The chat will start when you send the first message.
1“Angalieni, nitamtuma mjumbe wangu, atakayeiandaa njia mbele yangu. Ndipo ghafula Bwana mnayemtafuta atakuja hekaluni mwake. Mjumbe wa agano, ambaye mnamwonea shauku, atakuja,” asema Bwana wa majeshi.
2Lakini ni nani atakayeweza kustahimili hiyo siku ya kuja kwake? Ni nani awezaye kusimama atakapotokea? Kwa kuwa atakuwa kama moto wa mfua fedha au kama sabuni ya mfua nguo.
3Ataketi kama mfuaji na asafishaye fedha. Atawatakasa Walawi, naye atawasafisha kama dhahabu na fedha. Kisha Bwana atakuwa na watu watakaoleta sadaka katika haki,
4nazo sadaka za Yuda na Yerusalemu zitakubalika kwa Bwana , kama katika siku zilizopita, kama katika miaka ya zamani.
5“Basi nitakuja karibu nanyi ili kuhukumu. Nami nitakuwa mwepesi kushuhudia dhidi ya wachawi, wazinzi, waapao kwa uongo, wanaopunja vibarua malipo yao, wanaowadhulumu wajane na yatima, na wanaowanyima wageni haki, lakini hawaniogopi mimi,” asema Bwana wa majeshi.
6“Mimi Bwana sibadiliki. Kwa hiyo ninyi, enyi uzao wa Yakobo, hamjaangamizwa.
7Tangu wakati wa baba zenu mmegeukia mbali na amri zangu nanyi hamkuzishika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi,” asema Bwana wa majeshi.
“Lakini mnauliza, ‘Tutarudi kwa namna gani?’
8“Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia mimi.
“Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’
“Mnaniibia zaka na dhabihu.
9Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi.
10Leteni zaka kamili ghalani, ili kuwe na chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema Bwana wa majeshi, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi hata mkose nafasi ya kutosha.
11Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu, wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake,” asema Bwana wa majeshi.
12“Ndipo mataifa yote yatawaita mliobarikiwa, kwa maana nchi yenu itakuwa ya kupendeza sana,” asema Bwana wa majeshi.
13“Mmesema vitu vigumu dhidi yangu,” asema Bwana .
“Hata hivyo mnauliza, ‘Tumesema nini dhidi yako?’
14“Mmesema, ‘Ni bure kumtumikia Mungu. Tumepata faida gani kwa kushika maagizo yake na kwenda kama waombolezaji mbele za Bwana wa majeshi?
15Lakini sasa wenye kiburi wanabarikiwa. Hakika watenda maovu wanastawi, pia hata wale wanaoshindana na Mungu ndio wanaosalimika.’ ”
16Ndipo wale waliomcha Bwana wakasemezana wao kwa wao, naye Bwana akasikiliza na akasikia. Kitabu cha kumbukumbu kikaandikwa mbele yake kuhusu wale ambao walimcha Bwana na kuliheshimu jina lake.
17“Nao watakuwa watu wangu,” asema Bwana wa majeshi, “katika siku ile nitakapowafanya kuwa hazina yangu ya pekee. Nitawahurumia, kama vile kwa huruma mtu amhurumiavyo mwanawe anayemtumikia.
18Kwa mara nyingine tena utaona tofauti kati ya wenye haki na waovu, kati ya wale wanaomtumikia Mungu na wale wasiomtumikia.