Zaburi 46

Zaburi 46

Zaburi 46

Mungu yuko pamoja nasi

1Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,

msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.

2Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa,

na milima ianguke kilindini cha bahari,

3hata maji yake yakinguruma na kuumuka,

na milima itetemeke kwa mawimbi yake.

4Kuna mto ambao vijito vyake vinaufurahisha mji wa Mungu,

mahali patakatifu ambako Aliye Juu Sana anaishi.

5Mungu yuko katikati yake, hautaanguka,

Mungu atausaidia asubuhi na mapema.

6Mataifa yanafanya ghasia, falme zinaanguka,

yeye hupaza sauti yake, dunia ikayeyuka.

7Bwana wa majeshi yu pamoja nasi;

Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

8Njooni mkaone kazi za Bwana

jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.

9Anakomesha vita hata miisho ya dunia,

anakata upinde na kuvunjavunja mkuki,

anateketeza ngao kwa moto.

10“Tulieni, mjue kwamba mimi ndimi Mungu;

nitatukuzwa katikati ya mataifa,

nitatukuzwa katika dunia.”

11Bwana wa majeshi yu pamoja nasi;

Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.