The chat will start when you send the first message.
1Kwa nini mataifa wanashauriana kufanya mabaya,
na makabila ya watu kula njama bure?
2Wafalme wa dunia wanajipanga
na watawala wanajikusanya
dhidi ya Bwana
na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake.
3Wanasema, “Tuvunje minyororo yao
na kuvitupilia mbali vifungo vyao.”
4Yeye anayetawala mbinguni hucheka,
Bwana huwadharau.
5Kisha huwakemea katika hasira yake
na kuwaogopesha katika ghadhabu yake, akisema,
6“Nimemtawaza Mfalme wangu
juu ya Sayuni,
mlima wangu mtakatifu.”
7Nitatangaza amri ya Bwana :
Yeye aliniambia, “Wewe ni Mwanangu;
leo mimi nimekuwa Baba yako.
8Niombe, nami nitayafanya mataifa
kuwa urithi wako,
na miisho ya dunia kuwa milki yako.
9Utawapondaponda kwa fimbo ya chuma,
na kuwavunjavunja kama chombo cha mfinyanzi.”
10Kwa hiyo, ninyi wafalme, kuweni na hekima;
mwonyeke, enyi watawala wa dunia.
11Mtumikieni Bwana kwa hofu
na mshangilie kwa kutetemeka.
12Mbusu Mwana, asije akakasirika
nawe ukaangamizwa katika njia yako,
kwa maana hasira yake inaweza kuwaka ghafula.
Heri wote wanaomkimbilia.