The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Musa,
2“Sema na Haruni umwambie, ‘Utakapoziweka zile taa saba, zinatakiwa kuangaza eneo lililo mbele ya kinara cha taa.’ ”
3Haruni akafanya hivyo; akaziweka zile taa ili zielekee mbele kwenye kinara cha taa, kama vile Bwana alivyomwamuru Musa.
4Hivi ndivyo kinara cha taa kilivyotengenezwa: Kilitengenezwa kwa dhahabu iliyofuliwa, kuanzia kwenye kitako chake hadi kwenye maua yake. Kinara cha taa kilitengenezwa sawasawa kabisa na kielelezo ambacho Bwana alikuwa amemwonesha Musa.
5Bwana akamwambia Musa:
6“Watwae Walawi kutoka miongoni mwa Waisraeli wengine na uwatakase.
7Ili kuwatakasa, fanya hivi: Nyunyizia maji ya utakaso juu yao; kisha uwaambie wanyoe nywele kwenye mwili mzima, wafue nguo zao na hivyo wajitakase wenyewe.
8Waambie wamchukue fahali mchanga pamoja na sadaka yake ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta; kisha utamchukua fahali mchanga wa pili kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
9Walete Walawi mbele ya Hema la Kukutania na ukusanye jumuiya yote ya Waisraeli.
10Utawaleta Walawi mbele za Bwana , na Waisraeli wataweka mikono yao juu ya Walawi.
11Haruni atawaweka Walawi mbele za Bwana wawe sadaka ya kuinuliwa kutoka kwa Waisraeli, ili wawe tayari kuifanya kazi ya Bwana .
12“Baada ya Walawi kuweka mikono yao juu ya vichwa vya hao mafahali wawili, tumia mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi kwa Bwana , na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi.
13Waambie hao Walawi wasimame mbele ya Haruni na wanawe, kisha wawatoe wawe sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana .
14Kwa njia hii utakuwa umewatenga Walawi kutoka kwa Waisraeli wengine, nao Walawi watakuwa wangu.
15“Utakapokuwa umekwisha kuwatakasa Walawi na kuwatoa wawe sadaka ya kuinuliwa, watakuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania.
16Wao ndio Waisraeli ambao watatolewa kabisa kwangu. Nimewatwaa kama mali yangu mwenyewe badala ya mzaliwa wa kwanza, mzaliwa wa kwanza wa kiume kutoka kwa kila mwanamke Mwisraeli.
17Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume katika Israeli, awe wa mwanadamu au mnyama, ni wangu. Nilipowaua wazaliwa wote wa kwanza huko Misri, niliwatenga kwa ajili yangu mwenyewe.
18Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wote wa kwanza wa kiume katika Israeli.
19Kati ya Waisraeli wote, nimempa Haruni na wanawe Walawi kama zawadi ili wafanye kazi katika Hema la Kukutania kwa niaba ya Waisraeli, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili pasiwepo na pigo lolote litakalowapata Waisraeli wakati watakapokaribia mahali patakatifu.”
20Musa, Haruni na jumuiya yote ya Waisraeli wakawafanyia Walawi kama Bwana alivyomwamuru Musa.
21Walawi wakajitakasa wenyewe na wakafua nguo zao. Kisha Haruni akawasogeza mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili kuwatakasa.
22Baada ya hayo, Walawi walikuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania chini ya usimamizi wa Haruni na wanawe. Waliwafanyia Walawi kama vile Bwana alivyomwamuru Musa.
23Bwana akamwambia Musa,
24“Hili linawahusu Walawi: Wanaume wenye umri wa miaka ishirini na tano au zaidi watakuja kushiriki katika kazi kwenye Hema la Kukutania,
25lakini watakapofika umri wa miaka hamsini, ni lazima waache kazi zao za kawaida wala wasiendelee.
26Wanaweza kuwasaidia ndugu zao kufanya wajibu wao katika Hema la Kukutania, lakini wao wenyewe kamwe hawatafanya hiyo kazi. Basi, hivi ndivyo utakavyogawa wajibu kwa Walawi.”