Zaburi 21

Zaburi 21

Zaburi 21

Shukrani kwa Mungu kwa ajili ya ushindi

1Ee Bwana , mfalme huzifurahia nguvu zako.

Tazama jinsi furaha yake ilivyo kuu

kwa ushindi unaompa!

2Umempa haja ya moyo wake

na hukumzuilia maombi ya midomo yake.

3Ulimkaribisha kwa baraka tele

na kumvika taji la dhahabu safi kichwani pake.

4Alikuomba maisha, nawe ukampa,

wingi wa siku milele na milele.

5Kutokana na ushindi uliompa, utukufu wake ni mkubwa,

umeweka juu yake fahari na utukufu.

6Hakika umempa baraka za milele,

umemfanya awe na furaha

kwa shangwe ya uwepo wako.

7Kwa kuwa mfalme anamtumaini Bwana ;

kwa upendo usiokoma wa Aliye Juu Sana hatatikiswa.

8Mkono wako utawashika adui zako wote,

mkono wako wa kuume utawakamata adui zako.

9Wakati utajitokeza,

utawafanya kama tanuru la moto.

Katika ghadhabu yake Bwana atawameza,

moto wake utawateketeza.

10Utawaangamiza wazao wao kutoka duniani,

uzao wao kutoka wanadamu.

11Ingawa watapanga mabaya dhidi yako

na kutunga hila, hawawezi kufanikiwa,

12kwa kuwa utawafanya wakimbie

utakapowalenga usoni pao

kwa mshale kutoka upinde wako.

13Ee Bwana , utukuzwe katika nguvu zako,

tutaimba na kusifu nguvu zako.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.