Marko 3

Marko 3

Yesu amponya mtu aliyepooza mkono

(Mt 12:9‑14; Lk 6:6‑11)

1Yesu akaingia tena ndani ya sinagogi, na kulikuwa na mtu aliyepooza mkono.

2Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya huyo mtu siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki.

3Yesu akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele ya watu wote.”

4Kisha Yesu akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato: Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza.

5Yesu akawatazama kwa hasira watu waliomzunguka pande zote, akahuzunika sana kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukawa umeponywa kabisa!

6Kisha Mafarisayo wakatoka nje, nao wakaanza kufanya njama ya kumuua Yesu wakishirikiana na Maherode.

Makundi ya watu wamfuata Yesu

7Yesu na wanafunzi wake wakaondoka huko, wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya wakamfuata.

8Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, makundi ya watu wakamjia kutoka Yudea, Yerusalemu, Idumaya, na ngʼambo ya Yordani, pamoja na wale wa maeneo ya Tiro na Sidoni.

9Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake watayarishe mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga.

10Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa.

11Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”

12Lakini aliwaonya wasiwaambie wengine kumhusu.

Yesu achagua mitume kumi na wawili

(Mt 10:1‑4; Lk 6:12‑16)

13Yesu akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia.

14Akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume, ili wapate kuwa naye, na awatume kwenda kuhubiri

15na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu.

Simoni (ambaye alimwita Petro);

17Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo);

18Andrea,

Filipo,

Bartholomayo,

Mathayo,

Tomaso,

Yakobo mwana wa Alfayo,

Thadayo,

Simoni Mkananayo,

19na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.

Yesu na Beelzebuli

(Mt 12:22‑32; Lk 11:14‑23)

20Kisha Yesu alipoingia ndani ya nyumba, umati wa watu wakakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula.

21Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”

22Walimu wa sheria walioteremka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli! Anatoa pepo wachafu kwa nguvu ya mkuu wa pepo wachafu!”[#3:22 kwa Kiyunani ni Beelzebubu , yaani mkuu wa pepo wachafu]

23Basi Yesu akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani?

24Kama ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama.

25Nayo nyumba ikigawanyika dhidi yake yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama.

26Na kama Shetani akijipinga mwenyewe na awe amegawanyika, hawezi kusimama, bali mwisho wake umetimia.

27Hakuna mtu yeyote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali yake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu. Ndipo ataweza kuteka nyara mali yake.

28Amin, nawaambia, watu wataweza kusamehewa dhambi na kufuru zao zote;

29lakini yeyote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”

30Yesu alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”

Mama yake na ndugu zake Yesu

(Mt 12:46‑50; Lk 8:19‑21)

31Kisha wakaja ndugu zake Yesu pamoja na mama yake. Wakiwa wamesimama nje, wakamtuma mtu kumwita.

32Umati wa watu walikuwa wameketi kumzunguka, nao wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”

33Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”

34Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu.

35Mtu yeyote anayetenda mapenzi ya Mungu, huyo ndiye kaka yangu, na dada yangu, na mama yangu.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.