya vilima kuwa ukiwa, na urithi wake nimewapa mbweha wa jangwani.”
4Edomu anaweza kusema, “Ingawa tumepondapondwa, tutajenga upya magofu.”
Lakini hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi: “Wanaweza kujenga, lakini nitabomoa. Wataitwa Nchi Ovu, watu ambao siku zote wapo chini ya ghadhabu ya Bwana .
5Mtayaona kwa macho yenu wenyewe na kusema, ‘Bwana ni mkuu, hata nje ya mipaka ya Israeli!’
6“Mwana humheshimu baba yake, naye mtumishi humheshimu bwana wake. Kama mimi ni baba, iko wapi heshima ninayostahili? Kama mimi ni bwana, iko wapi heshima ninayostahili?” asema Bwana wa majeshi. “Ni ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau Jina langu.
“Lakini mnauliza, ‘Tumelidharau Jina lako kwa namna gani?’
7“Mnatoa sadaka chakula kilichotiwa unajisi juu ya madhabahu yangu.
“Lakini ninyi mnauliza, ‘Tumekutia unajisi kwa namna gani?’
“Kwa kusema kuwa meza ya Bwana ni ya kudharauliwa.
8Mnapoleta dhabihu za wanyama walio vipofu, je, hilo si kosa? Mnapoleta dhabihu zilizo vilema au wanyama wagonjwa, je, hilo si kosa? Jaribuni kuvitoa kwa mtawala wenu! Je, angefurahishwa nanyi? Je, atawakubalia?” asema Bwana wa majeshi.
9“Basi mwombeni Mungu awe na neema kwetu. Je, kwa sadaka kama hizo kutoka mikononi mwenu, atawapokea?” asema Bwana wa majeshi.
10“Laiti mmoja wenu angeifunga milango ya Hekalu, ili msije mkawasha moto usiokuwa na faida juu ya madhabahu yangu! Sina furaha nanyi,” asema Bwana wa majeshi, “nami sitaikubali sadaka toka mikononi mwenu.
11Jina langu litakuwa kuu miongoni mwa mataifa, kuanzia mawio ya jua hata machweo yake. Kila mahali uvumba na sadaka safi zitaletwa kwa Jina langu, kwa sababu Jina langu litakuwa kuu miongoni mwa mataifa,” asema Bwana wa majeshi.
12“Lakini mnalinajisi Jina langu kwa kusema kuhusu meza ya Bwana, ‘Imetiwa unajisi pamoja na chakula chake. Ni ya kudharauliwa.’
13Nanyi mnasema, ‘Mzigo gani huu!’ Nanyi mnaidharau kwa kiburi,” asema Bwana wa majeshi.
“Mnapowaleta wanyama mliopokonya kwa nguvu, walio vilema au walio wagonjwa na kuwatoa kama dhabihu, je, niwakubali kutoka mikononi mwenu?” asema Bwana .
14“Amelaaniwa yeye adanganyaye, aliye na mnyama wa kiume anayekubalika katika kundi lake na kuweka nadhiri ya kumtoa, lakini akatoa dhabihu ya mnyama aliye na dosari kwa Bwana . Kwa kuwa mimi ni Mfalme Mkuu, nalo Jina langu linapaswa kuogopwa miongoni mwa mataifa,” asema Bwana wa majeshi.