The chat will start when you send the first message.
1Kwa Bwana ninakimbilia.
Unawezaje basi kuniambia:
“Ruka kama ndege utorokee kwenye mlima wako.
2Hebu tazama, waovu wanapinda nyuta zao;
wanaweka mishale kwenye nyuzi zake
ili wakiwa gizani, wawapige
walio wanyofu wa moyo.
3Wakati misingi imeharibiwa,
mwenye haki anaweza kufanya nini?”
4Bwana yuko ndani ya Hekalu lake takatifu;
Bwana yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni.
Huwaangalia wana wa watu,
macho yake yanawachunguza.
5Bwana huwachunguza wenye haki,
lakini nafsi yake inachukia waovu
na wale wanaopenda mapigano.
6Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali
na kiberiti kinachowaka;
upepo wenye joto kali ndio fungu lao.
7Kwa kuwa Bwana ni mwenye haki,
yeye hupenda haki.
Wanyofu watauona uso wake.