The chat will start when you send the first message.
1Ee Bwana , usinikemee katika hasira yako,
wala kuniadhibu katika ghadhabu yako.
2Kwa kuwa mishale yako imenichoma,
na mkono wako umenipiga.
3Hakuna afya mwilini mwangu
kwa sababu ya ghadhabu yako,
mifupa yangu haina uzima
kwa sababu ya dhambi zangu.
4Maovu yangu yamenifunika
kama mzigo mzito mno.
5Majeraha yangu yameoza na yananuka,
kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu.
6Nimeinamishwa chini na kushushwa sana,
mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.
7Viuno vyangu vimejaa maumivu yaunguzayo,
hakuna afya mwilini mwangu.
8Nimedhoofika na kupondwa kabisa,
nasononeka kwa maumivu makuu ya moyoni.
9Ee Bwana, yote ninayoyaonea shauku
yako wazi mbele zako,
kutamani kwangu sana
hakufichiki mbele zako.
10Moyo wangu unapigapiga,
nguvu zangu zimeniishia;
hata macho yangu yametiwa giza.
11Rafiki na wenzangu wananikwepa
kwa sababu ya majeraha yangu;
majirani wangu wanakaa mbali nami.
12Wale wanaotafuta uhai wangu
wanatega mitego yao,
wale ambao wangetaka kunidhuru
huongea kuhusu maangamizi yangu;
hupanga hila mchana kutwa.
13Mimi ni kama kiziwi, asiyeweza kusikia,
ni kama bubu, asiyeweza kufungua kinywa chake;
14nimekuwa kama mtu asiyesikia,
ambaye kinywa chake hakiwezi kutoa jibu.
15Ee Bwana , ninakungojea wewe,
Ee Bwana Mungu wangu, utajibu.
16Kwa kuwa nilisema, “Usiwaache wafurahie,
wala wajitukuze juu yangu
mguu wangu unapoteleza.”
17Kwa maana ninakaribia kuanguka,
na maumivu yangu yananiandama siku zote.
18Naungama uovu wangu,
ninataabishwa na dhambi yangu.
19Wengi wamekua adui zangu bila sababu;
wale wanaonichukia bure ni wengi.
20Wanaolipa wema wangu kwa maovu
hunisingizia ninapofuata lililo jema.
21Ee Bwana , usiniache,
usiwe mbali nami, Ee Mungu wangu.
22Ee Bwana Mwokozi wangu,
uje upesi kunisaidia.